Bi Kidude apuuza agizo, apanda jukwaani

Msanii mkongwe wa muziki wa mwambao, Asha Baraka (Bi Kidedu) akiwa jukwaani kusalimia mashabiki wa Tamasha la Sauti za Busara kwenye Viwanja vya Ngome Kongwe Zanzibar. Kulia ni kiongozi wa Kundi la wanawake la Taarabu, Tausi Women Taarabu, Mariamu Hamdani.

Muktasari:

Bi Kidude, sekunde chache baadaye alionekana jukwaani akiwa mkakamavu na kuwasalimia mashabiki, lakini alipoambiwa ashuke, aligoma na kusema lazima afanye kazi japo kidogo.
Ndipo akaanza kuimba nyimbo za kiarabu na zile za Unyago ambazo inasemekana yeye ndiyo huzitumia kuwafundisha mabinti wanaojiandaa kuolewa.

Mwimbaji mkongwe wa muziki Tanzania, Kidude Bint Baraka juzi usiku alikuiuka agizo la Serikali ya Zanzibar kutokuimba kwenye tamasha la Sauti za Busara.

Msanii huyo, alipanda jukwaa la Ngome Kongwe kwa ajili ya kuwasalimia mashabiki wa tamasha hilo, lakini baadaye aligoma kushuka bila kuwapa raha mashabiki.
Hiyo ilikuja muda mfupi kabla ya kupanda jukwaani Kundi la Zanzibar Unyago, ambalo Bi Kidude ndiyo mlezi na mwalimu.

Washereheshaji Carola Kinasha na mchekeshaji Evans Bukuku waliwataarifu maelfu kuwa Bi Kidude atapanda jukwaani kuwasalimu mashabiki na kisha kuondoka.

Bi Kidude, sekunde chache baadaye alionekana jukwaani akiwa mkakamavu na kuwasalimia mashabiki, lakini alipoambiwa ashuke, aligoma na kusema lazima afanye kazi japo kidogo.
Ndipo akaanza kuimba nyimbo za kiarabu na zile za Unyago ambazo inasemekana yeye ndiyo huzitumia kuwafundisha mabinti wanaojiandaa kuolewa.

Bi Kidude pia alitoa fursa kwa mashabiki wake kumuuliza maswali mbalimbali, ambapo aliwajibu katika namna ya kuchekesha.

Wiki mbili zilizopita, Baraza la Sanaa Zanzibar, liliwazuia waandaaji wa tamasha hilo kumtumia mkongwe huyo kutokana na hali yake ya afya kuwa dhaifu.