Dreamliner ATCL yafumuliwa injini Malaysia

Muktasari:

Ndege ya Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL), Boeing Dreamliner ipo kwenye matengenezo makubwa ya lazima katika mji wa Kuala Lumpur, nchini Malaysia, Mwananchi limebaini.


Dar es Salaam. Ndege ya Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL), Boeing Dreamliner ipo kwenye matengenezo makubwa ya lazima katika mji wa Kuala Lumpur, nchini Malaysia, Mwananchi limebaini.

ATCL imekiri kuwa ndege hiyo yenye namba za usajili 5H-TCJ ipo kwenye matengenezo hayo tangu Novemba 2023 na inatarajiwa kukamilika Juni, 2024.

Hii ni ndege ya pili ya Tanzania kupelekwa nje kwa ajili ya matengenezo makubwa, baada ya Bombardier Q300, iliyopo katika Kisiwa cha Malta tangu Novemba 15, 2020.

Kwa mujibu wa ukurasa wa Instagram wa @malaysianwings2.0, Boeing 787-8 Dreamliner ya ATCL yenye miaka minne tangu ilipotengenezwa, imeshushwa injini zake kwa ajili ya kufanyiwa matengenezo.

Alipoulizwa kupitia mtandao wa WhatsApp jana, Mtendaji Mkuu wa ATCL, Ladslaus Matindi alisema, “ndege hiyo yenye namba za usajili 5H-TCJ ilikwenda Malaysia kwa matengenezo ya lazima Novemba mwaka jana na ndiyo maana inaonekana haina injini zote mbili.

“Kutokana na wingi wa injini zinazohitaji matengenezo ya lazima na uchache wa injini za kukodi, ndege hulazimika kusubiri zamu ya matengenezo ya injini zake kufika na kumalizika. Matengenezo ya injini hizi yanatarajiwa kukamilika mapema mwezi ujao na kurudi nchini,” alisema.

Tatizo la injini za Rolls Royce

Akizungumzia sababu ya ndege hizo ‘mpya’ kupelekwa kwenye matengenezo ya lazima, Matindi alisema injini za Rolls Royce, zinazotumiwa na ndege za aina hiyo, zina tatizo la usanifu (design).

“Injini za Rolls Royce, zina tatizo la usanifu (design),” ameandika Matindi na kumtaka mwandishi kufuatilia zaidi kupitia mtandao wa Google.

Kwa mujibu wa mtandao wa Aviation Nuggets, waendeshaji kadhaa wa Dreamliner wameripoti kutokea kwa uchovu unaohusiana na kutu kwenye injini za Trent 1000 Package C, hitilafu ambazo zinaweza kusababisha hitilafu ya injini.

Suala hilo limesababisha kuongezeka kwa viwango vya ukaguzi (kupunguza muda wa ukaguzi kutoka safari 200 hadi 80), hali ambayo huongeza gharama za matengenezo na kupunguza upatikanaji wa ndege.

Kasoro hizo zinaweza kusababisha injini kushindwa kufanya kazi, mtandao huo umesema.

Mtandao huo unasema kampuni ya Boeing iliripoti kwa FAA (Idara ya Anga ya Marekani) kuwa mtengenezaji wa injini hizo hivi karibuni aligundua hitilafu kwenye hali ya mtiririko wa hewa katika injini wakati wa uendeshaji.

Kulingana na mtandao wa Aviation Nuggets, Wakala wa Usalama wa Anga wa Umoja wa Ulaya (EASA) ulitoa agizo la kufanyika kwa ukaguzi kwenye injini za Trent 1000-A, Trent 1000-AE, Trent 1000-C, Trent 1000-CE, Trent 1000-D, Trent 1000-E, Trent 1000-G, na Trent 1000-H.

Kwa mujibu wa mtandao huo, FAA ya Marekani imepunguza ndege aina ya Dreamliners Model 787-8 na 787-9, zilizothibitishwa kutumia injini za Rolls-Royce plc (RR).

Katika taarifa yake, Rolls Royce imesema, “Sehemu ya ukaguzi na majaribio yetu ya mara kwa mara ya injini hizo, tumeamua kufanya ukaguzi wa ziada wa injini hizo kuliko ilivyopangwa awali.

“Kupunguzwa kwa kasi ya ukaguzi kunatokana na ufahamu wetu zaidi wa uimara wa compresa ya ‘Trent 1000 Package C’, hali ambayo tulionyesha mwanzoni mwa mwaka huu.”

Taarifa hiyo imesema ukaguzi huo utasaidiwa na miongozo ya usimamizi wa huduma na uendeshaji wa ndege kwa mashirika ya ndege, itakayotolewa na mamlaka ya uhalali. Kwa bahati mbaya, hii itasababisha usumbufu zaidi kwa wateja wetu.

“Kuna injini 380 za ‘Package C’ zilizopo kwa mashirika ya ndege, hata hivyo, kasoro hiyo haipo kwenye injini za Trent 1000 Package B au injini za Trent 1000 TEN,” umesema mtandao huo.

Bombardier kurejea Juni

Kwa upande wa ndege ndogo ya Bombardier Q300 DHC Dash 8 iliyoko nchini Malta, Matindi amesema tayari matengenezo yake yamemalizika na inasubiri majaribio ya kuruka na ubadilishaji wa mfumo wa matairi (landing gears) ili irudi nchini mwezi ujao.

Ndege hiyo iliyosajiliwa kwa namba 5H-MWF, ilipelekwa nchini humo tangu Novemba 15, 2020.

Desemba 31, mwaka jana, gazeti hili liliripoti kuwa Bombardier Q300 DHC-8 Dash 8 ilikuwa inaelekea kutimiza miaka minne tangu ilipopelekwa Malta baada ya kupata hitilafu na ilikuwa haijajulikana matengenezo yake yatakamilika lini.

Wakati huo, Matindi alisema matengenezo ya ndege hiyo yangechukua muda mrefu kwa kuwa hiyo ni ndege ya zamani.

“Hiyo ni ndege ya zamani ndiyo maana imekaa muda mrefu, kwa sababu wanatakiwa watafute spare parts (vipuri), kwa hiyo itachukua muda mrefu.

“Hiyo ni Dash 8- Q 300, imekuja miaka 2000 huko, kwa hiyo haihusiani na ndege hizi zilizonunuliwa hivi karibuni. Ni ya zamani sana,” alisema Matindi.