Tabu: Nilirudia darasa mara tisa

Waswahili husema mcheza kwao hutunzwa, na hivi ndivyo lafudhi ya Kimakonde ilivyobadili maisha ya Tabu Mtingita mzaliwa wa Mtwara kuwa miongoni wa waigizaji mahiri nchi Tanzania.

Tabu ambaye aliingia kwenye uigizaji akiwa na umri wa miaka 40, ameliambia Mwananchi kuwa mwanzoni haikuwa rahisi kuingia katika tasnia hiyo.

“Kwanza kabisa haikuwa rahisi kama watu wanavyodhani mimi kuingia katika sanaa ya uigizaji japo nilikuwa napenda lakini kwa bahati mbaya wazazi wangu walikuwa hawataki kabisa nijihusishe na masuala hayo,” alisema Tabu.
Hata hivyo, ameeleza jinsi wazazi wake walivyokuwa wakimwekea matarajio katika elimu, ambayo amedai hakuwa na akili ya darasani hivyo alijikuta akirudia darasa zaidi ya mara tisa.

“Mimi bhana sikuwa na akili nilivyokuwa shule, japo wazazi wangu walijitahidi kunisomesha. Kwa sababu walitaka nikae ofisini lakini nilivyokuwa kidato cha nne niliambulia ziro licha ya kurudia darasa mara tisa,”  alisema.
Pamoja na umahiri wake kwenye vichekesho, Tabu ameeleza kuwa wasanii wa mjini siyo watu wa kushirikiana nao sana labda katika matatizo tu.
 

“Nimeamua kukaa mbali na wasanii wenzangu labda kwenye matukio kama msiba ndiyo naweza kushirikiana nao, ndiyo maana nipo Dar ila naishi Mbagala sehemu ambayo huwezi kuwakuta watu maarufu wakiishi,” alisema Tabu.
Hata hivyo, ameeleza kuwa kutopendana kwa baadhi ya  wasanii wa maigizo ndiyo chanzo cha kutofanikiwa.

“Sababu inayofanya tusifike mbali zaidi hatupendani sisi kwa sisi na mtu hawezi kum-support mwenzake mpaka amlipe, hiyo inatufanya kukosa mshikamano kitu kikubwa tunachopenda ni kudharauliana na kunafikiana katika kazi, yaani imekuwa kila mtu hapendi mafanikio ya mwingine,” alisema mwigizaji huyo.

Tabu hakuishia hapo na kueleza kuwa wasanii wa zamani ambao walikuwa wanaonekana kwenye movie kwa sasa hawaonekani, wamekuwa wakionekana watu wasio na uwezo.

“Wasanii wazuri siku hizi hawapo, wanachukuliwa watu ambao wanaonekana na followers wengi mtandaoni ndiyo wanawekwa katika tamthilia ambao hata hawawezi kuigiza na hata ukiwatazama unapoteza ladha ya filamu,” alisema Tabu.

Baadhi ya filamu ambazo Tabu amewahi kucheza ni kung’arisha jina lake zaidi  ni Maji ya Shingo, Panguso, Chini ya Kapeti, Kitimtim, Mama Ntilie na Mshenga.