IMELIPIWA-Ubungo: Halmashauri kinara katika uwezeshaji wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu
Muktasari:
Walikuwa ni miongoni mwa vijana waliokuwa na hamasa kubwa ya kujiajiri ili kujipatia kipato cha kuendesha familia zao pamoja na kutoa ajira kwa vijana wenzao.
Walikuwa ni miongoni mwa vijana waliokuwa na hamasa kubwa ya kujiajiri ili kujipatia kipato cha kuendesha familia zao pamoja na kutoa ajira kwa vijana wenzao.
Hata hivyo, changamoto ilikuwa jinsi ya kukuza mtaji wao ili kuanzisha kiwanda kidogo cha kutengeneza mapambo ya ndani kwa kutumia unga wa Gypsum.
Willson John Katibu wa Kikundi cha Umoja ni Nguvu Hondogo-Delini Kata ya Kibamba anakiri wao ni wanufaika wakubwa wa mikopo inayotolewa na Manispaa ya Ubungo.
Mikopo hiyo inatolewa chini ya kifungu cha 37A cha Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, sura 290 na kanuni za utoaji na usimamizi wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu za mwaka 2019.
Kupata mikopo hiyo inahitajika wanawake na vijana waunde kikundi cha watu wasiopungua watano huku watu wenye ulemavu wakitakiwa kuwa wanakikundi wasiopungua wawili.
Kikundi hicho kinatakiwa kiwe kimesajiliwa, kina akaunti ya benki yenye jina la kikundi na kijishughulishe na ujasiriamali au kiwe na kusudi la kuanzisha shughuli za ujasiriamali mdogo au wa kati.
John anasema Kikundi cha Umoja ni Nguvu kilianza mwaka 2020 kwa kuanzisha kiwanda kidogo cha kutengeneza mapambo ya ndani kwa kutumia unga wa Gypsum.
Anasema kikundi kilianza na vijana 10 na sasa kina vijana wanane ambapo wa wanaume ni sita na wanawake wawii wanaoendelea na mradi. Kikundi kilisajiliwa rasmi na Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo mwaka 2020 kwa cheti namba UMC/ VK/5174/2020.
Kikundi hicho kilianza shughuli zake na mtaji wa Sh3.45 milioni ikiwa ni michango ya wanachama (kiingilio na ada) na msaada kutoka kwa wadau wa maendeleo. Fedha hizo zilitumika kujenga banda dogo la kufanyia kazi, kununua mashine tano za mikanda, vitendea kazi vingine na gharama za uendeshaji. Mwaka 2021 walifanikiwa kupata mkopo wa Sh37.5 milioni kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.
“Februari 2021/2022 kikundi kilikidhi vigezo baada ya kutuma maombi ya mkopo Halmashauri na hivyo kufanikiwa kukopeshwa Sh37.5 milioni. Mkopo huu una kipindi cha marejesho cha miaka mitatu,” anasema John.
Kuhusu urejeshaji wa fedha hizo anasema mwanzoni walitia mkazo kuhakikisha fedha hizo wanazirudisha ili kupata mkopo mwingine.
“Baada ya kipindi cha miezi 3 walianza kurejesha Mei 2022. Kufikia Julai 2022 kikundi kilikuwa kimesharejesha jumla ya Sh3.12 milioni ambayo ni sawa na Sh 1.04 milioni kwa kila mwezi,” anasema John.
Anasema fedha walizopewa zimewasaidia kutengeneza karakana bora zaidi ya lle ya awali, kuongeza mashine 39 za kutengeneza mapambo aina tofauti na zile 5 za mwanzo, kuongeza mtaji kwa kununua mifuko 400 ya Gypsum Powder na mifuko 10 ya nyuzi (Fibers) na kununua vifaa vingine muhimu vya kazi kama mapipa, meza na rola za kufungashia.
Takwimu za Wizara ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) zilizotolewa na Waziri Ummy Mwalimu wakati akiwasilisha bajeti yake ya 2021/22 bungeni zilionyesha kuwa Serikali imetenga Sh64.5 bilioni kwa ajili ya mikopo kwa vikundi 18,244 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Kati ya fedha hizo, Sh25.8 bilioni zilitengwa kwa ajili ya vikundi 8,223 vya wanawake, Sh25.8 bilioni kwa ajili ya vikundi 6,966 vya vijana na Sh12.9 bilioni kwa ajili ya vikundi 3,055 vya watu wenye ulemavu.
Mikopo hiyo ni sehemu ya asilimia 10 ya mapato inayotengwa na kila Halmashauri ya Tanzania Bara kwa ajili ya vijana ambao hupata (asilimia nne), wanawake (asilimia nne) na watu wenye ulemavu (asilimia mbili).
John anasema mpaka sasa kikundi hicho kimefanikiwa kutengeneza ajira kwa vijana sita mbali ya wanakikundi, wawili kwa ajili ufungashaji na wanne kwa ajili ya kufyatua mikanda kwa lengo la kuongeza nguvu za uzalishaji kutokana na wanakikundi kuwa wachache.
Kimeongeza uzalishaji kutoka mikanda 900 kwa wiki hadi 5400 kwa wiki, kuongeza bidhaa mpya za maua, kona (Angle) na Stick na kimeweza kulipa kodi ya shilingi laki sita (600,000) kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ndani ya kipindi cha miezi mitano baada ya kupata mkopo.
John anasema matarajio yao kwa sasa ni kuwa na kiwanda kikubwa kitakachozalisha bidhaa bora za kutosha kuhudumia soko la ndani na la nje ya nchi, kukuza ajira na kuinua uchumi wa vijana kwa kuwapa ajira na elimu ya ufundi, kumiliki eneo binafsi la kikundi badala ya eneo la sasa la kukodi, kurudisha mkopo kwa wakati ikiwezekana kabla ya muda wa miaka 3 ili wengine nao wapate na kuanzisha uzalishaji wa gypsum board.
“Tunamshuru Mungu kwa kutupa maono ya kuanzisha kiwanda hiki. Aidha tunashukuru Serikali ya awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Manispaa ya Ubungo kwa kutenga bajeti hizi za kuwezesha vijana,” anahitimisha John.
Wakati wa maadhimisho ya wiki ya vijana duniani mwaka huu, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye ulemavu, Patrobas Katambi alitembelea baadhi ya vikundi vya vijana vya Manispaa ya Ubungo ambavyo vimenufaika na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu na kueleza kuwa dhima ya Serikali ni kuona vijana wanajiajiri kwenye shughuli za uzalishaji wakisaidiwa na Halmashauri kwa kuongezewa mikopo isiyo na riba kama sheria inavyoelekeza.
Kwenye ziara hiyo NaibuWaziri Katambi alitembelea kikundi cha Umoja ni Nguvu kinachojihusisha na utengenezaji wa mapambo ya ndani kwa kutumia unga wa gypsum na kikundi cha Briaco kinachojishughulisha na uzalishaji wa Kripsi za viazi mbatata na kuwataka vijana kuwa na malengo, kusudio na shabaha katika mipango kazi yao ili waweze kuzalisha bidhaa zenye ushindani kwenye soko la ndani na nje.
Mweka Hazina wa kikundi cha watu wenye ulemavu cha Kibamba (Kibamba Disable Group), Stella Kalinga anasema kikundi hicho kilichoanza mwaka 2021 kilikuwa na wanachama wanne ambapo baadaye mmoja alijitoa na sasa wamebaki watatu.
Anasema kikundi hicho kinajihusisha na mradi wa usafirishaji abiria kwa kutumia bajaji ambao ulitokana na mkopo waliyopata mwaka uliopita kutoka Halmashauri ya Ubungo.
“Baada ya kuunda kikundi chetu na kukisajili, tulienda Manispaa na Mungu akasaidia tukapata mkopo wa Sh8.5 milioni ambao tulikubaliana tuanzishe biashara ya bajaji. Tulitumia kiasi cha Sh7.3 milioni kwa ajili ya kununulia bajaji na pesa kidogo iliyobaki tulitumia kugharamia mahitaji mengine ili chombo hicho kiweze kufanya kazi,”anasema Stella.
Anasema bajaji hiyo wamemkabidhi mtu kwa ajili ya kufanya nayo biashara ambapo anawaletea fedha inayowasaidia kurejesha mkopo huo pamoja na kukidhi mahitaji ya familia zao.
“Mpaka sasa tumefanikiwa kurejesha Sh 7.1 milioni na kiasi kilichobaki tunatarajia kumalizia mwezi huu. Marejesho haya yametokana na fedha tunayoipata kutoka kwenye bajaji hiyo ambayo kiukweli imetusaidia kukidhi baadhi ya mahitaji yetu,” anasema Stella.
Anasema wakifanikiwa kumaliza mkopo huu wanatarajia kuchukua mwingine ambao utawawezesha kila mtu kwenye kikundi hicho kuwa na bajaji yake.
Mwenyekiti wa kikundi cha kina mama cha Newton kilichopo Kimara Kilungule, Albina John anasema kikundi hicho kilianza mwaka 2019 kikiwa na wanachama 25 lakini sasa wapo 12 kutokana na wengine kushindwa kufuata matakwa ya mkataba waliowekeana.
Albina anasema kikundi hicho kinajihusisha na shughuli mbalimbali ikiwemo; kutenegeneza chaki, batiki, kufungasha asali mbichi, kusindika pilipili, kutenegeza siagi ya karanga, kutengeneza sabuni za maji na kutengeneza jiki.
“Ili kupanua mtaji wa kikundi chetu Machi, 2021 tulipeleka maombi ya mkopo Halmashauri ya Ubungo na kwa bahati nzuri tulifanikiwa ambapo halmashauri hiyo ilitupatia kiasi cha Sh50 milioni fedha ambayo imetusaidia kwa kiasi kikubwa kukuza biashara yetu kwa kununua vitendea kazi ikiwemo mashine mpya na kupata eneo la kudumu kwa ajili ya biashara,” anasema Albina.
“Kabla ya kupata mkopo huo tulikuwa na mashine moja tu ya kuzalisha chaki ambayo ilikuwa na uwezo wa kuzalisha kilo 800 za chaki kwa siku lakini baada ya kupata mkopo huo tuliongeza mashine tatu na sasa tunazo nne,” anasema Albina.
Albina anasema lengo la kikundi cha Newton ni kutengeneza ajira kwa wakina mama wengine kwa sababu wanafahamu kwamba changamoto ya ajira ni kubwa.
Licha ya malalamiko ya baadhi ya wanawake na vijana kupewa kiasi kidogo cha fedha, Halmshauri ya Manispaa ya Ubungo imesema mikopo hiyo hutolewa kulingana na fedha uhitaji wa mradi ulioombewa baada ya upembuzi wa kina.
Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo imekuwa moja ya halmashauri vinara katika eneo hili ambapo kupitia mapato yake ya ndani imewawezesha wananchi katika makundi ya wanufaika kujikwamua kiuchumi pamoja na kuchangia juhudi za kukuza uchumi.
Halmashauri hiyo imekuwa ikitenga asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya mfuko wa kuwezesha vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kila mwaka.
Toka Halmashauri ilipoanza kutekeleza agizo la Serikali la kutoa mikopo ya asilimia 10 kupitia mfuko wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu mwaka 2017/2018, hadi kufikia April, 2021/2022 jumla ya Sh7.559 bilioni zimetolewa kwa vikundi 1350 vyenye wanufaika 10,163.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ubungo, Beatrice Dominic anasema kila mwananchi mwenye sifa ya kupata mikopo hiyo anakaribishwa kupeleka maombi bila kujali itikadi ya chama chake wala kabila.
“Serikali iliweka fedha hizi ili kuhakikisha mjasirimali anakuza kipato chake na Taifa kwa ujumla, hivyo kwa yeyote anayetaka kupata mkopo huo hana budi kuomba ili aweze kuongeza kipato cha familia,” anasema Mkurugenzi huyo.
Afisa Maendeleo wa Manispaa ya Ubungo anasema katika utoaji wa mikopo hiyo huzingatia zaidi andiko la mradi, uhalisia wa utekelezaji wake kutoka kwa wanakikundi.
Anasema wanazingatia sheria ya utoaji wa mikopo hiyo na si vinginevyo ikiwemo kuwapatia watu mikopo walio kwenye vikundi bila kujali itikadi zao za vyama.
Anasema mikopo ikitolewa, wana utaratibu wa kuwafuatilia wahusika kupitia maafisa wa maendeleo ya jamii katika kata ili kujua kama miradi iliyoombewa fedha ipo na inajiendesha.
“Hatua tunazochukua kwa vikundi ambavyo havijarejesha mikopo ni kuwafuatilia kujua changamoto na namna ya kukabiliana nazo ili waendeleze mradi na kufanya marejesho,” anasema Afisa Maendeleo huyo.
Hata hivyo, anasema mchakato wa kushughulikia changamoto mbalimbali ambazo zimejitokeza ikiwemo uchepushaji wa matumizi ya mikopo hiyo unafanyika.
Kuhusu utoaji wa elimu kwa vikundi hivyo Afisa Maendeleo anasema katika robo ya nne ya mwaka wa fedha 2021/2022, Idara ya Maendeleo ya Jamii ya Manispaa hiyo kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kabla ya kutoa mikopo hutoa elimu na mafunzo ya kuwajengea uwezo kwa vikundi vinavyoomba kupatiwa mikopo pamoja na vikundi vingine katika Kata na Mitaa ya Halmashauri.
“Mafunzo yanayotolewa yanalenga kuwajengea uwezo kwenye uongozi, tabia za fedha, uendeshaji wa miradi, usimamizi wa fedha, uwekaji wa akiba, utunzaji wa kumbukumbu, matumizi ya nembo za ubora, vifungashio na marejesho yaliyotolewa kwa vikundi 1350 vilivyopatiwa mikopo,” amesema.
Kwa sasa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo inasajili vikundi vinavyotegemea kupata mikopo kupitia mfumo wa mtandao ulioelekezwa na Serikali.
Ili kufanikisha usajili huo, vikundi vinapaswa kufika ofisi za Kata na kupata maelekezo ya usajili kwa Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Kata au kutembelea Youtube kwa kuandika Ubungo Manispaa namna ya kusajili vikundi mtandaoni.
Makala hii imelipiwa na Manispaa ya Ubungo. Mwananchi Communications Limited (MCL) haihusiki kwa namna yoyote na bidhaa ama huduma zinazotangazwa humo na haitawajibika kwa chochote kitakachojiri ukiamua kuzitumia.