Jinsi kamera zinavyozidi kudhibiti wezi majumbani

Muktasari:

  • Baada ya waporaji wa Goba kunaswa na kamera za ulinzi zilizofungwa, sasa wahalifu wanaziona kama kituo cha polisi, huku watu wengi wakiona umuhimu wa kuzifunga. Wataalamu Tehama wataja faida nne za kufunga kamera hizi zinazowasaidia makachero pia kupata ushahidi wanaoutaka. DCI Kingai atoa ushauri.

Dar/Moshi. Matukio ya wahalifu kunaswa katika kamera za usalama (CCTV) na video kuvisaidia vyombo vya uchunguzi kuwabaini kisha kuwanasa, yamechochea kasi ya ufungaji wake nchini.

Wataalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) wametaja faida nne za kufunga kamera za CCTV kuwa zinasaidia kubaini matukio na wahalifu, kuvirahisishia vyombo vya usalama katika upelelezi, kusaidia kuzuia uhalifu na kutunza kumbukumbu muhimu za eneo husika.

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Ramadhan Kingai alisema CCTV ni kifaa muhimu katika ulinzi na hurahisisha upelelezi pale mhalifu au wahalifu wanapofanikiwa kutenda uhalifu katika eneo husika, hivyo ni muhimu wengi wakazifunga.

Mbali na DCI kuhamasisha wafanyabiashara, taasisi na watu binafsi kufunga kamera za CCTV majumbani au ofisini mwao, alishauri kifaa kinachotunza kumbukumbu (DVR) kifungwe mbali na kisifikike kwa urahisi ili isiwe rahisi kwa wahalifu kukiharibu.

Tukio la Januari 7 la watu watatu wakiwa na bunduki ya kivita aina ya AK-47 kunaswa kwenye kamera wakati wanapora huko Goba jijini Dar es Salaam, ni moja ya matukio yaliyowaamsha Watanzania juu ya umuhimu wa kamera hizo.

Ni kupitia video hizo za CCTV, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alitangaza Jeshi la Polisi kufanikiwa kuwatia mbaroni wahalifu waliokuwa wakionekana kwenye kumbukumbu za kamera hizo.

Video za tukio hilo zilisambaa kwa kasi katika mitandao ya kijamii ikiwamo Twitter, Whatsapp, Facebook, Instagram na Youtube na kuzua taharuki ambazo zilizimwa na Jeshi la Polisi baada ya kuwanasa watuhumiwa hao.

Tukio jingine lililowahi kunaswa ni la usiku wa Oktoba 27 mwaka 2020, ambapo genge la watu wenye silaha walikwenda Hoteli ya Protea Aishi iliyopo Hai mkoani Kilimanjaro kumsaka Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe.

Kundi hilo likiwa na magari ambayo baadhi yalikuwa na namba za usajili zinazofanana na zinazotumiwa na magari ya Umoja wa Mataifa (UN), lilinaswa na kamera za CCTV wakifungua geti na kuwateka walinzi wa hoteli hiyo, kuwapora silaha na kuondoka nao.

Tukio jingine ni la mtu aliyefungua gari la mwandishi wa Star TV mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, Rodrick Mushi na kuiba begi lililokuwa na vitu mbalimbali ikiwamo kamera, power bank na kompyuta mpakato, tukio ambalo lilinaswa vizuri na kamera hizo za usalama.

Matukio ya uhalifu yanayonaswa katika kamera za CCTV kwa sasa na kusambazwa katika mitandao ya kijamii yanaongezeka na wataalamu wa Tehama wanasema hiyo inathibitisha maeneo mengi zaidi yamefungwa CCTV.

Aidha, kuna matukio mengine yamekuwa yakiripotiwa na Jeshi la Polisi kutoka mikoa mbalimbali nchini ya kukamatwa vitu vilivyoibwa maeneo tofauti. Baadhi ni vifaa vinavyokamatwa ni vipuri vya magari, simu, televisheni za kisasa, redio, pikipiki na fedha huku wamiliki wakiitwa kwenda kuvitambua ili wavichukue.


Wataalamu wa Tehama

Mtaalamu wa Tehama wa kampuni ya Smart IT ya mjini Moshi, Emanuel Makumulu alisema utandawazi na kukua kwa teknolojia kumesababisha kuibuka kwa vifaa vya kisasa zikiwamo kamera za CCTV kwa ajili ya kufuatilia masuala tofauti yakiwa ya usalama.

“Kamera za CCTV ndio habari ya mjini kwa sasa kwa sababu hata wezi wakifahamu nyumba imefungwa hizo kamera watafikiria mara mbilimbili kupita hapo. Kwa hiyo faida mojawapo ni hiyo kwamba zinazuia wizi,” alisema Makumulu.

Mtaalamu huyo alieleza faida nyingine ni kubaini tukio na wahalifu waliolitenda, kuvirahisishia vyombo vya usalama katika upelelezi kupitia video zinazotunza taarifa za siku nzima, kuzuia uhalifu na kutunza kumbukumbu muhimu za matukio yaliyotokea.

Makumulu, ambaye ameshafunga kamera za CCTV katika taasisi, biashara na nyumba za makazi kwenye mikoa tofauti, ikiwamo Dar es Salaam, Njombe, Iringa, Kilimanjaro, Manyara, Singida na Morogoro, alisema bei na uwezo wa kamera hizo hutofautiana.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya,Ulrich Matei akionyesha vitu mbalimbali vilivyoibwa majumbani ikiwemo TV na komputa baada ya jeshi hilo kufanya msako na kuwakamata watuhumiwa mbalimbali kabla awajaenda kuuza kwa watu,  mkoani humo Septemba, mwaka 2020. Picha na Maktaba

“Kuna seti ya kamera nne, nane, 16 na 32 na zinatofautiana kulingana na ubora. Nyingi zinazofungwa kwenye nyumba na biashara zina ukubwa wa megapixel mbili. Hata rangi hutofautiana, kuna zinazotoa picha za 2 black & white (nyeusi na nyeupe),” alisema mtaalamu huyo.

Makamulu alisema uwezo wa kamera kutunza picha unategemea ukubwa wa kifaa kinachotunza kumbukumbu (disk) kwani chenye GB 500 kinaweza kutunza taarifa zilizorekodiwa mpaka kwa kati ya wiki mbili hadi tatu mfululizo.

Kwa mujibu wa Makumulu, kwa seti yenye kamera nne ambayo ni black and white inaweza kugharimu hadi Sh850,000 pamoja na ufundi, lakini ile inayotoa picha za rangi (full colored) inaweza kugharimu mteja Sh1 milioni.

Kwa upande wake, mtaalamu wa Tehama wa kampuni ya JK Take Solution ya jijini Dar es Salaam, Jovin Kadutu alisema ufungaji wa kamera za CCTV unategemea eneo na mara nyingi inashauriwa zifungwe zikitizamana.

“Hii maana yake ni kwamba kama kamera moja haikupata vizuri hilo tukio basi kamera ya pili itakuwa imelipata. Teknolojia imekua sana, unaweza kuwa na CCTV nyumbani na umesafiri labda upo Mwanza na ukaona kinachoendelea nyumbani kwako au ofisini kwenye simu,” alisema na kuongeza:

“Hizi gharama za kufunga (CCTV) wala sio kubwa kulinganisha na faida zake katika masuala ya uhalifu. Kama ni mfanyabiashara huwezi kuwa sehemu moja wakati wote, lakini ukiwa na kamera za CCTV ukitoka ukirudi unatizama matukio yote.”

Kutokana na umuhimu wa kamera hizo katika masuala ya usalama, Kadutu anasema ndio maana hakuna benki nchini isiyokuwa na vifaa hivyo na sasa supermarkets nyingi pamoja na maduka nako wamefunga, achilia mbali nyumba za kuishi.

Mtaalamu mwingine wa kampuni ya PC Point ya jijini Dar es Salaam, Hussein Mfinanga alisema kutokana na kukua kwa teknolojia, hivi sasa kuna kamera ndogo za CCTV zinazolingana na bolti ndogo kiasi ikifungwa si rahisi mtu kuiona.

“Nimewafungia wengi hizi. Unakuta amefunga hizi Dome CCTV Cameras au hizi C-Mount CCTV ambazo zina uwezo wa kudaka kitu mpaka umbali wa futi 40 lakini anataka na hizi zenye jicho la size (ukubwa) ya bolti ili wahalifu wasizione,” alisema.


Ushauri wa DCI

Akizungumza na gazeti hili, DCI Kingai aliwashauri wafanyabiashara, taasisi na watu binafsi kwenye makazi yao kufunga kamera za CCTV, kwani mbali na kusaidia masuala ya ulinzi, huliwezesha Jeshi la Polisi kufanikisha upelelezi haraka.

“Kwanza nashukuru sana kwa hili wazo la ulinzi shirikishi ambao gazeti la Mwananchi mmeamua kufanya kuhamasisha matumizi ya kamera za CCTV katika sehemu za biashara, taasisi hata kwenye makazi ya watu. Ni jambo muhimu sana,” alisema.

DCI Kingai alisema uhalifu unatokea mahala popote, kwa hiyo kamera za CCTV ni nyezo muhimu inayosaidia na kurahisisha utambuzi wa watu wanaofanya jambo fulani kwenye eneo husika. Hata makachero wa jeshi hilo, alisema huwasaidia katika uchunguzi wa matukio yenye utata wa wahusika.

“Sio tu kwamba kamera hizi zinawatisha wezi wasisogelee eneo, ila hata wakifanikiwa kusogea na kutenda uhalifu sisi yanapokuwa yamefanyika makosa ya kijinai tunakuwa na urahisi wa kufanya utambuzi wa watuhumiwa. Kwa hiyo ninafurahishwa sana na hiki mnachokiandika, kitasaidia hata watu wetu (makachero) wanapokuwa wanafuatilia baada ya matukio kutokea inarahisisha utambuzi na hatimaye kukamata wahalifu,” alisema Kingai.

Hata hivyo, kamishna huyo wa polisi alikumbusha umuhimu wa kuweka kila kitu kwenye utaratibu utakaohakikisha taarifa zilizorekodiwa zinahifadhiwa kwa umakini bila kupotea ndani ya muda mfupi ili zitumike wakati wowote zikihitajika.

“Mimi naomba muwaelimishe wananchi, wakati wanafunga Digital Video Record (DVR) waiweke mbali kiasi kwamba isifikike kirahisi. Kuna baadhi ya wezi ni wajanja, wakijua kuna kamera za usalama huwa wanazi-destroy (wanaziharibu) ili kupoteza ushahidi,” alikumbusha.

DCI Kingai alisema kinachotakiwa ni DVR kuwekwa sehemu ambayo ni ngumu hata kwa mmiliki mwenyewe kuifikia ili iwe kazi itakayompotezea muda mwizi kuiona ama kuifikia ilipo ili aiharibu.


Wateja watoa ushuhuda

Akizungumza na gazeti hili, mwandishi wa Star TV mjini Moshi, Rodrick Mushi alisema mwaka 2017 aliegesha gari katika eneo la Jengo la Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) lakini alipoondoka kuna mwizi alilifungua gari lake na kuiba vitu kadhaa alivyoondoka navyo.

“Nili-park (niliegesha) kama kawaida nikatoka nikaenda maeneo ya Posta, lakini niliporudi na kuingia ndani ya gari haraka nikagundua begi langu lililokuwa na kamera, laptop, power bank na vifaa lingine halipo. Nikapata ushauri kwa vile jengo lile lina CCTV za TCB na Benki ya CRDB basi nikaombe nione nini kilitokea. Nilienda TCB, kwa kweli walinipa ushirikiano tukatizama tukaona toka ninaingia hadi huyo mtu anafungua gari langu,” alisema Mushi na kuongeza:

“Huyo mtu alikuwa amevaa kofia, tukamwona anaingia na kuchukua begi na kuondoka nalo. Nilienda polisi na ile video na kupitia alivyo na mavazi yake kuna wahalifu walikuwa lockup (mahabusu) walimtambua hadi jina.”

Mwandishi huyo alisema kutokana na utambuzi huo, polisi walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo na kupata baadhi ya vifaa na vingine tayari alikuwa ameshauza na alipofikishwa mahakamani alikiri hivyo alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela.

Meneja wa Benki ya NMB tawi la Hai mkoani Kilimanjaro, Abraham Mbise alisema katika ulimwengu wa sasa unaoshuhudia kukua kwa teknolojia, ujio wa kamera za CCTV umesaidia kuimarisha usalama na kurahisisha upelelezi.

“Hata mimi nyumbani kwangu nimefunga hizi kamera kwa sababu natambua umuhimu wake. Nikiwa ofisini ninaweza ku-access (kuona) kule nyumbani. Ukishafunga haina tena gharama labda kama unataka ku-access kutoka mbali,” alisema Mbise.

Meneja huyo alisema anatamani kuona wafanyabiashara wengi zaidi wakizifunga kamera hizo kwenye maeneo yao ya biashara pamoja na watu wenye uwezo kwenye makazi yao, kwani zina msaada mkubwa wa kuongeza ulinzi hivyo kupunguza uhalifu.