Wizara yabanwa kufungwa kwa mtandao wa X Pakistan

Muktasari:

  • Mahakama Kuu nchini Pakistan imeibana Wizara ya Mambo ya Ndani nchini humo kuhusu agizo lake la kusitisha matumizi ya mtandao wa kijamii wa  X yaliyozuiwa tangu Februari, 2024 kwa sababu za kiusalama.

Mahakama Kuu nchini Pakistan imeibana Wizara ya Mambo ya Ndani nchini humo kuhusu agizo lake la kusitisha matumizi ya mtandao wa kijamii wa  X yaliyozuiwa tangu Februari, 2024 kwa sababu za kiusalama.

Machi mwaka huu, Mamlaka ya Mawasiliano ya Pakistan (PTA) iliieleza mahakama kwamba ilisitisha matumizi ya mtandao huo baada ya kupokea maelekezo kutoka kwa Wizara ya Mambo ya Ndani na mashirika ya kijasusi.

Mbali na mtandao huo, PTA imesema ilipokea agizo la kusitishwa  kwa muda kwa huduma za data za mtandao wa simu na tovuti.

Kufuatia agizo la PTA, wizara ya mambo ya ndani imeieleza mahakama kuu ya Islamabad kuhusu tishio hilo la usalama ambapo katika usikilizaji wa kesi jaji alieleza kwamba sheria haiipi mamlaka wizara kuchukua hatua kuhusu ripoti za usalama zinazotolewa na mashirika ya kijasusi.

Wakili wa walalamikaji amenukuriwa na vyombo vya habari akisema kufungwa kwa mtandao huo hakuwezi kuwa tishio la ugaidi.

"Inaonekana hakuna uhalali uliotolewa wa kusimamisha mtandao wa X,’ amesema jaji akibainisha kuwa mahakama itatoa maagizo ikiwa wizara ya mambo ya ndani haitaondoa maagizo yaliyotolewa na kesi hiyo kuahirishwa hadi Mei 9, mwaka huu.