Jinsi elimu bure ilivyoibua changamoto lukuki

Muktasari:

  • Elimu bure imeanza rasmi mwaka 2016 ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014 na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015.
  • Mwananchi ilitembelea kwenye shule kadhaa za msingi za jijini hapa, ambapo ilibaini kuna mwitikio mkubwa wa uandikishwaji wa watoto tofauti na miaka iliyopita, ingawa pia kuna changamoto mbalimbali zinazokwaza utekelezaji wa dhana hiyo.

Serikali ya Awamu ya Tano ilianzisha utaratibu wa kutoa elimu ya awali, msingi na sekondari bure, lengo lake likiwa ni kuongeza wingi wa wanafunzi shuleni hasa kutoka kwenye kaya masikini ambazo zilishindwa kumudu gharama za michango ya shule, hivyo kuwa kikwazo kwa watoto wao kupata elimu.

Elimu bure imeanza rasmi mwaka 2016 ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014 na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015.

Mwananchi ilitembelea kwenye shule kadhaa za msingi za jijini hapa, ambapo ilibaini kuna mwitikio mkubwa wa uandikishwaji wa watoto tofauti na miaka iliyopita, ingawa pia kuna changamoto mbalimbali zinazokwaza utekelezaji wa dhana hiyo.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kibonde Maji, Temeke, Dar es Salaam, Hassa Msonzo anasema kumekuwa na mwitikio mzuri kwa wazazi na walezi, katika kuandikisha watoto darasa la kwanza kutokana na hatua ya Serikali kutangaza kutoa elimu bure.

“Hadi sasa tumeandikisha wanafunzi 423 mwitikio ni mkubwa, hata hivyo tuna changamoto kwenye miundombinu inakuwa ni kikwazo kwa namna moja, kwani idadi yote hiyo kuna vyumba vitatu ambavyo wanatumia hivyo imekuwa ngumu kuwapanga kwa idadi inayotakiwa,” alisema Msonzo.

Alisema wamewagawanya wanafunzi hao katika makundi matatu ikiwa ni wanafunzi 141 na wakati mwingine wamelazimika kuwaweka wengine kwenye hema ili kuhakikisha wanapata uelewa wa kile kinachofundishwa.

“Kati ya hao 244 ni wavulana na wasichana ni 179, walimu nilionao shule nzima ni 68 wanajitosheleza kwa mahitaji tuliyonayo hapa, isipokuwa tatizo ni madarasa na matundu ya vyoo,” alisema.

Mwalimu Msonzo alisema kuna jumla ya matundu ya vyoo 26 wakati mahitaji ni matundu 117 kulingana na idadi ya wanafunzi 2,715 waliopo shule nzima.

“ Idadi ya jumla ya wavulana kwa sasa ni 1,326 ambapo wavulana 50 wanatakiwa kutumia tundu moja na wasichana wapo 1,389 wasichana 40 wanapaswa kutumia tundu moja,” alisema.

Mwalimu Msonzo shule yake haina tatizo na madawati kutokana na hamasa ambayo Serikali ilifanya ya kuchangisha madawati .

Shule ya Msingi ya Makumbusho

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Benedictor Lyimo alisema hali imekuwa ni tofauti kutokana na maisha katika eneo hilo kuwa ghali, hivyo kusababisha wazazi wengi kuamua kuhama.

Alisema kwa mwaka huu wameandikisha wanafunzi 121, wavulani wakiwa 69 wasichana 52 wakati mwaka jana waliandikisha wanafunzi 167.

“ Wakati idadi ya kuandikisha ikipungua jumla ya wanafunzi 70 waliombewa uhamisho na wazazi au walezi wao, kati yao wavulana walikuwa ni 40 wasichana 30 ,” alisema .

Mwalimu Lyimo anasema anashukuru kwamba idadi ya madarasa ni 22 ambayo yanatumiwa na wanafunzi 1,085 walimu wakiwa 29. Changamoto ipo kwenye matundu ya choo ambapo yapo 14 wakati yanayohitajika ni 51.

Shule ya Msingi ya Tandale

Jumla ya wanafunzi 320 wameandikishwa kuanza darasa la kwanza katika shule hii kwa mwaka huu, wavulana wakiwa 164 wasichana 156.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Jenster Emil anasema kuna changamoto kadhaa ikiwamo idadi ndogo ya walimu wa darasa la kwanza. Kwa sasa wapo wanne ambao hawatoshi kulingana na idadi ya wanafunzi.

“Mwongozo tulionao ni wanafunzi 40 kwa mwalimu mmoja kwenye darasa, hivyo kwa idadi hiyo tunatakiwa kuwa na madarasa manane, sasa hapa nina uhaba pia wa hao walimu kwani jumla wapo 35, lakini wengine wapo masomoni pia wapo wanaoumwa wakati idadi ya wanafunzi ni 1,565,” alisema.

Alisema pia matundu ya vyoo yapo 18 ambayo hayatoshi ingawa kuna choo kingine kilitengenezwa, lakini hakijawahi kutumika kutokana na nyufa zilizojitekeza kwenye sakafu ya choo na kuwa tishio kwa usalama wa wanafunzi.

Changamoto zilizobainika kwenye shule hizo ni mfano mdogo wa mambo ambayo yamejitokeza kwenye shule kadhaa nchini, chini ya mfumo huu wa elimu bure, ambapo yanapaswa kutafutiwa ufumbuzi haraka ili kuboresha mazingira ya masomo.

Rais John Magufuli Machi 2 mwaka huu alianza ziara ya kikazi ya siku nne katika mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara, ambako alizungumzia jinsi anavyoamini kwamba wazazi wengi wamefanikiwa kuandikisha watoto wao shule kutokana na uamuzi wa Serikali wa kutoa elimu.

Alisema hatua hiyo inatokana na juhudi za Serikali yake katika kuhakikisha kwamba kila mtoto anapata fursa ya kupata elimu, bila kuwekewa kikwazo na michango ya ada.

Waziri wa Tamisemi, George Simbachawene alipozungumzia jinsi Serikali ilivyojipanga kugharimia uendeshaji wa elimu bure, kwa mwaka wa fedha 2016/2017 imetenga jumla ya Sh 131.4 bilioni ikiwa ni fedha za ruzuku ya uendeshaji wa shule, chakula, mitihani na fidia ya ada.

Alisema fedha hizo zinapelekwa moja kwa moja shuleni kutoka Hazina kwa wastani wa Sh18.777 bilioni kwa kila mwezi kwa ajili ya ruzuku ya uendeshaji wa shule. Sh10,000 ni kwa mwanafunzi wa msingi na Sh25,000 kwa mwanafunzi wa sekondari kwa mwaka.

Kwa wanafunzi wa shule za bweni imetegwa Sh1,500 kwa siku kwa wale wa shule za msingi, wakati kwa sekondari chakula, fidia ada ya Sh 20,000 kwa mwanafunzi wa kutwa na Sh70,000 kwa mwanafunzi wa bweni wa kidato cha kwanza hadi cha nne kwa mwaka.

Mwongozo uliotolewa

Wizara za Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi pamoja na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) walitoa mwongozo wa utoaji wa elimu ya msingi bila malipo, mwongozo wa uandikishaji darasa la kwanza 2016, maelekezo kwa wanafunzi wanaojiunga kidato cha kwanza mwaka 2016, miongozo kuhusu matumizi ya fedha zitakazopelekwa shuleni.

Pamoja na mambo mengine pia katika mwongozo huo yamebainishwa majukumu yanayotakiwa kufanywa na wizara hiyo, Tamisemi, wakurugenzi wa manispaa na halmashauri ya wilaya, wakuu wa shule, bodi za shule, wazazi na wananchi.

Majukumu ya wazazi na walezi kuanzia Januari, wazazi wanapaswa kununua sare za shule na michezo, vifaa vya kujifunzia vikiwemo madaftari na kalamu na chakula kwa wanafunzi wa kutwa na kugharimia matibabu kwa watoto wao.

Wanatakiwa pia kulipia nauli ya kwenda shule na kurudi kwa wanafunzi wa kutwa na wanafunzi wa bweni wakati wa likizo; kununua magodoro, shuka, vifaa vya usafi binafsi kwa wanafunzi wanaosoma shule za bweni na wanaoishi katika hosteli zinazotumiwa na Serikali.

Pia, wanatakiwa kukemea na kutoa taarifa kuhusu mienendo inayokwenda kinyume na elimu ya msingi bila malipo.

Tamisemi kwa upande wake pamoja na majukumu mengine kadhaa, inawajibika katika kutoa mwongozo wa matumizi ya fedha za umma kwa wakuu wa shule, kuratibu uandaaji wa mipango na bajeti ili kupata mipango na bajeti ya taifa kila mwaka inayozingatia mahitaji halisi ya elimu ya msingi bila malipo.

Pia, Tamisemi inatakiwa kufanya ukaguzi wa ndani, ufuatiliaji na tathmini za mara kwa mara, ili kuhakikisha elimu ya msingi bila malipo inatolewa kwa ufanisi na viwango vya ubora inavyostahili.

Kamati au Bodi za Shule

Wizara katika waraka huo inataka kamati za shule kufuatilia na kusimamia matumizi ya fedha zinazotolewa na Serikali ili ziweze kuleta tija; kuhakikisha kuwa sera, nyaraka, maelekezo na miongozo ya Serikali inazingatiwa na kutoa ushauri stahiki.

Pia, waraka huo umeainisha majukumu ya walimu ambao kazi yao kubwa ni kusimamia sera na miongozo ya utoaji elimu bure. Wanafunzi ambao ndio walengwa wakuu wa utoaji elimu pia wametakiwa kuhakikisha wanakuwepo shule katika kipindi chote cha masomo.