Benki Kuu bado yajivuta matumizi ya sarafu mtandaoni

Muktasari:

  • Wachumi washauri BoT itoe muongozo na elimu ya kutosha kwa sababu wimbi la watumiaji wa sarafu mtandaoni (cryptocurrency) ni kubwa.

Dar es Salaam. Wakati Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ikisema inaendelea na uchunguzi kuhusu matumizi ya sarafu mtandao nchini, wachumi wameishauri kutoa mwongozo haraka, kwani kasi ya utumiaji bado ni kubwa.

BoT imesema hayo kupitia ripoti inayoitwa ‘Mifumo ya ulipaji fedha’ iliyochapishwa katika tovuti yake Februari 5, 2024

“Mfumo wa malipo wa Tanzania unaathiriwa na maendeleo ya ndani na kimataifa katika teknolojia zinazoibuka, zikiwemo sarafu za kidijitali (sarafu mtandao). Benki Kuu ya Tanzania imekuwa ikitafiti na kuchunguza uwezekano wa utoaji wa sarafu mtandao yake (CBDC).

Loading...

Loading...

“Benki bado inachunguza vipengele vya kiutendaji vya CBDC kwa kuwashirikisha wadau wake kama vile benki, mashirika ya kimataifa na kikanda,” imesema sehemu ya ripoti hiyo.

Kauli hiyo ya BoT imekuja ikiwa ni inakaribia miaka mitatu tangu Rais Samia Suluhu Hassan alipoiagiza ifanye maandalizi ya uwezekano wa kuruhusu sarafu za kidijitali, Juni 13, 2021.

Rais Samia aliielekeza BoT kuanza maandalizi muhimu ili isije kushtukizwa na mabadiliko ya dunia, wakati sekta ya benki ikichukua mwelekeo mpya na sarafu hizo za kidijitali zikionyesha dalili za kuchukua nafasi muhimu katika masuala ya fedha.

"Tumeshuhudia kuibuka kwa sarafu mpya kwa kutumia intaneti," alisema Rais Samia.

"Ukanda wote huu, ikiwemo Tanzania, hawajakubali au kuanza kutumia njia hizi. Wito wangu kwa Benki Kuu ni kwamba, muanze kufanyia kazi maendeleo haya. BoT inatakiwa kuwa tayari kwa mabadiliko na si kukutwa haijajiandaa,” alisema.

Mwongozo na elimu

Hali ikiwa hivyo, mtaalamu wa uchumi wa kidijitali, Oscar Mkude amesema kuna haja wakati BoT ikiendelea na uchunguzi kuhusu matumizi rasmi ya sarafu za kidijitali, itoe muongozo na elimu ya kutosha kwa sababu kuna wimbi la watumiaji wa fedha hizo.

“BoT wajitokeze watoe maelekezo kuhusu hali iliyopo, kwa sababu wakati wanaendelea na uchunguzi bado sarafu mtandao inaendelea kutumika kwa kiwango kikubwa na kutokana na asili yake, bado ni hatari kutumika kwa sababu thamani yake haitabiriki,” ameshauri Mkude.

Amesema ni muhimu fedha hiyo kwa minajili ya kuidhibiti, ikatengenezewa sheria au sera ambayo itatumika kukabiliana na matatizo yoyote yanayojitokeza kutokana na utumiaji wake.

Kauli ya Mkude inaungwa mkono na Profesa Abel Kinyondo, mchumi mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), anayeshauri BoT itoe ufafanuzi na elimu ya kutosha kuhusu fedha hizo wakati ikiendelea na uchunguzi.

“BoT inatakiwa itoe elimu na maelezo ya kutosha na si kila wakati kusema wanafanya utafiti, inabidi watoe elimu ya kutosha ili watu waingie wakiwa na taarifa za kutosha,” ameshauri Profesa Kinyondo.

Amesema kuna haja ya BoT kuzifafanua hatari zilizopo katika sarafu mtandao, kwa sababu hata utafiti wanaoufanya matokeo yake watu wanaweza wakawa tayari wanayafahamu.


BoT yafafanua
Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba amesema elimu kuhusu hatari ya matumizi ya sarafu mtandao wanaendelea kuitoa lakini kinacholeta kigugumizi cha kuruhusu matumizi ya sarafu hizo ni namna ya kuzisimamia.

“Elimu tunaendelea kutoa lakini bado ukizitumia fedha hizi unapopata changamoto hakuna taasisi ambayo itawajibika kwa sababu hakuna anayezisimamia. Sasa hivi watu wengi wanalizwa mtandaoni kwa sababu kuna matapeli katika mifumo ambao wanatoa fedha mtandao feki,” amesema Tutuba.

Amesema changamoto katika sarafu mtandao si Tanzania pekee bali duniani kote, kwani magavana wote wametoa nafasi ya kuendelea uchunguzi wa teknolojia hiyo.

“Mwezi wa sita (Juni) tulikuwa Uswisi katika mkutano wa magavana wote duniani, kuliibuka dhana tofauti kuhusu sarafu mtandao kwa sababu kuna ambao walitoa wasilisho wakasema ichukuliwe kama mtaji, wengine wakasema ichukuliwe kama fedha na wengine walisema kama Tehama, swali la msingi lilibaki je, tunazisimamiaje?” amesema.


Kuikubali au kuikataa?

Kuhusu utayari wa Tanzania kuingia katika matumizi ya sarafu za kidijitali, Profesa Kinyondo anaonyesha wasiwasi wa kuathirika kiuchumi, lakini akieleza kuwa endapo dunia itaenda huko, (Tanzania) hatuna budi kuitumia.

“Uamuzi huo utategemea ka tunachokitaka, unadhani tunahitaji kuwa nayo (sarafu ya kidijitali)? sihisi hivyo, lakini utambue kwamba sisi si kisiwa lazima pia uangalie na dunia inavyoenda.

“Isije huko baadaye dunia ikakumbatia sarafu mtandao sisi bado tukawa nyuma, lakini bado kabla hatujaingia huko tutambue uwapo wa hatari kubwa katika matumizi hayo ndiyo maana watu wengi duniani bado wanajifunza,” amesema Profesa Kinyondo ambaye amewahi kuwa mkurugenzi wa mipango na utafiti katika Taasisi ya Utafiti ya Repoa.

Amesema wasiwasi wake katika sarafu mtandao ni mkanganyiko kuhusu kupanda na kushuka kwa thamani yake, jambo alilosema linaweza kuwa na athari chanya kwa nchi zinazoendelea.

Lakini Mkude yeye amesema suala la sarafu hizo kutoweza kudhibitika, linaleta shaka katika uchumi wa nchi, hivyo BoT inahitaji kuwa makini zaidi.

“Nchi nyingi bado zinajiuliza maswali kwa sababu sifa mojawapo ya fedha, ziwe inatambulika duniani, ziwe inaweza kubadilishwa na ziweze kudhibitiwa, lakini sarafu mtandao inakosa sifa hizo,” amesema Mkude.

Uwepo mdahalo

Ili kufikia suluhisho sahihi, Mchumi Mack Patrick amesema kuna haja ya kuwa na mdahalo wa wazi kwa wadau wa fedha ili kuona umuhimu na matumizi ya cryptocurrency.

“Tunahitaji mjadala wa pamoja wa kina kuhusu jambo hili kwa sababu bado ni hatari katika mazingira ya nchi zinazoendelea kama Tanzania kutokana na kupanda na kushuka kwake thamani.

“Ni wakati wa BoT kutoa msimamo wa moja kwa moja mbali na kuendelea na utafiti kwa muda mrefu huku bado miongoni mwa watumiaji wakilalamika, huku wengine pengine wakifaidika,” amesema Patrick.

Mtumiaji wa sarafu mtandao, Hilda Mbukina amesema tatizo lilipo kwa Watanzania ni kukosa elimu sahihi lakini bado kuna nafasi ya kujifunza zaidi kuhusu teknolojia hiyo.

“Bado Tanzania tupo nyuma katika matumizi ya sarafu mtandao na hatuna elimu ya kutosha, ndiyo maana muda mwingine tunaambizana vitu visivyo vya kweli na vinavyotia hofu kuhusu teknolojia hii ambayo wenzetu wananufaika nayo,” amesema Hilda.

Amesema kuna haja Serikali kutoa msimamo kuhusu suala hilo ambalo anadai ni kimbilio la ajira kwa vijana wengi.

“Sasa hivi vijana wengi waliohitimu wanakosa ajira lakini wanakuja huku mtaani wanafanya cryptocurrency (miongoni mwa aina ya sarafu mtandao) na wengine wanafanikiwa kabisa,” amesema Hilda.

Kauli ya Hilda kuhusu ajira, inashabihiana na ripoti ya ‘Tanzania in figures 2022’ iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) iliyosema ajira nyingi zipo katika sekta zisizo rasmi.


Takwimu sarafu mtandao

Kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia, hadi Septemba 10, 2023, thamani ya sarafu za kidijitali (Bitcoin, Litecoin, Monero, Ethereum, na fedha nyinginezo za mtandaoni) ni takriban Dola za Marekani 1.04 trilioni.

Pia makadirio kulingana na tovuti ya Triple-A inayofanya utafiti kuhusu uchumi wa kidijitali yanaonyesha kufikia mwaka 2023, viwango vya umiliki wa fedha mtandao duniani viliongezeka kwa asilimia 4.2 na idadi ya watumiaji walikuwa milioni 420 duniani.