Tishio la kutoweka kwa ndizi labadili mtindo wa maisha

Gari likiwa linapakuwa ndizi katika bandari ya ziwa Vistoria jijini Mwanza. Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Madhara yake yanaonekana wazi hasa katika vijiji vya Wilaya ya Muleba, migomba imeharibika jamii imelazimika kubadili mfumo wa maisha na kuweka kando baadhi ya mambo ambayo uwepo wake hutegemea mazao yatokanayo na ndizi.

Tishio la kutoweka kwa migomba mkoani Kagera mbali na kusababisha uhaba mkubwa wa chakula na kuyumbisha uchumi wa familia nyingi, pia mfumo wa maisha umebadilika ili kukabiliana na hali hiyo kwa sasa.

Madhara yake yanaonekana wazi hasa katika vijiji vya Wilaya ya Muleba, migomba imeharibika jamii imelazimika kubadili mfumo wa maisha na kuweka kando baadhi ya mambo ambayo uwepo wake hutegemea mazao yatokanayo na ndizi.

Kwa wakazi wa mkoa huu hususan Kabila la Wahaya, zao la ndizi linalotokana na kilimo cha migomba lina nafasi muhimu katika shughuli mbalimbali za kitamaduni. Mbali na chakula pia ni miongoni mwa mazao muhimu ya biashara.

Kinywaji cha rubisi ni miongoni mwa mazao mengi yanayotokana na zao la ndizi. Sasa kasi ya migomba kushambuliwa na magonjwa na kusababisha ndizi kuadimika, matumizi ya kinywaji hicho yameanza kusahaulika taratibu.

Kinywaji hicho hutokana na ndizi kali ambazo baada ya kuvundikwa kwa siku kadhaa hukamuliwa juisi ambayo inaweza kutumiwa kulingana na mahitaji ingawa ili kupata pombe ya rubisi itahitaji siku moja zaidi baada ya kuweka mtama ili kupata uchachu.

Wanawake waliotegemea kuendesha maisha yao na familia kwa kuuza togwa, moja ya mazao yanayotokana na zao la ndizi, hivi sasa wanalazimika kutafuta njia nyingine za kujikimu kutokana na uhaba mkubwa wa ndizi.

Kwa watumiaji wa kinywaji cha rubisi kama sehemu ya utamaduni. Utafiti wa Kituo cha Habari cha Marekani (CNN) kwamba Tanzania ni miongoni mwa nchi sita za Afrika zinazoongoza kwa wananchi kunywa ‘mataputapu’ ikiwemo rubisi, kwao haiwezi kuwa hoja muhimu sana.

Baadhi ya watumiaji wa kinywaji hicho wanaweza kuhusisha matokeo ya utafiti huo na kasumba ya kikoloni katika maeneo mengi ya Afrika ambapo pombe za kienyeji zilipewa kila aina ya jina chafu ili kutoa fursa ya pombe za kizungu kupata soko.

Utafiti huo wa mwaka 2013 unaitaja Uganda kama kinara kwa kunywa pombe chafu iitwayo Luwombo ikifuatiwa na Rwanda huku Tanzania ikishika nafasi ya tano nyuma ya Burundi na matokeo kudai asilimia kubwa ya nchi za Afrika wanapenda kutumia pombe kali kwa lengo la kuondoa msongo wa mawazo.

Hata hivyo, matokeo ya utafiti huo hayawezi kupindua ukweli kuwa kinywaji hicho kinatumika kuhifadhi mambo ya kitamaduni kama kwenye taratibu za kuoa na kuolewa na kama kinywaji muhimu kwenye matukio ya kijamii na mikusanyiko mbalimbali.

Mtaalamu kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo, Maruku Mugenzi Byabachwezi anasema migomba ni zaidi ya zao la biashara kwani hutumika kama utambulisho na masuala mengine ya kitamaduni na kuwa wanafanya juhudi ya kutoa elimu ili kupambana na hali ngumu ya sasa.

Baadhi ya watoto kutoka katika familia maskini wamefanikiwa kunusa kuta za vyuo vikuu baada ya ndizi kuongezwa thamani na kuzalisha vinywaji mbalimbali.

Wapo waliojitwisha vibuyu na kuuza vinywaji hivyo kwa bei ya rejareja katika magulio na mikusanyiko ya watu.

Hadi kinywaji cha rubisi kinapoelekea kutoweka kama yalivyo mazao mengine yanayotokana na ndizi, hakuna ushahidi wa jitihada zilizowahi kufanyika kuwasaidia wazalishaji wa aina hiyo ya kinywaji ili kiongezwe thamani na kuwa kinywaji kinachoweza kupata soko nje ya wenyeji wake.

Ugonjwa hatari

Ugonjwa hatari wa Unyanjano unaojulikana kitaalamu kama (Banana Xanthonas Wilt-BXW) ndiyo umebadili mkondo wa maisha na hata kuleta hofu kubwa kwa wakazi wa Mkoa wa Kagera kutokana na uwezekano mkubwa wa kulipuka kwa baa la njaa.

Miongoni mwa matukio ambayo siyo ya kawaida ikilinganishwa na miaka michache iliyopita ni baadhi ya mashamba ya migomba kubadilishwa matumizi ya kilimo cha mazao mengine kama karanga, magimbi na mihogo.

Hali ya mashamba kubadilishwa matumizi baada ya migomba kushambuliwa na ugonjwa huo inajionyesha wazi katika vijiji tofauti vya Kata za Buganguzi na Kishanda Wilayani Muleba huku baadhi ya mashamba yakionekana kutelekezwa.

Mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Buhanga Deusdelith Muhazi alisema njia pekee iliyobaki ya wananchi kujinasua na janga hilo ni kufyeka mashamba yenye migomba iliyoathirika na kulima mazao mengine ingawa nayo hayawezi kukidhi mahitaji makubwa ya chakula.

Baada ya ugonjwa huo kuteketeza migomba hata huduma mbalimbali za kijamii zilizoendana na matumizi ya ndizi nazo zimebadilika kwani kwa familia zilizo nyingi ni rahisi zaidi kupata fungu la magimbi kuliko chane ya ndizi.

Matukio ya misiba na sherehe nayo yamechukua sura mpya ambapo matumizi ya ndizi katika matukio hayo hayapewi kipaumbele tofauti na zamani ambapo katika matukio kama hayo ilikuwa ni marufuku kupeleka mazao ya nafaka kwa ajili ya huduma.

Kwa mujibu wa mtaalamu kutoka kituo cha utafiti Maruku Leonard Mukandara anasema wakulima wanaweza kuepukana na mashambulizi ya ugonjwa wa unyanjano kwa kutumia mbegu bora na kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalamu.

Kwamba tofauti ya migomba ya asili na ile iliyofanyiwa utafiti na watalaamu ni kuwa migomba ya kisasa ina uwezo mkubwa wa kuvumilia magonjwa ikiwemo kirusi kinachoeneza ugonjwa wa unyanjano.

Taarifa za kiutafiti zinaonyesha kuwa ugonjwa huo uligundulika kwa mara ya kwanza kwa wakulima wa Kijiji cha Kabale Tarafa ya Izigo Wilayani Muleba Mkoani hapa mwaka 2005 na tangu wakati huo umesambaa kwa kasi katika wilaya zote.

Kwa mujibu wa Mtafiti Mkuu na mtaalamu wa utafiti wa wadudu na magonjwa katika kituo cha utafiti Maruku Salimu Sai anasema asilimia sabini ya ugonjwa huo unasambazwa na vifaa vya shambani.

Anasema lazima vifaa hivyo visafishwe kwa ‘jiki’ ambayo husaga vimelea vya bakteria au mkulima kupitisha vifaa hivyo kwenye maji ya moto au moto kila baada ya kifaa kutumika kwenye kila shina la mgomba.

Serikali ya mkoa yazinduka

Kutokana na kuwepo kwa kila aina ya dalili mbaya inayoashiria ujio wa baa la njaa, Mkoa wa Kagera umezindua operesheni kabambe ya kupambana na usambaaji wa ugonjwa wa unyanjano na kuagiza sheria ndogo zitungwe ili kuwabana wakulima watakaozembea.

Kupitia kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa kilichofanyika hivi karibuni wajumbe walibariki operesheni hiyo huku kila wilaya ikiagizwa kuzingatia suala hilo katika bajeti zao na kutangazwa mwaka 2014 kuwa wa kutokomeza ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali mstaafu Fabian Massawe operesheni hiyo itakuwa na awamu tofauti kuanzia kuelimisha na hatimaye kipindi cha kufanya tathimini kutokana na operesheni itakayokuwa imefanyika ya kutokomeza ugonjwa huo.

Ugonjwa wa unyanjano wa migomba hauna uhusiano na ugonjwa wa mnyauko wa mibuni au mazao mengine hivyo mkulima anapong’oa migomba iliyoathirika halazimiki kufanya hivyo kwa mazao mengine.