Hujafa hujaumbika, simulizi ya wavuvi walionusurika mdomoni mwa mamba Mtera

Mwandishi wa Mwananchi, Sharon Sauwa (kulia) akifanya mahojiano na Mkazi wa Kitonngoji cha Kenya, Yohana Mpangala ambaye alikabiliana na mamba kwa saa 5 kabla ya kuokolewa. Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

  • Kumekuwa na matukio ya watu kushambuliwa na mamba na viboko wakati wa uvuvi kwenye Bwawa la Mtera na Serikali imefuatilia na kubaini si wote wanastahili fidia kwa kuwa wameingia kwenye eneo lisilostahili.

Dodoma. Ndani ya chumba kilichojengwa kwa udongo na kuezekwa kwa majani, anaishi Yohana Mpangala.

Tunapofanya mazungumzo, nguo zake zimechafuka kwa udongo mwekundu.

Anapotembea anatumia gongo kwa kuwa sehemu ya mguu wake mmoja imekatika.


Ni nini kimempata?

Mpangala ni mmoja wa watu waliopata ulemavu kutokana na wanyamapori, mamba na kiboko waliopo kwenye Bwawa la Mtera ambalo mbali ya uvuvi, maji yake yanatumika kuzalishaji umeme.

Bwawa hili lipo katikati ya mikoa ya Dodoma ikiwa na kilomita za mraba 440 na Iringa yenye kilomita za mraba 220.

Akizungumza na Mwananchi Digital katika Kijiji cha Kenya, kilichopo Iringa Vijijini, Mpangala anasema alifika hapo akitokea wilayani Ludewa, mkoani Njombe mwaka 2017 kwa ajili ya shughuli za uvuvi.

Anasema siku ya tukio mwaka 2018, alitoka kwenda kuvua samaki kwenye bwawa hilo la Mtera.

Anaeleza akiwa kwenye mtumbwi saa nne asubuhi alikamatwa na mamba na walipambana hadi saa 10.00 jioni alipotoka bwawani.

Ni kwa vipi alipambana na mamba kwa zaidi ya saa tano? Mpangala anasema mnyama huyo alikuwa akimzamisha majini na kisha anamwachia hadi akapata fursa ya kupanda juu, hali iliyomfanya aweze kuvuta hewa.

“Alianza kunishika mkono akanizamisha kwenye maji, akanipandisha juu nikawa napiga kelele nikiendelea kujivuta kuelekea mwisho wa maji kwa saa zote kabla ya kupata msaada wa wavuvi wenzangu,” anasimulia.

Anasema hata walioenda kumwokoa walisimama pembezoni mwa bwawa kwa muda wakiogopa kuwa mamba angeweza kumuacha yeye na kuwavamia wao, lakini baada ya kuwa wengi waliamua kumsaidia.

Anaeleza ilipofika jioni baada ya kupambana na mamba kwa muda mrefu alichoka, hivyo akashindwa kupiga kelele, akanyoasha mkono kuomba msaada.

Mpangala anasema alitolewa bwawani akiwa hajitambui baada ya kupoteza damu nyingi baada ya mguu na mkono kuliwa na mamba.

Aishi kwa kusaidiwa

Anasema baada ya kutoka Hospitali ya Lugalawa alikokaa kwa zaidi ya miezi sita kutokana na vidonda kuchelewa kupona, alishindwa kuendelea na shughuli za uvuvi kwa kuwa alipata ulemavu.

Anasema pia alipata changamoto nyingine ya mkewe aliyezaa naye watoto sita kumkimbia baada ya kuona atashindwa kumhudumia.

“Maisha yangu ni magumu. Baadhi ya watoto wameondoka na mke wangu na wengine amewachukua dada yangu ndiye anawatunza. Unavyoniona hapa, nategemea mtu nyumba yake ikibomoka aniite nikakandike udongo, ninachokipata ndicho natumia kula na wakati mwingine wanakijiji wananisaidia,” anasema.

Anasema chumba anachoishi alipewa na watu kijijini hapo baada ya kukosa uwezo wa kupanga kama ilivyokuwa awali alipokuwa akijiingizia kipato kutokana na uvuvi.

Mpangala ambaye bado anasema hajapata kifuta machozi kutoka serikalini kutokana na kushambuliwa na mamba, anaomba msaada aweze kufungua biashara kwa kuwa hawezi tena kuvua.

Mwingine ajeruhiwa mkono

Mkazi mwingine wa Mtera, Henry Nyandoa aliyeanza uvuvi katika bwawa hilo mwaka 2019, anasema alishambuliwa na mamba Novemba 11, mwaka jana akiwa na wenzake wawili ndani ya mtumbwi.


Henry Nyandoa, mkazi wa Kijiji cha Mtera, mkoani Dodoma aliyenusurika kuliwa na mamba baada ya kuokolewa na wavuvi wenzake akizungumza na Mwandishi wa Mwananchi, Sharon Sauwa.  Picha na Merciful Munuo


“Tukiwa tunataka kuondoka, ghafla mamba alinirukia mkononi na kunivuta kwenye maji. Alikuwa mkubwa akawa anauingiza ndani ya mdomo wake kadri muda ulivyoenda,” anasema.

Nyandoa anasema wenzake walikuwa na ujasiri wakafanya jitihada za kumuokoa lakini mkono ulikuwa ndani ya mdomo wa mamba hadi kwenye mabega.

Anaeleza kuwa wenzake walimshika mkono wakajaribu kumvuta kutoka mdomoni mwa mamba lakini kutokana na ukubwa wa mnyama huyo ilishindikana.

Anaeleza baadaye kwa kutumia fimbo mwenzake alimpiga mamba kichwani.

“Alimpiga mara ya tatu kichwani akaniachia na hiyo ndiyo ilikuwa pona yangu. Nilikuwa naona damu zinatoka na mapigo ya moyo yanaenda kwa kasi,” anasimulia.

Anaeleza tukio hilo lilichukua dakika kama tano hadi alipookolewa lakini mamba alikuwa ameshamvunja mkono.

Nyandoa anasema alipelekwa Kituo cha Afya cha Mtera ilikobainika amevunjika mkono, hivyo akapelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kwa ajili ya matibabu zaidi.

Anasema alipatiwa matibabu kwa wiki mbili kabla ya kuruhusiwa kurejea nyumbani kwa masharti ya kurudi hospitali kwa uangalizi baada ya wiki sita.

Hata hivyo, kutokana na kukosa fedha za kugharimia matibabu, anasema alirudi mara mbili, akashindwa kurudi mara ya tatu kuangalia kama amepona.

“Nilipangiwa nirudi tena hospitali kuangaliwa lakini kutokana na hali mbaya ya kiuchumi nimefikia mwisho siwezi tena kugharimia matibabu,” anasema.

Baada ya kukosa fedha za kugharimia plasta ngumu (POP) mpya, wamemrudishia ya awali kwa kuishona na uzi.

Ameiomba Serikali na Watanzania kumsaidia apate matibabu ya mkono huo ili aweze kujitafutia mahitaji yake baada ya kusimama shughuli za uvuvi tangu Novemba 2023.

Amesema kwa sasa anategemea msaada wa wenzake ambao nao wanaelemewa, kwa malazi, chakula na mahitaji mengine.


Wajihami kwa mawe

Katika kila mtumbwi utakaoukuta kwenye bwawa hilo kunakuwa na mawe madogo zaidi ya matatu ambayo wavuvi wanasema huyatumia kupambana na mamba.

Mkazi wa Kitongoji cha Chamdumbwi A, wilayani Mpwapwa, mkoani Dodoma, Joseph Ngayoo anasema kiboko akishavuta harufu ya binadamu huibuka, hivyo unaweza kumkwepa tofauti na mamba.

“Lakini mamba anavizia, unaweza umsimjue kwa sababu kichwani yuko kama jiwe, kwa hiyo wanatusumbua zaidi kuliko viboko,” anasema.

Ameiomba Serikali kuwavuna mamba hao ili maisha ya wavuvi yawe salama.

Oscar Lukui, maarufu Kambona anasema wanapomuona mamba humtupia jiwe ili kumfanya aogope na kuondoka.

“Tunategemea msaada wa Serikali maana ukiviua viumbe hivi wanakushtaki, hivyo inabidi kuwaambia ili waje wawadhibiti wenyewe,” anasema Lukui, anayevua kwa kipindi cha miaka sita sasa kwenye bwawa hilo.

Anna Rogers, mkazi wa eneo hilo anasema wakazi wa kitongoji hicho wanategemea maji ya bwawa hilo kwa matumizi ya nyumbani lakini kutokana na uwepo wa mamba wamekuwa wanahofia kwenda kuyachota.

Anasema hivi sasa hawatumi watoto kuchota maji bwawani kwa hofu ya kuliwa na mamba.

“Hata sisi tunapoenda tunatupa mawe bwawani ili mamba kama yupo tumuone na akimbie. Tunaiomba Serikali itusaidie mradi wa maji ya bomba ufike kwenye kitongoji chetu ili tuepuke changamoto ya kuchota maji bwawani,” anasema.

Anaeleza kuwa mwaka jana walizika watoto wawili waliouawa na mamba walipoenda kuchota maji kwenye bwawa hilo.

Mkazi wa Kijiji cha Migoli, wilayani Iringa, Humphery Njooka anasema kutokana na changamoto za wanyama hao, wameingia hofu ya usalama wao wawapo katika shughuli za uvuvi.

Amesema watu takribani wanne wamepata ulemavu kwa kushambuliwa ama mamba au viboko.


Walilia kifuta machozi

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kenya, katika Kijiji cha Migori, Mariam Njowoka anasema kitongojini hapo wamekufa watu wanane kwa kuliwa na mamba na viboko na waliojeruhiwa ni sita.

Anasema wavuvi wengi wanaojeruhiwa au kuuawa na wanyama hao hawalipwi kifuta machozi, akibainisha kwenye kijiji chake wapo watu zaidi ya watano hawajalipwa.

“Mwanangu alipigwa na kiboko mwaka 2018, nimekaa naye zaidi ya miezi minne hospitali lakini hadi leo ni kimya sijapata kifuta machozi,” anasema.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mtera, mkoani Dodoma, Simon Lukui anasema mamba ni tishio, akieleza mwaka 2023 watu wawili walipoteza maisha na wengine wawili walijeruhiwa kijijini hapo.

“Mmoja hivi karibuni katika harakati za kurusha kasia, mamba alimdaka mkono wakakurupushana, bahati nzuri wenzake walikuwa karibu hivyo walimuokoa lakini amepata ulemavu wa mkono kutokana na majeraha yaliyosababishwa na mamba,” anasema.

Mamba pia wameua mifugo wakiwamo ng’ombe, mbuzi na nguruwe wanapoenda kunywa maji katika bwawa hilo.


Serikali yazungumza

Ofisa wanyamapori katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Charles Mdendemi anakiri bwawa hilo lina changamoto ya mamba na viboko.


Ofisa Wanyamapori katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa mkoani Iringa, Charles Mdendemi akizungumza wakati akifanya mahojiano na Mwananchi kuhusu changamoto ya mamba na kiboko kwenye Bwawa la Mtera. Picha na Merciful Munuo


Anasema mwaka 2014 hadi 2019, takwimu zinaonyesha watu 15 waliuawa na viboko, huku wawili wakijeruhiwa.

Mdendemi anasema walichukua hatua ya kumwandikia barua Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii mwaka 2016 na mwaka 2018 walikumbushia baada ya wananchi kulalamika kuwa wanyama hao wamekuwa wengi na hivyo wanawadhuru.

“Wizara ilisikia, mwaka 2020 waliwatuma Tawiri (Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania), utafiti ulivyofanyika ulikuja na matokeo mbalimbali ikiwemo bwawa hilo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 660 lilikuwa na uwezo wa kuhimili viboko 1,070 lakini waliokutwa ni 261,” anasema na kuongeza dhana kuwa viboko ni wengi haikuwa sahihi.

Hata hivyo, anasema Serikali ilichukua hatua kwa halmashauri kushirikiana na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa) kufanya doria ya kuwabaini viboko wakorofi.

Anasema katika awamu ya kwanza walibainika viboko wakorofi watano ambao waliuawa na baada ya miezi mitatu ilifanyika doria nyingine wakauawa wengine watatu.

“Doria hizi zimekuwa zikifanyika kila mwaka na ikitokea kiboko anaelekea kumdhuru mwananchi au amemdhuru basi anauawa,” anasema.

Anaeleza mwaka huu 2024, mtu mmoja aliuawa na mamba, hivyo ulinzi katika eneo hilo unaendelea kufanyika kwa kushirikiana na Tawa.

Amesema kutokana na idadi ya samaki kupungua kwenye bwawa hilo, wavuvi wamekuwa wakiwafuata kwenye kina kirefu cha maji ambako ndiko viboko hukaa.

Anaeleza changamoto pia husababishwa na baadhi ya wananchi kufanya shughuli za makazi, kilimo na ufugaji kando mwa bwawa hivyo wanyama hao kupita usiku kwenda kujitafutia chakula na kusababisha kuwadhuru watu.

Mdendemi anasema Serikali imetoa elimu kwa wananchi jinsi ya kujua tabia za wanyama hao, kuwakwepa, kuondoka kwenye maeneo hatarishi na kuwaeleza kuwa usiku si muda mzuri kuwa maeneo jirani na bwawa.

Anasema Serikali ikiendelea kuchukua hatua za kuwalinda dhidi ya wanyama hao, wananchi wanatakiwa kuchukua tahadhari kujiepusha na madhara.

Kuhusu kutolipwa kifuta machozi, anasema hilo linatokana na kanuni ya kifuta machozi ya mwaka 2011 kuwakataa.

Alitoa mfano wa watu wanaokataliwa na kanuni hiyo ni wanaoenda kufanya shughuli zisizo rasmi na wanaopata madhara chini ya kilomita tano ya eneo la hifadhi.

“Sehemu kubwa ya watu wanaoenda kuvua wakijeruhiwa hawatakiwi kulipwa kifuta machozi kwa sababu wamekumbwa ndani ya eneo la mnyama alipo. Tunaendelea kuwaelimisha juu ya kujilinda zaidi,” amesema.

Habari hii Imeandaliwa kwa kushirikiana na Bill & Mellinda Gates.