Wananchi Tambani wajenga daraja la miti

Muktasari:

Tangu mvua za masika zilipoanza wakazi hao wamekuwa wakilazimika kulipa Sh500 ili kuvushwa  kwenye  maboya na vivuko vya mbao kutokana na bonde hilo kukosa daraja.

 

Mkuranga. Wakazi wa kata ya Tambani wilayani Mkuranga wameunganisha nguvu na kujenga daraja la miti katika bonde la Mkoga ili kuwarahisishia mawasiliano kati ya Tambani na Mbande.

 Tangu mvua za masika zilipoanza wakazi hao wamekuwa wakilazimika kulipa Sh500 ili kuvushwa  kwenye  maboya na vivuko vya mbao kutokana na bonde hilo kukosa daraja.

 

Pamoja na lengo la kukabiliana na gharama za kuvushwa wakazi hao walilenga kuwahakikishia usalama watoto wao wanapokwenda na kurudi kutoka shule.

 

Wakizungumza na gazeti hili wakazi hao wamedai kuwa wamechoka kulalamika hivyo wameamua kuchukua hatua.

 

Mmoja wa wakazi hao Hamad Soboga amesema suala la bonde hilo kukosa daraja limekuwa likiwaumiza kwa muda mrefu.

 

"Jambo linalotupa uchungu ni kuwaona watoto wetu wanashindwa kwenda shule kwa sababu ya maji kujaa, kuna wakati tunalazimika kwenda nao ili tuwavushe na kuwasubiri wanaporudi yaani kwa kifupi ni mtihani,"

 

"Tukakaa na kujiuliza adha hii hadi lini wacha tuumize akili tufanye ubunifu na hatimae tukakubaliana tujichangishe na wenyewe tujitoe tutengeneze daraja hili la miti,"

 

Kwa upande wake Maulid Antony 'Makaburi' amesema wameona kilio chao cha  muda mrefu hakisikiki ndiyo maana wakachukua hatua hiyo.

 

"Yaani huku tumekuwa kama tunajiongoza wenyewe, Serikali ya wilaya ni kama haitutambui  sasa tumeona isiwe shida wacha tujishughulishe ili tupate urahisi wa kufika kwenye majukumu yetu na watoto kwenda shule,"

 

Naye Siwema Said ameongeza  hatua hiyo na kueleza kuwa itawakomboa wakazi wa Tambani. "Ilikuwa hatuna raha watoto wakienda shule,unabaki roho juu hujui atarudi salama au lah, ingawa hata sasa bado naona unafuu utakuwepo,"

 

"Kilio chetu kinabaki pale pale Serikali itusikie tuna shida sana wakazi wa Tambani, hili bonde limekuwa kikwazo wakati mwingine hata mvua haijanyesha hapa lakini maji yanatoka mbali yanakuja kufurika,"

 

Amesema  hali ya eneo hilo kufurika maji inaleta hofu hasa inapotokea kuna mgonjwa au mjamzito anayetakiwa kuwahishwa hospitalini.

 

 

Hatua hiyo ya wananchi imekuja ikiwa ni wiki mbili baada ya gazeti hili kutoa habari kuhusu kukosekana kwa daraja katika eneo hilo.

 

 

Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya  ya Mkuranga Mhandisi Mshamu Munde amesema  ofisi yake inatambua changamoto hiyo na inaifanyia kazi.