Bi Kidude afariki,kuzikwa leo

Muktasari:

SAUTI ZA BUSARA

Bi Kidude hakuwahi kukosa kushiriki Tamasha la Muziki la Sauti za Busara kwa zaidi ya miaka 10, lakini mwaka huu alizuiwa kutokana na kile kilichoelezwa kuzorota afya yake. Hata hivyo alipopewa nafasi ya kusalimia mashabiki aliamua kuimba kabisa.

 “Muhogo wa Jang’ombe ee, sijauramba mwiko, usitukane wakunga na uzazi ungalipo...mwenda tezi na omo huishia ngamaniii...,” ni sehemu ya mashairi ya wimbo wa Fatma Binti Baraka ‘Bi Kidude’, Muhogo wa Jang’ombe, moja ya nyimbo zilizompa mafanikio.

Sauti ya Bi Kidude, mkongwe wa muziki wa mwambao Afrika Mashariki anayekadiriwa kuwa na miaka zaidi ya 100, haitasikika tena kwenye kumbi za burudani na dhifa mbalimbali baada ya kufariki dunia jana mchana mjini Zanzibar.

Bi Kidude alikuwa gwiji katika muziki wa mwambao, alitunga, kuimba na kushiriki nyimbo nyingi akiwa na Kikundi cha Culture Musical Club cha Zanzibar pamoja na vikundi mbalimbali ikiwa ni pamoja na; Muhogo wa Jang’ombe ambao baadaye aliimba na Judith Wambura ‘Lady Jaydee’, Msondo, Ahmada na Offside Trick, Kijiti, Uzuri wa Mwanaume si sura na Alaminadura.

Kifo chake
Kifo cha Bi Kidude kimekuja ikiwa ni siku chache baada ya kuwapo na taarifa ya kuzorota afya yake kwa miezi kadhaa kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kutokana na uzee.

Kidude ambaye alizuiwa kushiriki Tamasha la Sauti za Busara mwaka huu, aliwahi kuzushiwa kifo mara kwa mara mwaka juzi na mwaka jana, lakini ndugu zake walithibitisha jana kuwa alifariki kwenye  Mji wa Hakuna Matata, katika Kitongoji cha Bububu nje kidogo ya Mji wa Zanzibar na mwili wake umepelekwa Raha Leo kwa maandalizi ya mazishi.

Mmoja wa wajukuu wa ndugu zake, Omar Ameir Makungu alithibitisha jana kuwa Kidude alifariki saa 7 mchana na anatarajiwa kuzikwa leo saa 7, Kitumba karibu na Mwera Wilaya ya Magharibi Zanzibar.

Bi Kidude aliyezaliwa Kitumba kilometa 15 kutoka Mji wa Zanzibar alikuwa anadai baadhi ya familia yake walitoka Congo na Burundi na walikuja Zanzibar wakati wa utumwa.
Iliwahi kuelezwa kuwa katika uhai wake, alionana na Malkia Elizabeth nyumbani kwake nchini Uingereza.

Katika maisha yake hakujaliwa kupata mtoto wa kumzaa ameizunguka dunia katika fani yake hiyo ya kuimba taarabu na katika miaka ya mwisho alikuwa akifanya onesho alikuwa hapendi kuondoka jukwaani.

Kudude ambaye alipewa jina hilo na kuwa maarufu zaidi kuliko jina lake halisi la Fatma kwa vile alizaliwa mtoto ‘njiti’ atakumbukwa zaidi katika mchango wake kwenye sanaa ya muziki wa taarabu akifuata nyendo za mwasisi wa muziki huo Afrika Mshariki, Siti Binti Saad wa Zanzibar.
Mbali na kuimba taarabu, Bi Kidude alikuwa mahiri katika ngoma ya unyago ambayo lengo lake ni kuwafunda wasichana ili kuelewa masuala ya ndoa na kuishi na waume zao vizuri na kuwakabili wanaume wenye tabia chafu.

Bi Kidude alikuwa maarufu mjini Zanzibar, lakini umaarufu wake ulivuka mipaka baada ya mwaka 1984 kufanyiwa kipindi maalumu cha mahojiano katika Televisheni Zanzibar na aliyekuwa Mkurugenzi wa televisheni hiyo, Abdallah Mwinyi Khamis ambaye hivi sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.
Bi Kidude akaanza kuimba zaidi kwenye hafla mbalimbali na wimbo wake wenye zaidi ya miaka 70.

TUZO:
Mwaka 2012 alitunukiwa Tuzo ya ‘Michezo na sanaa’ na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, pia mwaka mwaka 2005 huko Gateshead, Newcastle nchini Uingereza, alitwaa tuzo ya heshima kutoka  World Music Expo (WOMEX) na kuzawadiwa Euro 5,000.

Pia alipata Tuzo ya Maisha ya Tamasha la Filamu la Nchi za Jahazi (ZIFF) mwaka 1999.
Katika kazi zake za usanii, wimbo uliompa umaarufu mkubwa ni ule uliojulikana kwa jina la ‘Muhogo wa Jang’ombe’, sambamba na ‘Ahmada’ alioimba na vijana wa Kundi la Offside Trick.
Enzi za uhai wake aliwahi kusema hafahamu tarehe halisi aliyozaliwa wala mwaka, isipokuwa anachojua ni kwamba alizaliwa wakati rupia ikitumika kama fedha na wakati huo ulikuwa kabla ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia.

Kama watoto wa kawaida alianza kuimba kwa sauti isiyo na mpangilio. Ilipofika mwaka 1920 alianza kuwa kinara wa kuimba na kucheza kwa ustadi ngoma ya unyago.

Bi Kidude alianza kuimba alipokuwa na umri wa miaka 10 na alijifunza kutoka kwa msanii mkongwe na aliyetamba sana enzi hizo Sitti binti Saad.
Wageni wengi kutoka sehemu mbalimbali walikuwa wakifika Zanzibar kuja kumwona Sitti na kwa vile Bi Kidude na Sitti walikuwa wako karibu.

Maisha ya ndoa:
Alipokuwa na miaka 13, kwa mara ya kwanza alitoroka nyumbani kwao Zanzibar na kukimbilia Tanzania Bara, baada ya kulazimishwa kuolewa. Lakini alipokuwa kigoli wa kutosha kuolewa aliolewa ingawa ndoa hiyo haikudumu kutokana na manyanyaso aliyokuwa akiyapata.

Aliamua kukimbilia Kaskazini mwa Misri ikiwa ni katika miaka ya 1930, huko aling’ara katika fani yake ya uimbaji na uchezaji ngoma.
Lakini ilipofika miaka ya 1940 aliamua kurudi nyumbani Zanzibar ambako aliendelea na shughuli zake za uimbaji.

Bi Kidude ameimba muziki wa taarabu katika vikundi mbalimbali na alianza kazi hiyo kwa kuburudisha katika majahazi yaliyokuwa yanachukua Waafrika na Waarabu katika Pwani ya Afrika Mashariki.

Kidude ambaye katika uhai wake alikuwa anadai kuwa aliolewa na wanaume kadhaa na kumwita kila mtu mwanangu alisema kwamba alikuwa anahitaji kupata mtoto, lakini bahati mbaya Mwenyezi Mungu hakumpa.
Kidude umaarufu wake ulitanda zaidi kutokana na sifa ya kuwa ni mwimbaji mwenye umri mkubwa kutumbuiza jukwaani.

Mkongwe huyu wa muziki wa taarab hadi anaiaga dunia hajawahi kutamka kwamba ataacha kuimba kwani alikuwa anasema kuwa kuimba ndiyo maisha yake.
Kidude alitembelea nchi nyingi, ikiwa ni pamoja na Oman, Ufaransa, Hispania, Ufini, Ujerumani na Uingereza.

Mahojiano ya mwisho:
 “Watu wamenizushia kufa, na wewe hukuja kuniona, ulifikiri nimekufa? Mimi  mzima, si unaniona, cheki, ila kitu kimoja tu nisaidie nataka sigara, na kiu sana na sigara, na wewe pia unakataa kunipa sigara.

“Mi nimeshapona si unaona? (anavuta mkono kwa nguvu na kuuminya), siyo unaona nimeshapona mimi niletee sigara ama huniletei basi siongei  tena na wewe.”
“Kweli nilikuwa naumwa, ngozi yote ilivuka hii, nilikonda sana, ila sasa Alhamdulillah mi mzima, mi mzima, naweza ondoka,” alisema akiwa na matumaini makubwa.

Tamasha lake la mwisho:
Mwaka 2012  Baraza la Sanaa Zanzibar lilipiga marufuku kwa promota au mwandaaji wa tamasha lolote kumsimamisha jukwaani Bi Kidude kutokana na afya yake.
Agizo hilo lilikuwa gumu kwa waandaaji wa Tamasha la Sauti za Busara baada ya kumtaka awasabahi mashabiki  hata hivyo akaingia kuimba.
Sauti za Busara 2013, lilikuwa tamasha la mwisho kwa Bi Kidude kutumbuiza.

Wasemavyo wasanii wa taarabu:
Kiongozi wa muziki wa taarabu hapa nchini Shakila Said Khamis anasema tasnia imempoteza mtu muhimu na mwenye kuelewa.

“Tumempoteza mtu mwenye kuelewa na muhimu kwetu, alikuwa mtu asiye na hiyana, lakini Mungu amempenda zaidi.”
Bi Shakila anasema licha ya kuwa mwanamuziki mwenzake, Bi Kidude alimlea na alikuwa kama mama yake pia alimfundisha kuimba muziki huo.

Kiongozi wa Bendi ya Taarabu ya Five Star, Ally Juma ‘Ally Jey’ anasema kifo cha nguli huyo ni pigo kubwa kwa muziki wa taarabu nchini licha ya ukongwe aliokuwa nao.

“Tumempoteza bibi makini aliyekuwa akitusihi tuwe na upendo. Binafsi nitamkumbuka kwa mengi hasa upendo aliokuwa nao na namna alivyojitahidi kutuunganisha. Kikubwa aliutangaza muziki wa taarabu duniani, amezunguka katika mataifa mengi.”

Mwimbaji na kiongozi wa  bendi ya taarabu kutoka Kundi la Mashauzi Classic, Isha Ramadhani ‘Isha Mashauzi’ anasema katika utoto wake alitamani sana kuimba kama Bi Kidude.

Nukuu zake:

“Mimi asili yangu ni Mmanyema wa Kigoma, baba yangu na mama yangu alikuwa Mngindo, lakini baba yangu alilowea Zanzibar, ndipo sisi tukazaliwa huko mpaka sasa naishi Zanzibar, lakini mie Mmanyema.”

“Nchi hii kaitengeneza John Rupia, mimi niko hapa, mama Haambiliki alikuwa anafanya vichekesho, nimemlea mimi, mama mzazi wa mwanamuziki Shakira nimemlea mimi. Hao kina Mzee Yusuf nimewalea wazazi wao.”

“Enzi zetu taarabu ulikuwa mtu ukiisikiliza ufanye kazi kupata maana. Kwanza, watu walikuwa wanaanza kuimba saa nane za usiku, ikifika saa 11 unafungwa muziki. Mimi nashangaa siku hizi taarabu inaanza saa mbili.”

“Nimevuta sigara kabla hujazaliwa na mpaka sasa navuta sijapata TB wala ugonjwa wa mapafu. Nilianza kuvuta sigara aina ya Seven Seven, Mkasi, Simba, Kulindondo, Gundufleki na sasa Embassy na nina uwezo wa kumaliza pakiti moja kwa siku tatu.”

Imeandikwa na Masoud Sanani, Herieth Makwetta na Vicky Kimaro, Zanzibar na Dar es Salaam, Mwananchi