Iran yadai kuzima mashambulizi ya Israel, yazitungua droni tatu

Muktasari:

  • Taarifa hiyo imetolewa saa chache baada ya vyombo vya habari vya Marekani, vikiwanukuu maofisa wakuu wa Marekani, kuripoti kuwa makombora ya Israel yamepiga eneo la Iran.

Iran. Vyombo vya habari vya Serikali nchini Iran vimesema kuwa mfumo wa ulinzi wa anga wa nchi hiyo uliangusha ndege tatu zisizo na rubani (droni) katika Mji wa Isfaha usiku wa kuamkia leo Ijumaa Aprili 19, 2024.

Taarifa hiyo imetolewa saa chache baada ya vyombo vya habari vya Marekani, vikiwanukuu maofisa wakuu wa Marekani, kuripoti kuwa makombora ya Israel yamepiga eneo la Iran.

Tovuti ya Aljazeera imesema kuwa televisheni ya Taifa ya Iran iliripoti kutokea kwa milipuko katika Mji wa Isfahan, ambapo  mfumo wa ulinzi wa anga ukiyazuia, huku safari za ndege katika maeneo kadhaa ikiwa ni pamoja na Tehran na Isfahan zikisitishwa.

Ajazeera imeripoti kuwa anga la maeneo hayo lilifunguliwa kwa takriban saa nne na nusu baada ya tukio hilo na hakukuwa na ripoti za majeruhi.

Awali tovuti ya ABC ilimnukuu Ofisa Mkuu wa Marekani, kwamba Israel ilirusha makombora katika eneo moja nchini Iran. Habari za CBS pia ziliripoti kwamba shambulio hilo limeikumba Iran.

Israel iliahidi kujibu mashambulizi baada ya Iran Jumamosi iliyopita kurusha droni za makombora nchini humo.

Msemaji wa Shirika la Anga za juu la Iran, Hossein Dalirian alisema ndege kadhaa zisizo na rubani zimetunguliwa kwa mafanikio.

"Hakuna ripoti za shambulio la kombora kwa sasa," Dalirian alisema kwenye mtandao wa kijamii wa X.

Isfahan ni jiji muhimu kimkakati pia upo karibu na mji wa karibu Natanz ambalo ni eneo la lenye nyuklia ya Iran.