Kijana jela miaka 30 kwa kubaka mke wa mtu

Mshtikiwa, Sostenes Vakuka aliyevaa kodi la mkorea akitoka katika ukumbi wa Mahakama ya Wilaya ya Mufindi baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 Jela kwa kosa la ubakaji. Picha na Mary Sanyiwa

Mufindi. Mahakama ya Wilaya ya Mufindi imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela, Sostenes Vakuka baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kubaka.

Vakuka (32), mkazi wa kijiji cha Ihowanza, Kata ya Malangali ametiwa hatiani kwa kumbaka mwanamke mwenye miaka 20, ambaye ni mke wa mtu.

Hukumu hiyo imetolewa jana Desemba 6, 2023 na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Mufindi, Edward Uphoro.

Katika kesi hiyo,  ilidaiwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Februari 25, 2023 saa moja usiku katika Kijiji cha Ihowanza, kwamba akiwa nyumbani kwa mwanamke huyo alimuingilia kinguvu bila ridhaa yake, huku akimuuliza ni nani amemruhusu kuishi katika nyumba hiyo.

Siku ya tukio inaelezwa mume wa mwanamke huyo alikuwa amekwenda dukani kununua mahitaji.

"Mwanamke huyo akiwa anaendelea na shughuli zake, mshtakiwa alifika nyumbani hapo na kugonga hodi, alifungua mlango akidhani mume wake amerudi kutoka dukani, kumbe alikuwa mshtakiwa," ulidai upande wa mashtaka.

Inadaiwa baada ya mshtakiwa kuingia ndani na kufanya kitendo hicho, mwanamke huyo alipiga kelele kuomba msaada.

Upande wa mashtaka ulidai mumewe aliporejea alimkuta mshtakiwa akiendelea na kitendo hicho, hivyo alimkamata lakini katika purukushani alikimbia.

Wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi watatu na kielezo kimoja cha fomu namba tatu ya polisi (PF3).

Mshtakiwa alijitetea mwenyewe katika kesi hiyo na hakuwa na kielezo chochote.

Hakimu Uphoro amesema baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili, amejiridhisha upande wa mashtaka umethibitisha shtaka pasipo kuacha shaka.

Kutokana na ushahidi huo, Mahakama imemtia hatiani mshtakiwa kwa kosa la ubakaji ambalo ni kinyume cha kifungu 130 (1),(2),(a) na kumhukumu  kutumikia kifungo cha miaka 30 jela, chini ya kifungu 131(1) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu sura ya 16 rejeo la mwaka 2022.

Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Ahmad Magenda ameeleza hana kumbukumbu ya makosa ya jinai yaliyotendwa na mshtakiwa, hivyo kuomba Mahakama itoe adhabu kali, ili iwe fundisho kwake na watu wenye tabia kama hiyo.

Alipopewa nafasi ya kujitetea, mshtakiwa amesema hana cha kuiambia Mahakama kuhusu shtaka hilo kwa sababu halifahamu.