Bi Star, Wema Sepetu, Irene Paul kuchuana msanii bora wa kike wa filamu

Wema Sepetu

Muktasari:

Msanii Shamila Ndwangila' Bi Star'  ametajwa kuwa mmoja wa wasanii watakaochuana katika kipengele cha kumsaka  msanii bora wa kike katika tuzo za filamu.

Dar es Salaam. Msanii aliyetingisha kwenye filamu ya ‘Kombolela’ Shamila Ndwangila' Bi Star'  ametajwa kuwa mmoja wa wasanii watakaochuana katika kipengele cha msanii bora wa kike katika tuzo za filamu.

Orodha ya wateule hao imetangazwa leo, Ijumaa Desemba 9, 2022 na Mkurugenzi wa maendeleo ya filamu kutoka Bodi ya filamu, Emmanuel Ndumukwa kwenye mkutano na waandishi wa habari.

Katika kipengele cha msanii bora wa kike waliotajwa kuchuana ni Bi Star aliyeigiza kama Mwadawa kwenye filamu ya ‘Kombolela’.

Mastaa wengine waliotajwa katika kipengele hicho ni Wema Sepetu aliyeigiza kama Malkia katika filamu ya ‘Malkia’.

Pia yupo Irene Paul aliyeigiza kama Tanasha katika filamu ya ‘Yalaiti’.

Wasanii wengine waliotajwa ni Thecla Mjata, Nyota Waziri ambaye ni mwanamuziki anayefanya vizuri kwenye uga wa uigizaji na Tunu Mbegu. Numukwa amesema kuwa tuzo hizo zinatarajiwa kutolewa Desemba 17 jijini Arusha ambapo wasanii 162  watachuana huku filamu 60 zikishindanishwa.