Bosi mpya Udart atambulishwa rasmi

New Content Item (1)

Dar es Salaam. Siku chache tangu Mwananchi Digital iandike kuhusu kuwapo kwa mabadiliko ya uongozi katika kampuni ya Uendeshaji Usafiri wa Haraka (Udart), hatimaye bosi huyo ametambulishwa rasmi leo Jumanne Oktoba 24, 2023.

Si mwingine, ni Giliard Ngewe aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri ardhini (Latra).

Utambulisho huo umetolewa katika ziara ya Waziri wa Tamisemi, Mohammed Mchengerwa katika ofisi za Udart ambao ndio wasimamizi wakuu wa mradi wa mabasi ya ‘mwendokasi’ huku akiwapa tahadhari kuwa hatasita kuchukua hatua kwa watendaji wazembe katika usimamizi wa mradi huo.

Ngewe mbali ya kujitambulisha mwenyewe katika utambulisho wa watumishi waliokuwepo katika ukumbi wakati Waziri akipewa taarifa ya mradi huo kabla yakuutembelea mradi, pia alitambulishwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), Dk Edwin Mhede.

Ngewe anatambulishwa rasmi zikiwa zimepita siku 12 tangu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, aipe siku 12 Kampuni ya Udart, kutengeneza mabasi 70 yaliyoharibika ili kupunguza adha ya usafiri kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.

Oktoba 12, Chalamila alifanya ziara katika kituo cha kupanda mabasi hayo cha Kimara na Mbezi, ikiwa ni siku moja baada ya Mwananachi Digital iripoti changamoto wanazopitia abiria katika kupata huduma ya usafiri huo hasa muda wa asubuhi.

Kabla Ngewe hajapewa mikoba hiyo, Mkurugenzi wa Udart alikuwa John Nguya ambaye aliondolewa kimyakimya.