Afariki dunia kwa kusombwa na mafuriko Same

Mwili wa Joseph Ndadi(21)  aliyefariki dunia  kwa kusombwa na maji baada ya kukatika kivuko ukinyanyuliwa ili kupelekwa  kwenye gari.

Muktasari:

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro, Jeremiah Mkomagi amemtaja aliyefariki dunia kuwa ni Joseph Ndadi (21)

Same. Mtu mmoja amefariki dunia Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro kwa kusombwa na maji baada ya kivuko kilichopo Kijiji cha Mabilioni kusombwa na mafuriko.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro, Jeremiah Mkomagi amethibitisha kutokea kwa kifo hicho huku akimtaja aliyefariki dunia kuwa ni Joseph Ndadi (21), mkazi wa Kijiji cha Mabilioni.

Amesema Ndadi alifariki dunia Aprili 13, 2024 wakati akijaribu kuvuka kupitia kivuko hicho akiwa na mwezake ambaye ameokolewa.

Mkomanyi amesema chanzo cha kuvunjika kwa kivuko hicho ni kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha wilayani humo na kusababisha kivuko kukatika na vijana hao kusombwa na mafuriko.

“Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji walipopata taarifa ya kuharibika kwa kivuko hicho Kijiji cha Mabilioni, walifika eneo la tukio na kushirikiana na vyombo vingine pamoja na wananchi na kufanya jitihada za kumtafuta kijana, Joseph Ngadi, alipatikana akiwa tayari amefariki,” amesema Kamanda Mkomagi.

Amewataka wananchi kuchukua tahadhari wanapotumia vivuko katika kipindi hiki ambacho mvua kubwa zinaendelea kunyesha maeneo mbalimbali wilayani humu.

Mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini zimeripotiwa kusababisha athari kwa wananchi ikiwamo kuharibu makazi yao, miundombinu, mazao, mifugo na pia baadhi yao kupoteza maisha.

Hata hivyo, Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) imetahadharisha kuwepo kwa mvua kubwa mikoa ya  Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, Pwani, Lindi na Mtwara na visiwa vya Unguja na Pemba.

Endelea kufuatilia mitandao yetu kwa taarifa zaidi.