GGML yaahidi kuendeleza ushirikiano na Serikali kudhibiti Ukimwi

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (kulia) akimpatia cheti  Meneja Mwandamizi wa Afya, Usalama na Mazingira na wa GGML, Dk Kiva Mvungi kwa kutambua mchango wa kampuni hiyo katika Mfuko wa Udhamini wa Ukimwi (ATF) katika kuisaidia Serikali kuendeleza mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi. Ni katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani Morogoro Disemba mosi.

Morogoro. Meneja Mwandamizi wa Afya, Usalama na Mazingira wa Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML), Dk Kiva Mvungi amesema kampuni yake itaendelea kushirikiana na Serikali katika mapambano dhidi ya Ukwimwi ili kufikia malengo yaliyowekwa.

Dk Kiva ametoa kauli hiyo kutokana na Serikali kutambua mchango wa GGML katika jitihada za kukabiliana na Ukimwi na kuwapa cheti cha kuthamini mchango wao katika sherehe za Siku ya Ukimwi duniani kilichofanyika juzi mkoani Morogoro ambapo Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa alikuwa mgeni rasmi.

Amesema dhamira ya GGML ni kuendeleza jitihada za mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi na kila mwaka kupitia kampeni ya GGM Kili Challenge wamekuwa wakitoa mchango wao na mwaka huu wamechangia Sh100 milioni.

Kampeni hiyo ambayo iliasisiwa mwaka 2002, hushirikisha wapanda mlima Kilimanjaro kwa njia ya miguu na baiskeli kwa lengo la kuchangisha fedha za kutunisha mfuko wa mapambano ya Ukimwi (ATF), kuwezesha upatikanaji wa afua mbalimbali na kuwezesha taasisi binafsi zinazojihusisha na vita dhidi ya janga hilo.

“Kimsingi tunajivunia sana hii kampeni kwa kuwa hadi sasa imesaidia miradi zaidi ya 100 nchini kote tangu kuanzishwa kwake mwaka 2002” amesema Dk Kiva.

Juzi, Desemba, 1, 2023 katika maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani yaliyofanyika viwanja vya shule ya sekondari ya Morogoro, mjini Morogoro, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwahakikisha wadau kwamba Serikali itaendelea kuunga mkono jitihada wanazoonyesha katika kukabiliana na janga la VVU/ Ukimwi nchini.

Pia, aliipongeza Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) na wadau wengine kwa kuiunga mkono Serikali kwa mchango wa namna mbalimbali ili kuendeleza mapambano ya kutokomeza virusi vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi.

 “Nitambue mchango wa sekta binafsi na taasisi mbalimbali na wadau wa maendeleo ndani na nje ya nchi katika mapambano dhidi ya Ukimwi na hakika mafanikio haya tuliyoyatamka hapa yanatokana na ushiriki wenu ninyi wadau. 

“Hivyo natoa shukrani nyingi za dhati sana kwenu kwani nyie wadau muhimu kwa maendeleo ya vita hii naamini tukiendelea kuungana pamoja na Serikali yetu tutafikia malengo yetu, vilevile niwahakikishie kwamba Serikali yenu itaendelea kuunga mkono jitihada hizi za kutokomeza VVU/ Ukimwi hapa nchini,” alisema Majaliwa 

 “Niupongeze na kuushukuru Mgodi wa Geita Gold Mining Limite (GGML) kwa jitihada zake, tunashukuru sana kwa kuunga mkono kwenye ufadhili wa afua za VVU/ Ukimwi hapa Tanzania,” alisema Majaliwa 

Kutokana na jitihada hizo katika maadhimisho hayo, Majaliwa alitunuku cheti GGML kutokana ufadhili wake kwenye Mfuko wa Udhamini wa Ukimwi (ATF) ambacho kilipokelewa na Dk Kiva.

Awali, Majaliwa alizindua ripoti ya utafiti wa viashiria vya Ukimwi ambayo inaonesha maambukizi mapya miongoni mwa watu wazima wenye umri zaidi ya miaka 15 yanaendelea kupungua. 

“Maambukizi mapya miongoni mwa watu wazima wenye zaidi ya miaka 15 yanaendelea kupungua kutoka watu 72,000 waliokuwepo mwaka 2016/2017 hadi watu 60,000 kwa mwaka 2022/2023. Hii ni sawa upungufu wa asilimia 0.18 ambapo asilimia 0.24 ni wanawake na asilimia 0.11 ni wanaume,” alisema. 

Amesema Serikali iliamua kufanya utafiti kwa lengo la kujua hali ya sasa ya VVU na Ukimwi ilivyo hapa nchini na matokeo yameonesha kuwa Tanzania imepata mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya Ukimwi.