Mke wa Mohbad akanusha kupima DNA kwa siri

Dar es Salaam. Omowunmi Aloba, maarufu Wunmi mke wa marehemu msanii kutoka nchini Nigeria Mohbad amekanusha kufanya vipimo vya siri vya nasaba deoxyribonucleic acid (DNA) kwa mwanaye, Liam Mohbad.

Hii ni baada ya kuzuka kwa uvumi kupitia mitandao ya kijamii ikiripoti kuwa wakati baba mkwe Joseph Aloba (baba mzazi wa Mohbad), akisisitiza uchunguzi wa DNA ufanyike dhidi ya mjukuu wake Liam Wunmi alifanya vipimo vya siri ndiyo maana hataki kutoa majibu.

Kwa mujibu wa chombo cha habari cha ‘Sahara Reporters’ kilidai kuwa waliwasiliana na Wunmi jana Alhamisi Mei 2, 2024 kujua undani kuhusu uvumi huo ndipo mwanadada huyo aliweka wazi na kueleza kuwa hakuna ukweli wowote kwenye hilo.

Tangu kifo cha Mohbad, kumekuwa na mzozo kuhusu baba wa Liam, huku baadhi ya wananchi na baba Mohbad wakiomba uchunguzi wa DNA ufanyike kwa Liam, ambapo mwanadada huyo alieleza kuwa inabidi baba Mohbad apate ruhusa kutoka Mahakamani ili aweze kumuachia mwanaye kupima DNA.

Mohbad alifariki Septemba 12, 2023 jijini Lagos akiwa na umri wa miaka 27 huku uchunguzi wa kifo chake bado ukiwa unaendelea.