Boniface Jacob: Kutoka umeya hadi ufugaji

Boniface Jacob, meya mstaafu wa Manispaa ya Ubungo

Muktasari:

  • Baada ya kukaa kwenye baraza la madiwani kwa miaka 10, Boniface Jacob, meya mstaafu wa Manispaa ya Ubungo anafurahia maisha nje ya ulingo wa siasa.

Baada ya kukaa kwenye baraza la madiwani kwa miaka 10, Boniface Jacob, meya mstaafu wa Manispaa ya Ubungo anafurahia maisha nje ya ulingo wa siasa.

Akijitambulisha kwa jina la Bonny Yai, mfugaji huyu wa kuku wa mayai anasema soko ni kubwa kiasi cha kumuelemea, hivyo kuanza kutafuta wafugaji wenzake anaoshirikiana nao kukidhi mahitaji ya wateja.

Jacob, mwenyeji wa ubungo mwenye asili ya Kyela mkoani Mbeya anasema ukiwa na bidhaa mkononi ni rahisi kutafuta wateja, usipofanya hivyo utapata hasara na ukitafuta hutolikosa.

“Nilianza kwa kuuza nchini, lakini sasa hivi napeleka mayai mpaka nje ya nchi. Nilianza na Comoro, nililipata hilo soko baada ya kuwa na mayai mengi kipindi fulani ambayo soko lake lilikuwa linasumbua,” anasema Jacob alipotembelea ofisi za Mwananchi.

Akiwa anavuna kati ya mayai 3,000 mpaka 5,000 kila siku, meya huyu mstaafu anasema soko la nje ni zuri zaidi, ingawa linahitaji uelewa wa mambo mengi kuanzia ratiba ya meli, mteja atakayeupokea mzigo, ufungashaji na kodi za kulipia.

Wakati trei moja likiuzwa wastani wa Sh6,500 nchini, anasema akilifikisha Comoro huliuza kati ya Sh30,000 hadi Sh40,000. Changamoto iliyopo ni usafiri wa kwenda huko, kwani anasema kuna wakati meli huwa inapatikana mara mbili kwa mwezi.

“Kwenye kuku nimepiga hatua, nilianza kama Bon Yai lakini hivi sasa nafikiria kuanza kusambaza nyama ya kuku. Tunalenga maduka makubwa ya ndani pamoja na kusafirisha kwenda nje ya nchi kwa sababu masoko tumeshayapata. Tunasubiria vifaa vya kuchinjia, kunyonyolea hata kukatia,” anasema.

Jacob ambaye ni mjumbe mstaafu wa kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anasema kutokana na kujitangaza kwake kwenye mitandao ya kijamii amepata wateja wengi kuliko uwezo wake wa kuzalisha mayai.

Ili kuwahudumia wateja wengi kadiri awezavyo, anasema anawashirikisha wafugaji wenzake ambao humkusanyia mayai kisha kumpelekea ofisini kwake, Mabibo External naye kuyasambaza.

Wafugaji anaoshirikiana nao ni wa Bagamoyo na Mlandizi mkoani Pwani yalipo mashamba yake na hufanya hivyo kwa makubaliano maalumu yanayosaidia kuwapa soko kubwa wajasiriamali hao wadogo.

“Nimepunguza kasi ya kujitangaza na kutafuta masoko mapya ili kutosheleza mahitaji ya waliopo kwanza. Kuna wakati napokea oda nyingi mpaka nachanganyikiwa,” anasema Jacob.

Kwa wateja alionao, anasema wengi wanatoka mikoa ya kusini hasa Lindi, Mtwara na Ruvuma pamoja na kanda ya kati kuanzia Morogoro, Dodoma, Singida, Shinyanga hadi Tabora.

Ingawa Dar es Salaam watu wanaongoza kwa kula chipsi mayai, anasema hakuna wateja wakubwa kwani kwa uzoefu wake hajawahi kupata anayenunua trei 100 au 200 kila baada ya wiki kama ilivyo kwenye mikoa hiyo mingine.

Kwa mikoa ya kaskazini, Jacob anasema hakuna wateja wakubwa pia kwa sababu wananchi wengi huko ni wafugaji wa kuku na mifugo mingine.

“Barabara ya kusini kuanzia Wilaya ya Rufiji (Pwani) hadi Tunduru (Ruvuma) kuna soko kubwa la mayai ya kisasa ndio maana ni rahisi kupata chipsi samaki lakini sio chipsi mayai. Huko soko lipo wazi,” anasema akifafanua kwamba kwa Dar es Salaam, wateja wengi wananunua kati ya trei tano hadi 10, tofauti na kwingine ambako mtu mmoja anaagiza kuanzia trei 1,000 mpaka 3,000.

Kuhusu mabadiliko ya bei sokoni, Jacob ambaye ni mwalimu kitaaluma anasema kitovu huwa jijini Dodoma ambako hutegemea kama vyuo vimefunguliwa au vimefungwa.

Vyuo vikifunguliwa, anasema mahitaji ya mayai huwa juu, lakini vikifungwa hushuka kwani chipsi mayai hayaliwi sana. Mwenendo huo, anasema huathiri bei ya bidhaa hiyo katika mikoa mingine pia.


Biashara zaidi

Kutokana na uzoefu alioupata kwenye ufugaji wa kuku wa mayai, Jacob anasema anao mpango wa kutanua shughuli hizo kwa kusambaza nyama kwenye maduka makubwa nchini.

Licha ya kuuza nyama, diwani huyu wa Makuburi kuanzia mwaka 2010 mpaka 2020 anasema anao mpango wa kufungua mashamba ya kutotolesha vifaranga pia ili kuimarisha shughuli zake za shambani.

Katika kutanua shughuli zake za ujasiriamali, anasema anajihusisha pia na usafirishaji wa mazao kwenda nje ya nchi. Mazao haya anasema hutegemea mahitaji yaliyopo, lakini iwe korosho, dengu au choroko akipata oda tu hukusanya mzigo.

“Nimejikita katika ujasiriamali na utafutaji kwa sababu naamini siasa ni fedha. Ukiwa na fedha utafanya siasa nzuri na mawazo yanayojitegemea. Nafanya ununuzi wa mazao na kuyasafirisha kwenda nje ya nchi, ninalo ghala maeneo ya Ubungo,” anasema.

Mambo hayo yote anasema yanafanyika kwa kufuata sheria, kwani amesajili kampuni inayosimamia mambo yote hayo, akililenga zaidi soko la kimataifa akianzia Comoro na Kenya, huku akijitanua taratibu.


Dhana ya vijana kujiajiri

Kwa fursa zilizopo, Jacob anasema vijana wanaweza kujiajiri iwapo mazingira yatakuwa rafiki kwao kwa kuziondoa changamoto zilizopo, hasa upatikanaji wa mtaji.

Ili kufuga kuku 1,000 wa nyama, anasema zinahitajika Sh7 milioni kwa mtu mwenye mabanda tayari au Sh35 milioni kwa anayetaka ufuga kuku wa mayai. Ingawa vijana wengi wangependa kushiriki ufugaji huu, si wote wanaoweza kuupata mtaji huo.

Yeye ameweza kwa sababu alijiwekea akiba kidogo alipokuwa diwani akaweza kununua shamba na kujenga mabanda, ila ni ngumu kwa kijana aliyehitimu chuo kuwa na uwezo wa kufanya hayo yote na bado awe na fedha za uendeshaji zinazojumuisha ununuzi wa vifaranga, chanjo, vyakula pamoja na kulipia maji na umeme.

Ili kuwasaidia vijana kujiajiri katika sekta ya kilimo, Jacob anaishauri Serikali irahisishe upatikanaji wa mitaji. Utaratibu wa kuwaandalia mashamba makubwa katika kila mkoa unaoendelea kufanywa na Wizara ya Kilimo anasema utasaidia lakini unatakiwa kuboreshwa zaidi.

Licha ya kutenga mashamba, anasema uwekwe utaratibu utakaowawezesha kupata mbegu, mbolea na viuatilifu vyote muhimu vinavyohitajika. Hata kwa miradi ya ufugaji, anasema yakishajengwa mabanda, wapewe mtaji wa uendeshaji wa mradi husika.

“Kama kuna dhamira ya dhati katika hili basi benki za kilimo zijielekeze kuvisaidia vikundi vya vijana wadogo, kuwasimamia na kuwalea katika mashamba walau kwa miaka mitatu kabla hawajaenda kujitegemea,” anasema.

Hata mikopo inayotolewa na halmashauri zote nchini kwa kutenga asilimia 10 ya mapato yao ya ndani, anasema utaratibu unaotumika kutoa mikopo hiyo hauwawezeshi vijana kujiajiri, kwani wengi wana ndoto na mipango mikubwa kuliko kiasi kinachotolewa.

“Nimekuwa diwani halafu meya kwa muda mrefu, nafahamu taratibu zilizowekwa na Serikali Kuu zinazibana halmashauri, kwani zinatakiwa kutoa mkopo wa kikundi. Kwa mfano vijana wakiwa 10 halafu wapewe mkopo wa Sh1 milioni utawasaidia nini? Hawatoweza kumudu gharama za ufugaji, hivyo changamoto ya mtaji ikitatuliwa, vijana wapo tayari kujiajiri,” anasema.

Kwa utaratibu unaotumiwa sasa hivi na halmashauri nyingi, anasema ni ngumu kuona matokeo ya moja kwa moja, ingawa kiasi kinachotolewa ni kikubwa ambacho kingeweza kuwa na mchango kwenye uchumi wa kaya na Taifa kwa ujumla.

Ukiacha utaratibu uliowekwa na Serikali Kuu, anasema watendaji wanaoisimamia mikopo hiyo nao huweka urasimu unaowafanya baadhi ya vijana wenye uhitaji kutonufaika nayo.

“Halmashauri pia zinaweza kukopesha kwa njia za miradi, yaani itengeneze mabanda au mashamba kwa kuweka miundombinu inayotakiwa kisha kijana anaingia kusimamia banda la kuku au shamba la zao lililochaguliwa, baada ya muda ataweza kujitegemea,” anasema.

Endapo Serikali itabadilisha utaratibu na kuruhusu mtu mmoja mmoja kukopa kwa namna atakayoweza kurudisha fedha alizokopeshwa, anasema itasaidia kuwafikia vijana wengi hivyo kuwawezesha kiuchumi.

Kwa kuanzisha miradi ya kuwawezesha vijana, anasema itakuwa rahisi kuwafikia wengi. Anatolea mfano, alipokuwa meya wa Ubungo kwamba waliwahi kuanzisha mradi wa kukopesha bajaji pamoja na kufyatua matofali ambayo inaendelea mpaka leo.

“Vijana tuliowakopesha bajaji wanafahamu baada ya muda wa mkataba zitakuwa za kwao, wanazitunza na kuziendesha kwa umakini. Tuliowapa mradi wa matofali wanausimamia vizuri. Hali ingekuwa tofauti kama tungewapa fedha taslimu vijana hawa,” anasema.

Leo hii, akikutana na bajaji ambayo halmashauri iliikopesha, anasema hujisikia fahari kwamba walichokikusudia kimetimia na kinamsaidia kijana waliyemlenga, huku wale waliopewa fedha taslimu wengi wakiwa hawajulikani walipo.