Uanaume haulindwi kwa kupuuza hisia

Nimekuwa nikizungumzia dhana ya uanaume na madhara yake kwa afya ya akili ya wanaume. Ikiwa hukuweza kusoma makala zilizopita, nilirejea kidogo tafiti mbalimbali zinazoonesha kuwa wanaume wengi wanakufa kabla ya wake zao. Ukifuatilia wastani wa kuishi kwenye nchi mbalimbali duniani, mwanamume anakuwa chini ya mwanamke kwa miaka kadhaa.

Tunaweza kufanya mambo kadhaa kumsaidia mwanamume. Kwanza, haja ya kujenga jamii inayoamini katika usawa wa kijinsia. Nisimumunye maneno. Usawa katika mahusiano ni suluhisho la kwanza kumsaidia mwanamume kuishi maisha yasiyo na shinikizo kubwa la kujitwisha majukumu yote begani mwake.

Usawa ni neno rahisi kulisema, lakini inapokuja kwenye maisha halisi hali inakuwa tofauti. Kuna wakati unaweza kushangaa hata wanaohubiri usawa wa kijinsia, hawaamini wanaweza kubeba majukumu ya familia ambayo kwa kawaida, ingetarajiwa abebeshwe mwanamume.

Lakini pia, kuna hili la wanaume wenyewe kutokuwa na tabia ya kujenga mahusiano ya karibu na watu. Haishangazi, mathalani, mwanamume kuwa na watu anaozungumza nao mara kwa mara lakini sio marafiki zake. Tizama wanayozungumza maofisini, mitaani na mitandaoni. Kama sio mpira, basi ni siasa. Kama sio siasa basi kutambiana biashara, kazi, vitu na ashakumu sio matusi, uwezo wa kuwapata wanawake.

Nadra sana kukuta mwanamume anazungumzia mambo yanayousuka suka moyo wake. Hatupendi kusema yanayotusumbua. Hatupendi kusema yanayotuogopesha. Hatupendi kusema yanayotusuta moyoni. Tumeaminishwa kuwa kuficha zile aibu zetu huo ndio uanaume.

Hali hii inachangia sana kuzorotesha afya ya akili ya mwanamume. Mtu anakuwa na mambo mengi yanayomzonga zonga na anaamua kuulinda uanaume wake kwa kunyamaza. Unakutana na mtu anacheka kicheko bandia lakini moyoni kajaza mengi. Unakutana na mtu anazungumzia mpira unaamini hana baya, lakini anawaza mengi yanayomnyima usingizi.

Tofauti na wanaume wengi, wanawake hawaoni shida kusema yanayowasumbua. Asipomwambia mpenzi wake, atazungumza na rafiki yake. Asipozungumza na rafiki yake, atazungumza na yeyote mtaani na hakuna mtu atamshangaa. Kuzungumza kunawasaidia sana wanawake kupumzisha mioyo yao, jambo ambalo kwa mwanamume inakuwa kama kuweka rehani uanaume wake.

Mahusiano ya karibu na watu ni hitaji la kimaumbile. Ukitaka kujua hili halina jinsia tazama watoto. Hata mtoto wa kiume hawezi kuishi mbali na mbeleko ya mtu anayeweza kumkimbilia michezo inapomgombanisha na wenzake. Usalama wake ni kuwa na mtu wa kumkimbilia. Bahati mbaya, katika tamaduni nyingi mtoto wa kiume amekuzwa kuamini hahijitaji mtu wa karibu wa kumfunulia moyo wake.

Mwanamume, kwa kutokuelewa umuhimu wa ukaribu, anaweza kuwa hata na mke wake na bado akakosa ujasiri wa kumwambia vitu vinavyomsumbua na kuinyanyasa nafsi yake. Hawa ndio wanaoulinda uanaume kwa fedha na wanasahau kuwa na wao pia wana mengi yanayohitaji msaada wa kusikilizwa.

Juzi nilikuwa natazama tofauti za kijinsia kanisani kwetu. Kila baada ya ibada, unasikia, “Wanawake wabaki.” Unaona wanabaki. Wanajua umuhimu wa kuwa pamoja na kuna mambo wanashirikishana. Mwenzao amepatwa na shida. Wanakwenda kumtembelea. Hata mwanamke anapokuwa na changamoto zake nyumbani, kanisani ana kundi kubwa la wenzake wanaoweza kumbeba. Ukienda kwenye ibada za katikati ya juma, walio wengi ni wanawake. Wanawaume watasema wana majukumu mengi. Huko waliko hawana mtu wa kusema nao mambo ya kina yanayogusa hisia zao za ndani. Hawaoni sababu ya kukusanyika. Ukiwauliza watasema, wana mambo mengi ya kufuatilia.

Ukichunguza hata baada ya ibada, wanaume wengi wanafanya haraka kondoka. Hawana muda wa kuhusiana na wengine zaidi ya salamu fupi fupi zenye haraka. Kazini wanakotumia muda mwingi hali haiwezi kuwa tofauti sana.

Mitaani wanakokwenda kupumzikia hali haiwezi kuwa tofauti. Nani anaweza kusikiliza changamoto zao?