Rais Samia: Tanzania itaisaidia Somalia kuimarisha ulinzi

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Samia Suluhu Hassan akiwa pamoja na mgeni wake Rais wa Shirikisho la Jamhuri ya Somalia Dk Hassan Sheikh Mohamud wakati alipowasili katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es Salaam leo Aprili 27, 2024.

Muktasari:

Serikali za Tanzania na Somalia zimekubaliana  mambo matatu yanayolenga kukuza na kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo zilizopo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Rais Samia: Tanzania itaisaidia Somalia katika ulinzi

Serikali za Tanzania na Somalia zimekubaliana  mambo matatu yanayolenga kukuza na kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo zilizopo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Bakari Kiango

Dar es Salaam. Viongozi wakuu wa nchi za Tanzania na Somalia wamekubaliana masuala mbalimbali ikiwemo kushirikiana katika kukuza diplomasia, sekta za afya na elimu ili kuimarisha uhusiano miongoni mwa mataifa hayo mawili.

Viongozi wa mataifa hayo, Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Shirikisho la Somalia, Dk Hassan Sheikh Mohamud wameeleza hayo leo Jumamosi  Aprili 27, 2024 Ikulu jijini Dar es Salaam, wakati wa mkutano wao na wanahabari.

Hii ni ziara ya kwanza ya Rais wa Somalia nchini tangu ashike madaraka. Jana Ijumaa Aprili 26, 2024 alihudhuria maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, sherehe zilizofanyika uwanja wa Uhuru mkoani Dar es Salaam.

Rais Samia amesema licha ya Tanzania na Somalia kuwa na uhusiano na mwingiliano kwa miaka mingi, lakini katika mazungumzo yao wamegusia kuimarisha zaidi ushirikiano na uhusiano baina ya mataifa hayo mawili.

"Tumeona kuna umuhimu wa kuwa na mfumo rasmi wa kuimarisha uhusiano huu, ni dhamira yetu kuimarisha mikutano ya ushirikiano baina ya Tanzania na Somalia, kupitia mikutano yetu ya kisekta tutaibua maeneo na miradi ya ushirikiano yenye manufaa kwetu sote.”

"Tumekubaliana mawaziri wetu wa kisekta na wataalamu wakiratibiwa na mawaziri wa mambo ya nje, wakutane wazungumze kisha tuibue maeneo ya ushirikiano," amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema Tanzania inapongeza jitihada za Somalia za kuendeleza vipaumbele vyake vya kitaifa na kusimamia ajenda za Taifa lao kupitia mashauriano ya kisiasa sambamba na kurudisha amani ya nchi yao.

Amesema Tanzania itaendelea kuunga mkono jitihada za kurejesha amani katika taifa hilo.

 "Tumewahakikishia kuwa tutaendelea kusisitiza umuhimu wa kuondolewa kwa zuio la ununuzi wa silaha kwa jeshi la Somalia ambalo limewekwa, hatua itakayowezesha, vyombo vya ulinzi na usalama na Serikali ya Shirikisho la Somalia kutimiza wajibu wao au kujilinda wenyewe.”

"Kama mnavyojua hali ya wenzetu haipo vizuri sana kwa hiyo tumewahakikishia kuunga mkono katika kujenga uwezo wao kama nchi kujilinda wenyewe," amesema Rais Samia.

Pia, Rais Samia amesema Serikali ya Somalia imekuwa ikichukua hatua kubwa za kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii, hivyo wamekubaliana kuimarisha uhusiano katika maeneo hayo hasa kwenye sekta za afya na elimu.

Amesema Serikali ya Tanzania imewapa mwaliko wakati wowote Somalia wakitaka  msaada katika sekta za elimu na afya kuja nchini kuzungumza na wapo tayari kuwasaidia.

Kwa upande wa ushirikiano wa kimataifa na kikanda, Rais Samia ameipongeza Somalia kwa hatua ya kuingia kuwa mwanachama wa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

"Tumezungumzia umuhimu wa nchi zetu za kuchukua hatua za makusudi za kukuza biashara na uwekezaji ili watu wetu watumie fursa hizo ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, tumemuahidi ushirikiano wetu katika majukwaa ya kikanda na kimataifa ambapo nchi zetu ni wanachama," amesema Rais Samia.

Kwa upande wake, Dk Mohamud amemshukuru Rais Samia kwa mwaliko wake wa kuja nchini, akisema Tanzania na Somalia ni washirika wa karibu iliyotokana na misingi ya kuheshimiana.

"Dada yangu (Rais Samia), nimefurahi sana na mazungumzo yetu ya kimkakati ya kuongeza ushirikiano, Somalia tuna njia mbalimbali za kujenga uchumi na tumefanikiwa kushusha deni la Taifa. Tuna furaha kuwa sehemu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.”

"Ushirikiano huu utawezesha Somalia na Tanzania kutumia vema fursa zilizopo, tunashukuru sana kwa uongozi wako na ulivyo mwema kwetu sisi. Pia ushirikiano huu utaleta manufaa kwenye ulinzi na usalama na ushirikiano wa kikanda," amesema Rais Mohamud.

Rais Mohamud amesema nchi yake inaheshimu mifumo na sheria za kimataifa hivyo dhamira ya Serikali ya Tanzania kusimama nao ni msaada mkubwa kutokana na nyakati walizozipitia.

"Tutaendelea kuomba msaada wa uzoefu katika sekta mbalimbali za utaalamu. Somalia tutaendelea kubadilisha uzoefu ili kujenga amani na utulivu," amesema Rais Mohamud.