Uchaguzi mdogo kata 22 picha ileile ya uchaguzi 2024, 2025

Muktasari:

  • Machi 20, 2024 kata 22 zilifanya uchaguzi wa madiwani na Chama cha Mapinduzi (CCM) kilinyakua zote huku zikiibuliwa dosari mbalimbali ambazo zimechambuliwa na wadau wakionyesha njia.

Dar es Salaam. Uchaguzi mdogo uliofanyika Machi 20, 2024 katika kata 22 nchini umepokewa kwa hisia tofauti na wadau wa demokrasia, wakisema ni kipimo halisi cha uchaguzi ujao wa serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu mwaka 2025.

Katika uchaguzi huo, wapo waliocheka na waliolia kutokana na yaliyofanyika. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeshinda kata zote huku wapinzani wakilia kuchezewa rafu na chama hicho, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Jeshi la Polisi.

Hata hivyo, taasisi hizo zilizolalamikiwa zimepuuza madai hayo zikisisitiza mwenye malalamiko afuate sheria na kama ana ushahidi aende mahakamani.

Akijibu tuhuma hizo, Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime amesema majukumu ya chombo hicho yapo kisheria, ikiwamo kulinda maisha ya watu na mali zao, kubaini na kuzuia uhalifu, kusimamia sheria na kulinda amani na si kulumbana na mtu yeyote yule kwenye vyombo vya habari.
“Kama kuna mtu mwenye malalamiko yenye ushahidi afuate sheria kama inavyoelekeza ili tuhuma hizo zichunguzwe.

Pia, kama kuna malalamiko juu ya uchaguzi sheria inaelekeza ni nini cha kufanya na si kujenga chuki katika jamii,” anasema Misime.

Jibu alilolitoa Misime linafanana na lililotolewa na Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi aliyesema sheria za nchi zipo wazi, kama (wanaolalamika) wanahisi mambo hayakwenda vizuri waende mahakamani na si vinginevyo.

“Sheria inasema unaenda mahakamani kama una ushahidi, ukiona mtu hataki kufuata utaratibu anaenda kufanya mkutano na vyombo vya habari, maana yake mambo anayoongea ni ya kutunga na mimi siwezi kusimama kujibu mambo ya kutunga,” alisema Dk Nchimbi.

“CCM matumaini yetu waliochaguliwa walifanya kampeni kistaarabu na wale wenye wasiwasi wafuate taratibu za kisheria, wakiendelea kupiga kelele wanataka huruma,” alisema alipozungumza na Mwananchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Habari na Elimu kwa Mpigakura wa NEC, Giveness Aswile alisema wasimamizi wa uchaguzi kwenye halmashauri husika ndio wanaweza kuzungumzia kasoro husika.


“Wanaopaswa kujibu malalamiko (ya udanganyifu) ni wasimamizi wa uchaguzi kwenye halmashauri, lakini Tume inasubiri ripoti kutoka maeneo yote na tutafanya tathimini baada ya kupokea taarifa ya utendaji,” alisema Aswile akinukuliwa na Mwananchi.

Dosari zilizoibuliwa
Katika uchaguzi huo, mambo mbalimbali yamejitokeza, mengi yakilalamikiwa na wadau, hasa vyama vya siasa, ikiwamo ushiriki mdogo wa vijana kwenye upigaji kura, udanganyifu katika mchakato wa uchaguzi, ukamataji wa wagombea na mengine.
Hata hivyo, wasimamizi wa uchaguzi kwenye maeneo husika wamesema hakukuwa na udanganyifu wowote na uchaguzi ulienda vizuri hadi hatua ya ya kutangaza matokeo.


Malalamiko ya udanganyifu

Baadhi ya viongozi walitoa malalamiko kuhusu hali ilivyokuwa kwenye kata zao katika uchaguzi, huku wakiitupia lawama Tume ya Uchaguzi.

Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo – Tanzania Bara, Issihaka Mchinjita amedai chama chake kilishuhudia watu wakitumbukiza kura bandia kwenye masanduku na jambo hilo lilifanyika kwenye kata zote zilizofanya uchaguzi.

“Wasimamizi wa uchaguzi waliwanyima nakala za matokeo mawakala wa vyama vya siasa na hawabandika matokeo kwa kisingizio cha ‘kukosa gundi. Hili limefanyika kwenye Kata ya Kabwe, Jimbo la Nkasi Kaskazini,” amesema Mchinjita.
Akitoa tathimini ya uchaguzi huo hivi karibuni, mbunge wa Nkasi Kaskazini, (Chadema), Aida Kenani anasema mambo yaliyofanyika kwenye uchaguzi wa mwaka 2020 bado yanaendelea kwa kilichotokea kwenye kata hiyo.
“Wananchi walitimiza wajibu wao wa kupiga kura na mgombea aliyewekwa kupitia Chama cha ACT Wazalendo alishinda kwa ushahidi kabisa, kilichofanyika ni uporaji na kinanyong’onyesha Watanzania umuhimu wa kwenda kupiga kura,” anasema.

Hata hivyo, wakati wadau hao wa uchaguzi wakilalamika, baadhi ya wasimamisi wa uchaguzi waliutetea.

Msimamizi wa uchaguzi, Kata ya Chiputa, Ibrahim Mwanauta anasema katika kituo alichosimamia, uchaguzi huo ulifanyika kwa uhuru na haki na ndiyo maana ulimalizika salama.
“Kituo nilichosimamia tulimaliza salama, hakuna sehemu yoyote iliyoleta shida, sasa sijajua kama kulikuwa na shida nyingine lakini kama msimamizi, uchaguzi ulikuwa huru na haki,” anasema.
Msimamizi wa Uchaguzi Kata ya Kabwe, William Mwakalambile naye anasema hadi shughuli ya uchaguzi inaisha hakukuwa na malalamiko yaliyofikishiwa na kama wanaona haki ilipotoshwa waende mahakamani.

“Sina taarifa kama hawakutendewa haki, sijajua ni haki ipi ambayo hawakutendewa, taratibu zote zilizingatiwa kama maelezo ya Tume yanavyotaka na hakuna kilichokiukwa,” anasema.



Bila sheria yataendelea

Licha ya utetezi wa wasimamizi, Said Msonga ambaye pia ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa, anasema bila kubadilisha sheria zilizopo, malalamiko hayo hayawezi kupungua kwa sababu watendaji wengi wanafanya kazi kwa mazoea.
“Naamini kama kweli kuna nia ya dhati na utashi, itakaposainiwa ile miswada mitatu iliyopitishwa na Bunge, inaweza kuwa msaada kwa kuwa mabadiliko yataanzia ndani ya Tume,” anasema Msonga.

Lakini mchambuzi mwingine, Kiama Mwalimu yeye anasema kwa kuwa dosari zinazolalamikiwa ni tuhuma, ni muhimu kwa wenye ushahidi kwenda mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake na jamii ijue ukweli.
“Kulalamika peke yake hakutoshi bila kuwa na ushahidi na haya ni mambo ya kisiasa, kila mtu anakuwa na michezo yake ili aweze kumzidi mshindani wake, lakini kama mazingira hayo hayakuwa ya haki, vyombo vya sheria inabidi vitumike kutafsiri,” anasema Mwalimu.
Anasema aliyeshindwa anatoa malalamiko, hata aliyeshinda angejikuta katika mazingira hayo pia, kwa kutoka hadharani kueleza yake.
“Suluhisho ni kuweka ushahidi mezani na Mahakama ni chombo chenye uwezo huo, lakini kulalamika hivihivi haiwezi kusaidia si kwa chama cha upinzani au tawala,” anasema mchambuzi huyo.


Vijana hawana imani tena

Kuhusu ushiriki mdogo wa vijana,
msomi wa sayansi ya siasa, Dk Paul Loisulie anasema vijana wengi hawana imani na mchakato wa upigaji kura kwa sababu “wanashuhudia sarakasi zinavyopigwa.”
“Pamoja na kwamba rika la vijana ni la utafutaji na hawako tayari kupoteza muda kwenye foleni, lakini wengi ukizungumza nao wanaeleza jinsi wanavyokatishwa tamaa na siasa zetu za wenye fedha kupewa nafasi na kutangazwa washindi, hata kama hawakubaliki kwa wananchi,” anasema Dk Loisulie.