Mpina 'anavyobanana' na CCM

Luhaga Mpina

Muktasari:

  • Mpina amekuwa kwenye msuguano na uongozi wa chama hicho mkoani Simiyu, kiasi cha kuitwa kwenye Kamati ya Usalama na Maadili ya chama  ya Wilaya ya Meatu na kuhojiwa.

Bariadi. Kauli ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Shemsa Mohammed ya kumtaka Mbunge wa Kisesa Wilaya ya Meatu mkoani humo, Luhaga Mpina kuacha siasa alizoziita za ‘majitaka’ imeendelea kukoleza msuguano kati ya mbunge huyo na chama chake.

Mpina amekuwa kwenye msuguano na uongozi wa chama hicho mkoani Simiyu, kiasi cha kuitwa kwenye Kamati ya Usalama na Maadili ya chama  ya Wilaya ya Meatu na kuhojiwa.

Waziri huyo wa zamani wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi alihojiwa na kamati hiyo Januari 25, mwaka huu katika ofisi za CCM wilayani humo, akitakiwa kujibu tuhuma mbalimbali zilizokuwa zinamkabili, ikiwemo iliyodaiwa ni “kutofanya mikutano, kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.”

Mara baada ya kamati hiyo kumaliza kumhoji, suala hilo lilipelekwa ngazi ya mkoa kwa hatua zaidi. Hata hivyo, tangu wakati huo, hakuna taarifa ambazo zimekwishatolewa kuhusu hatua zilizochukuliwa.

Wakati suala hilo likiwa halijawekwa wazi hadharani, Aprili 25 mwaka huu, katika mkutano wa ndani uliofanyika katika Tarafa ya Kanadi, Kata ya Langangabilili wilayani Itilima, Shemsa ameibua madai mapya dhidi ya Mpina.

Miongoni mwayo ni kumshutumu Mpina “kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake ya kijimbo na kubaki kupambana na mawaziri”.

Pia mwenyekiti huyo anamshutumu Mpina kwa kuibua suala la kifo cha hayati John Magufuli,  Rais wa awamu ya tano, ambaye alifariki dunia Machi 17, 2021.

“Badala ya kuhangaika na matatizo ya wananchi, anahangaika na sababu ya kifo cha Rais Magufuli, aliyetuumba ndiye anajua lini na saa ngapi atatuchukua.”

“Anasema mawaziri hawafai, yeye alikuwa waziri hata salamu kwa wananchi wake alikuwa hawezi kuwasalimia, alitusaidia nini wananchi wa Simiyu alipokuwa waziri, arudi jimboni akatatue kero za wananchi,” amesema.

Hata hivyo, Mwananchi lilipomtafuta Mpina kwa simu akiwa Dodoma ili azungumzie madai hayo, amesema hana cha kuchangia katika hilo kwa kuwa yeye yuko bungeni Dodoma akiendelea na majukumu yake ya kwenye Kamati za Bunge.

“Mimi siwezi kuongelea alichokisema Mwenyekiti wa Mkoa wa Simiyu, niko bungeni naendelea na vikao vya Kamati za Bunge. Siwezi kuongelea mambo aliyosema katika mkutano wake wa hadhara alioufanya kwenye jimbo, ambao sikuhudhuria na nitaongeleaje nini alichokisema mtu mwingine," amesema Mpina.

Mmoja wa wajumbe wa vikao vya uamuzi ndani ya chama hicho wilaya ya Meatu, amesema suala la mbunge wao kuendeleza mapambano bungeni limekuwa linawaweka katika wakati mgumu.

“Unajiuliza hivi mbunge wetu anataka nini, akisimama huko bungeni yeye utaona anapambana na mawaziri, wananchi huku wanatuuliza, hivi mbunge wetu yeye kazi yake ni kushughulika na mawaziri au...” amesema mjumbe huyo na kuongeza:

“Huu si wakati mzuri, tunakwenda kwenye uchaguzi, tusipokuwa makini tunaweza kupoteza mitaa, vijiji na vitongoji na mwisho jimbo litaondoka, hili sisi hatutakubali.”

Kiongozi mwingine wa CCM ngazi ya mkoa huo amesema, jimbo la Kisesa liliwahi kuongozwa na upinzani mara mbili, mwaka 1995 na 2000: “Sasa tusipokuwa makini wanaweza kulichukua tena. Ndiyo maana tunamwona huyu mbunge wetu kama anataka jimbo liondoke.”


Mvutano hauna afya

Mbali na makada hao wa CCM, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wamesema mvutano huo wa  Mpina na chama chake hauna afya, kama anavyoeleza Saidi Msonga.

Msonga, mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii, amesema kauli ya mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu inaonyesha uhusiano mbaya uliopo kati yake na  Mpina.

"Kauli hiyo inaweza kuwa haina ishara nzuri ya kihusiano kati yake na mwanachama wake, mpaka wanafikia hatua kama hiyo, inaonyesha wanaanza kuchokana. Na Mpina anaonekana (kwa viongozi wake) kama mtu ambaye ni mtata, mkorofi na hakubaliani na uongozi uliopo na kutokukubaliana na mwenyekiti wake.

“Sidhani kama (ukifika hapo)unaweza kunusurika kwenye taasisi yako na ni kauli (ya mwenyekiti) ambayo haina afya sana," amesema.

Msonga amesema katika mazingira kama hayo, ukifika wakati wa uchaguzi, basi Mpina anaweza kuwekwa kando.

“Hiyo siyo kwa CCM tu, hata kwa vyama vingine wangekuwa wamefukuzana zamani, mfano tulishuhudia Chadema ilimfukuza Zitto Kabwe, CUF waliwafukuza kina Hamad Rashid na wengineo, lakini kwa upande wa CCM kidogo kumekuwepo uvumilivu, labda kwa sababu chama kinaongoza nchi ndo maana wanafuata utaratibu," amesema.

Akichambua suala hilo, Bubelwa Kaiza amesema Mpina alileta hoja ya msingi ya uchunguzi wa kifo cha Hayati Magufuli, ambayo watu wamekuwa hawaisemi wanaiacha kimyakimya.

Mpina na mawaziri

Mpina, aliyeingia bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 2005 na amekuwa waziri chini ya Magufuli kwa takriban miaka mitatu (2017-2020), amekuwa kwenye mvutano na mawaziri mbalimbali.

Mbunge huyo ambaye wakati wake zilifanyika operesheni kadhaa za mazao ya uvuvi na mifugo, amewahi kuwashambulia mawaziri bungeni, akiwamo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Januari Makamba na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba.

Mawaziri wengine ambao wamekuwa wakivutana mara kadhaa bungeni ni Abdallah Ulega (Mifugo na Uvuvi) na George Simbachawene wa Ofisi ya Rais- Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Pindi Mpina anapoibua ama tuhuma au jambo bungeni juu ya mawaziri hao, nao humjibu kadiri alivyouliza na wakati mwingine mvutano huo huibua mjadala mkali mitandaoni.

Mathalan, Aprili 19, mwaka huu, Mpina alimtaka Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ajiuzulu kwa madai kuwa maagizo yake ambayo amekuwa akiyatoa huwa hayatekelezwi na kuwa nchi imefeli.

Akijibu kauli za Mpina bungeni, Simbachawene alimtaka aache kudharauliana.

Simbachawene alihoji kauli ya Mpina kuwa nchi imefeli, akisema inawezaje kutekeleza miradi mikubwa mingi ambayo kama nchi nyingine zikitekeleza zinafilisika.

Simbachawene alisema nchi inakusanya kodi kati ya Sh1 trilioni hadi Sh3 trilioni kwa mwezi.

“Nchi yetu inaheshimika, Rais wetu anaheshimika ndiyo maana kila mahali anapoenda duniani wanampa Shahada ya udaktari. Ni heshima, wanampa zawadi zote za kubeba wanaona hazifai hadi wanaamua kumpa zawadi ya kichwani,” alisema Simbachawene.

“Kule Meatu kwake tu (Mpina), Tarura (Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini) amepelekewa fedha lakini Sequip (Mradi wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari) amepelekewa shule mbili na Boost (Mradi wa Kuimarisha Ufundishaji na Ujifunzaji wa Shule za Awali na Msingi) amepelekewa madarasa chungu nzima,” alisema.

Mpina pia aliwahi kumvaa Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kutokana na alichokiita “hoja zake za uongo zilizosababisha kuongezeka kwa bei ya mbolea, huku akisingizia vita ya Ukraine wakati vita imeanza huku tayari mfuko wa mbolea unauzwa Sh130,000.