Uchumi watikisa shule binafsi

Muktasari:

Ni ya shule za binafsi baada ya kukosa wanafunzi kwa kile kinacholalamikiwa na wamiliki kuwa ni kutokana na sera ya elimu bure kwa shule za Serikali

Dar es Salaam. Baadhi ya Majengo ya shule binafsi za msingi na sekondari yako hatarini kubadilishiwa matumizi kutokana na kukosa wanafunzi wa kutosha baada ya Serikali kuboresha shule zake na kutoa elimu bure, huku hali ya kiuchumi ikizidi kuwaumiza wananchi.

Wakati Serikali imeondoa posho, kudhibiti safari za nje na ndani katika jitihada za kudhibiti matumizi, biashara zimedorora, hali ya kukopesheka imeshuka, mambo ambayo yamefanya wazazi kulazimika kuwahamishia watoto wao katika shule za Serikali ambazo gharama zake ziko chini ili kukabiliana na hali ngumu ya maisha.

Uchunguzi wa Mwananchi uliolenga kujua athari za moja kwa moja kwa shule binafsi baada ya Serikali kuamua kutekeleza ahadi yake ya kutoa elimu bure kuanzia msingi hadi kidato cha nne, umebaini kwamba baadhi ya shule zinaweza kufungwa na majengo yake kubadilishwa matumizi iwapo hali haitarekebishwa.

Tayari baadhi ya wamiliki wa hoteli wamegeuza majengo yao kuwa hosteli kwa ajili ya wanafunzi wa vyuo, ofisi au maghala baada ya kubadilika kwa sera za matumizi na hali hiyo inainyemelea sekta ya elimu.

Hofu hiyo ililifanya Shirikiko la Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi (Tamongsco) kumfuata Waziri wa Elimu, Teknolojia na Sayansi, Profesa Joyce Ndalichako kujadiliana naye ili kupata ufumbuzi wa pamoja.

Elimu bure ni utekelezaji wa ahadi iliyomo katika Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu uliopita, na mgombea wake, Rais John Magufuli alianza kuitekeleza wakati shule zilipofungua mapema Januari.

Watoto wengi waliandikishwa kuanza masomo katika shule za msingi za Serikali mwaka huu na waliofaulu kuingia kidato cha kwanza, walijiunga na shule za Serikali na uwezekano wa mwenendo huo kuendelea ni mkubwa.

Hii ni tofauti na ilivyokuwa miaka iliyopita wakati wazazi wengi walipokuwa wakipendelea kuwapeleka watoto wao shule binafsi zinazotumia lugha ya Kiingereza, au kutowapeleka shule za Serikali iwapo wanafaulu darasa la saba.

Hofu ya shule kufungwa ni dhahiri kwani baadhi ya shule za sekondari mwaka huu zilipata wanafunzi wa kujaza mikondo miwili tu kati ya mitatu ya kidato cha kwanza.

Mwenyekiti wa Tamongsco, Mrinde Mzava amesema uamuzi wa Serikali kutoa elimu bure, ulizitenga shule binafsi katika utekelezaji.

“Kuanzishwa kwa shule binafsi ilikuwa kuitikia wito wa Serikali ambayo ilituomba wadau wenye uwezo wa kuwekeza kwenye elimu, tujitokeze. Tukajitokeza kwa nia ya kuinua na kuwezesha upatikanaji wa elimu nchini, ni wazi kuwa uamuzi huo imetutenga,” alisema.

Mzava alisema hadi sasa hakuna mfumo wowote unaoonyesha jinsi ambavyo shule binafsi zinaweza kwenda sambamba na utekelezaji wa elimu bure ili ziweze kuendelea kujiendesha.

“Kwa hali inavyokwenda ni wazi majengo ya shule nyingi baadaye yatageuka kuwa madanguro au baa. Lakini kama kungekuwa na ushirikishwaji kulingana na mazungumzo tuliyofanya na Profesa Ndalichako mambo yangekuwa mazuri kwa pande zote,” alisema.

Aidha, mawakala wa shule mbalimbali jijini Dar es Salaam ambao hutumika kutoa fomu za kujiunga na elimu ya sekondari wameeleza kwa nyakati tofauti kuwa kuna mabadiliko ikilinganishwa na miaka iliyopita.

“Mimi nimekuwa nikitoa fomu za shule mbalimbali. Tangu mwaka 2006 nafanya shughuli hiyo. Nimebaini tofauti kubwa kwa mwaka huu, uchukuaji fomu ni wa kusuasua,” alisema wakala huyo ambaye alikataa jina lake kutajwa gazetini na kuongeza: “Miaka iliyopita wapo wazazi waliokuwa wanachukua fomu hata za shule tano, lakini safari hii ni mbili tena anataka kwanza kujua kiwango cha ada.”

Mwenyekiti wa Tamongsco Kanda ya Dar es Salaam, Charles Totera alisema kutokana na uzoefu wake amebaini kuwa wazazi wengi huwa wazito kulipa ada ya awamu ya mwisho, Septemba hadi Desemba.

“Tofauti ninayoiona kwa mwaka huu ni kwamba uzito umeongezeka ingawa siwezi kusema ni kwa kiasi gani, lakini kilio cha hali ngumu kinasikika. Nafikiri hadi mwezi Februari mwakani tunaweza kupata tathmini nzuri ya wapi tunaelekea,” alisema.

Totera, ambaye ni mmiliki wa shule ya Totera, alisema hali hiyo imewaweka katika wakati mgumu wamiliki wengi wa shule, kiasi cha kufanya ulipaji wa mishahara na huduma muhimu kama chakula umekuwa wa mashaka.

Mtazamo wake unalingana na mmiliki wa shule ya awali na msingi ya Fortune, Hope Kaiza aliyesema kilio hicho cha wazazi kimemfikia.

“Wapo waliokuja kuniambia wanalazimika kuwahamishia watoto wao shule za Serikali kwa sababu hali ni ngumu hawawezi kumudu kulipa ada. Ni jambo la kuhuzunisha kwa sababu shuleni kwangu nilikuwa nawaruhusu kulipa ada kwa awamu nne na wengi walimudu,” alisema Kaiza ambaye shule yake iko Tabata Kinyerezi.

Kaiza alisema miongoni mwa wazazi hao wapo watumishi wa Serikali na wafanyabiashara. “Shule kufungwa si jambo rahisi kutokana na idadi kubwa ya watoto na uwezo wa shule za Serikali, lakini ukweli unabaki pale pale kwamba tunakumbana na changamoto ya hali ngumu ya maisha na uhamisho wa watumishi wengine kwenda Dodoma,” alisema.

Hali ni tofauti kwa mmiliki wa shule za sekondari za Paradigms, Mahmoud Mringo ambaye anasema tatizo ni wazazi kushindwa kujipanga kwa bajeti za maendeleo ya kifamilia kama ada na badala yake kuelekeza fedha katika mambo ya anasa.

“Sasa hii elimu bure ndiyo imewaharibu wengine. Wanaona kwamba elimu ni jambo jepesi. Wanaingia gharama katika kunywa bia na vitu vingine vya anasa. Badala yake wanashindwa kujipanga. Ikifika Januari na Februari ni kilio na kuomba kuvumiliwa,” alisema Mringo.

Alisema kwa sasa kuna mabadiliko tofauti na walivyozoea wengi kutokana na kukosa mipango ya kujipatia fedha au kutokuwa na uhakika wa kupata kipato cha ziada.

“Ni changamoto. Yaani imefika wakati ukimpigia mtu simu, hata kupokea anaogopa. Anajua unamkumbushia deni analodaiwa. Tunaona mengi si kwenye ada tu, hata kwenye huduma nyingine. Mtu asipojipanga atashindwa kulipia maji, umeme na huduma za afya,” alisema Mringo.

Mmoja wa wazazi aliyeathiriwa na hali ngumu ya uchumi, Edgar John, alisema kuwa anasomesha watoto wake shule ya kisasa, lakini alikwama kulipa ada baada ya biashara zake kwenda vibaya.

“Watoto walirejeshwa nyumbani, wakakaa wiki mbili huku nikiendelea kuhangaika kwa imani kwamba naweza kufanikiwa kupata fedha za kuwalipia, lakini ilishindikana na nikajadiliana na mama yao tukaamua kuwatafutia uhamisho,” alisema.

Mzazi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Yassin Yakubu alisema mtoto wake anasoma shule ambayo inasifika kwa ufundishaji na mara kadhaa imetoa wanafunzi bora kitaifa, lakini anafikiria kumhamishia shule ya ada nafuu baada ya kipato chake kuyumba.

 

Iandikieni wizara

Wakati wamiliki wa shule wakilalamikia kupungua kwa idadi ya wanafunzi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Maimuna Tarishi amewataka Tamongsco kuiandikia barua wizara hiyo kuhusu matatizo yao ili yaweze kushughulikiwa.

“Kama walizungumza na waziri, wafuate utaratibu unaotakiwa kuuliza mrejesho wa mazungumzo yao,” alisema katibu huyo.

Kati ya mapendekezo yanayoweza kuwa kwenye barua hiyo iwapo wataandika ni wamiliki wa shule binafsi kuingia ubia na Serikali.

“Wakati Serikali imekuwa na uhaba wa majengo, shule binafsi hazina wanafunzi hivyo madarasa yapo wazi. Kumbe Serikali ingeweza hata kukodi madarasa kwa mapatano ya bei mambo yangekuwa mepesi, watoto wangenufaika kwa elimu bora,” alisema mwenyekiti wa Tamongsco.