Wanne mbaroni kwa wizi wa mota za mashine za kusaga

Muktasari:

  • Katika msako huo Jeshi la Polisi limefanikiwa kukamata mota 20 katika maeneo mbalimbali ikiwemo Iringa, Wanging'ombe na Njombe.

Njombe. Jeshi la Polisi Mkoa wa Njombe linawashikilia watu wanne kwa tuhuma za kuhusika katika matukio ya wizi wa mota za mashine za kusaga nafaka zilizoibiwa kwenye maeneo tofauti hapa mkoani Njombe.

Hayo yamebainishwa leo Machi 28, 2024 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu matukio hayo.

Amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Betod Mtitu (38) ambaye ni dereva teksi eneo la Mji Mwema, Njombe, Emmanuel Chengula (24), fundi na mkazi wa Zengerengeti Njombe, Nassoro Chura (35) na Omary Manga (42), mkazi wa Ramadhani, Njombe.

Amesema baada ya kukamatwa kwa Mtitu kutokana na taarifa za raia wema, jeshi hilo lilifanikiwa kukamata mota 20 katika maeneo mbalimbali ikiwemo Iringa, Wanging'ombe na Njombe.

Amesema baada ya wizi huo, watuhumiwa hao walikwenda kuziuza na zingine kuzificha kwenye maeneo hayo tofauti.

Amesema jeshi hilo linawashikilia watuhumiwa wengine wawili Nerbert Mehenge (54), mkazi wa Nanenane na Tesifora Mgaya (32), mkazi wa Lupande, Ludewa wakiwa na gari aina ya Toyota Carina, rangi ya silver ambalo alidai wanalitumia katika kutapeli watu wakijifanya wanauza madini.

“Hawa watu wanajihusisha na masuala ya utapeli wa madini ya dhahabu na hapa Njombe wamekuwa wakifanya utapeli wa madini ya dhahabu na wamepora watu mbalimbali,” amesema Banga.

Amesema baada ya kukamatwa na kupekuliwa walikutwa na simu sita, madini feki, tochi tatu za kumulikia madini na vibao 64 vya kuwadanganyia watu kuwa ni fedha pamoja na bahasha tupu 10.

Amesema watuhumiwa hao wamefikishwa mahakamani kwa makosa ya utapeli na uchunguzi unaendelea kwa makosa mengine.

Amesema sambamba na hilo, Jeshi la Polisi linawashikilia watuhumiwa watatu huko Ludewa kwa kosa la mauaji ya Rainel Mapunda (60), mkazi wa Kimelembe ambaye aliviziwa akiwa anatoka kwenye kilabu cha pombe ya kienyeji na kujeruhiwa kwenye paji la uso na shingoni kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali.

Amesema chanzo cha mauaji hayo ni imani za kishirikina akidai marehemu anatuhumiwa kuhusika katika kifo cha mwanae wa kiume, aliyefariki kwa ajali ya gari mkoani Ruvuma.

“Hawa ndugu walikuwa wanatuhumu kuwa ajali ile imesababishwa na huyu marehemu ambaye ameuawa,” amesema Banga.