IMELIPIWA: Kuhuisha biashara na mabadiliko ya tabianchi kwa ukuaji shindani katika uchumi wa kijani

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Philip Mpango akihutubia katika Warsha ya 25 ya Utafiti na Sera iliofanyika Dar es Salaam mwaka jana.

Muktasari:

Mpango wa Taifa wa sasa wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa 2021/22-2025/26 unaweka kipaumbele katika maendeleo ya biashara katika kutekeleza malengo ya maendeleo ya kati ya Tanzania kufikia ushindani wa viwanda na maendeleo endelevu ya binadamu.

Na REPOA

Mpango wa Taifa wa sasa wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa 2021/22-2025/26 unaweka kipaumbele katika maendeleo ya biashara katika kutekeleza malengo ya maendeleo ya kati ya Tanzania kufikia ushindani wa viwanda na maendeleo endelevu ya binadamu.

Mpango huo umeweka lengo la kiutendaji la kuongeza mauzo ya nje hadi kufikia asilimia 28 ya Pato la Taifa na sehemu ya mauzo ya nje katika masoko ya dunia kufikia asilimia 0.15.

Hata hivyo, utimilifu wa uwezo wa kibiashara wa Tanzania kwa sasa unachangiwa na wasiwasi juu ya mabadiliko ya hali ya hewa. Utafiti unaonyesha kuwa mabadiliko ya hali ya hewa huathiri biashara kwa kuvuruga minyororo ya ugavi na usambazaji na kuongeza gharama za biashara.

Athari za biashara kwenye mabadiliko ya tabianchi sio lazima ziwe hasi. Kiuhalisia, tafiti za hivi karibuni zimeonyesha kuwa biashara inaweza kujenga minyororo ya thamani ambayo husababisha matumizi bora ya rasilimali na ufikiaji wa teknolojia zinazotumia kiwango kidogo cha kaboni.

Hivyo, kunapokuwapo sera bora za mazingira, vikwazo vidogo (mathalani, kwa kuondoa ushuru na vikwazo visivyo vya ushuru kwa bidhaa na huduma ambazo ni rafiki kwa mabadiliko ya tabianchi), na taasisi zinazofanya kazi vizuri, biashara ya kimataifa inaweza kuwa nyenzo imara ya kukabiliana na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

Warsha ya 26 ya Utafiti na Sera

Katika kukabiliana na ongezeko la mahitaji ya uchumi wa mseto na biashara shindani, wakati ambapo taasisi mbalimbali za kimataifa zikiimarisha juhudi za kupunguza ongezeko la joto duniani na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Warsha ya 26 ya Utafiti na Sera (WUS) litaandaliwa kwa ushirikiano na Benki ya CRDB, Mtoa Huduma za Kifedha anayeongoza nchini Tanzania ambaye sasa yuko Tanzania na Burundi, Afrika Mashariki.

Mkurugenzi Mtendaji wa REPOA, Dk Donald Mmari akitoa neno la ukaribisho katika Warsha ya 25 ya Utafiti na Sera (WUS) iliofanyika Dar es Salaam mwaka jana.

Ushirikiano huu utatoa fursa kwa CRDB kwa kuchochea na kukuza mijadala ya kisera na utafiti wa mazingira husika juu ya uhusiano baina ya biashara na mabadiliko ya tabianchi, uwezeshaji fedha wa kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi, na nguvu yao ya pamoja katika kukuza ushindani na uchumi wa kijani.

• Kuangalia kwa karibu biashara na mabadiliko ya tabianchi kama vichocheo vya msingi vya kuonyesha faida linganishi za Tanzania;

• Minyororo ya thamani ya kimataifa na fursa za uhusiano wa kimkakati ili kuongeza ushindani katika kilimo, viwanda na sekta nyinginezo;

• Jinsi taasisi za fedha zinavyoweza kukuza uzalishaji, usambazaji na sera za baishara zinazozingatia mabadiliko ya tabianchi.

Wakati hili likiwa ndiyo WUS ya kwanza la kuangazia sera za kijamii na kiuchumi juu ya mwingiliano wa mabadiliko ya tabianchi katika uzalishaji, biashara, na uwezeshaji fedha unaozingatia mabadiliko ya tabianchi, ni kongamano la pili mfululizo linalochambua kwa karibu biashara kama moja ya vipaumbele vya kiutendaji vya Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa Tanzania wa 2021/22 – 2025/26, na wakati huo huo kuarifu utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (2021-2026) na Mchango wa Taifa wa Kutokomeza Gesi Chafuzi (2021), ikijumuisha mfano halisi wa mchango wa sekta binafsi na taasisi za fedha kwenye ajenda hii ya kitaifa.

WUS inatoa mapitio ya utekelezaji wake kwa wakati na kuwakumbusha wadau wote kutathmini mchango wao katika kufikia malengo ya mipango na mikakati hii ya kitaifa.

Lengo la Warsha

Pamoja na uwepo wa kauli mbiu ya WUS, mazungumzo yatajikita kuangazia vipengele muhimu vinavyotokana na mabadiliko ya tabianchi na biashara na uchumi wa kijani na shindani, ambayo yenyewe yanahitaji uangalizi maalum wa kisera.

Fursa za soko

Sera bunifu za biashara zinaweza kutoa majibu ya Tanzania na nchi nyingine zinazoendelea dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. Moja ya bunifu zilizofanywa hivi karibuni ni maendeleo ya uchumi wa kijani unaozingatia uendelevu wa mazingira, uchumi na jamii.

Kutokana na ufinyu wa fedha za pamoja kimataifa na kutotimizwa kwa mkataba wa Copenhagen kuhusu uwezeshaji fedha wa mabadiliko ya tabianchi (Ugawaji wa Dola za Marekani bilioni 100 kwa mwaka kwa nchi zinazoendelea), ubunifu katika sera zinazounga mkono biashara na fursa za soko unasalia kuwa mojawapo ya hatua za msingi ambazo Tanzania na nchi nyingine zinazoendelea zinaweza kuzitumia ili kugeuza changamoto kuwa matumaini na matarajio halisi.

Kuhuisha Uwekezaji

Ugumu wa kupata fedha za mabadiliko ya tabianchi umechangia matukio ya hali mbaya ya hewa kuongeza hatari kwa mamilioni ya watu kuishi maisha duni, kuhatarisha usalama wa chakula na maji, na sekta za uzalishaji na minyororo ya usambazaji.

Wakati ikionekana kuwepo kwa hitaji la kuimarisha upatikanaji na usimamizi wa wa fedha za kimataifa za mabadiliko ya tabianchi kwa Tanzania, mbinu ya kuhamasisha upatikanaji rasilimali fedha ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kutoka kwenye taasisi za fedha za ndani itakuwa ni suluhisho lenye tija na linalotazamiwa zaidi.

Fedha za ufadhili za kimataifa na mifuko ya ufadhili kama vile Mfuko wa Mazingira wa Dunia (MMD), Nchi Maskini Zaidi Duniani (NMD), na MKMT imeweka masharti magumu na ya kiufundi zaidi ambayo bila ya mwongozo maalum itakuwa vigumu kwa waombaji katika nchi zinazoendelea kupatiwa fedha hizo na pengine zisisaidie kutatua mahitaji ya ndani.

Benki ya CRDB, hata hivyo, imeweza kupata kibali kutoka kwa MKMT, na hivyo kufungua njia katika eneo la ufadhili wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi unaweza kuchangiwa na sekta binafsi.

Wakati ikionekana ni muhimu kwa jukumu kuu la Benki ya CRDB katika MKMT kufahamika kwa wadau mbalimbali wa maendeleo, jukumu la uongozi wa Benki pia linapaswa kupanuliwa na kuungwa mkono vyema kisera ili kuwezesha taasisi za fedha za ndani kutoa ufadhili unaonendana na shughuli husika hususan katika uzalishaji unaozingatia mabadiliko ya tabianchi na upanuzi wa kibiashara.

Kujengea utayari kwa taasisi

Kilimo, uchumi wa bluu, na mifugo vinachukua sehemu kubwa ya biashara ya ndani na nje katika Jumuiya za Kiuchumi za Kikanda (RECs).

Kubadilika kwa hali ya hewa kunaweza kulazimisha jumuiya hizo, hususan EAC kutathmini upya ardhi, bahari, na maliasili zake nyingine na kutumia mifumo kwa nia ya kubuni mbinu mpya za rasilimali za pamoja ili kuwezesha usafirishaji wa mifugo na samaki kuvuka mipaka ya nchi wakati wa vipindi vya hali ya hewa visivyotabirika.

Hii inaweza kuruhusu matumizi ya bora ya rasilimali za ardhi na maji kutokana na tofauti za hali ya hewa kati ya nchi zetu. Mifumo hiyo pia inaweza kusaidia kuweka soko la chakula, samaki, na mifugo kuwa hai na kukuza amani na utulivu kwenye shoroba muhimu za maliasili katika shoroba (kwa mfano ushoroba wa Maasai Mara-Loliondo na ushoroba wa malisho ya Rwanda-Kagera).

Jambo la pili ni kujengea uwezo Wizara muhimu za Serikali na taasisi za usaidizi wa kibiashara (STUK) katika kusaidia uzalishaji unaozingatia mabadiliko ya tabianchi na upanuzi wa biashara—Kilimo cha matunda na mbogamboga, maua na ufugaji nyuki, uchumi wa bluu na misitu, na vipengele muhimu vya mauzo mengine ya kilimo na minyororo ya asili ya thamani.

Wizara muhimu za sekta zinapaswa kuweka pamoja sera za uzalishaji na biashara zinazohitajika ili kusaidia ukuaji endelevu unaozingatia mabadiliko ya tabianchi na upanuzi wa biashara.

STUK muhimu, hususan ofisi za viwango—ikiwa ni pamoja na zile mpya za Zanzibar—zinapaswa kusaidia ipasavyo wazalishaji na wauzaji bidhaa nje katika maeneo muhimu ya uzalishaji na usafirishaji nje ya nchi (pamoja na kanda za uzalishaji na mauzo ya nje wa Zanzibar-Pemba) ili kukidhi kikamilifu mahitaji ya ubora unaoongezeka wa masoko ya kimataifa.

Hivyo, mada hii ndogo itaangalia jinsi mfumo ikolojia wa kitaasisi unaoendana na hali ya uchumi wa kijani unavyoweza kuboreshwa na kuunganishwa vya kutosha na sekta nyingine muhimu za uzalishaji ili kuwezesha utimilifu wa faida kutoka katika ushirikiano wa pande zote wa biashara na uzalishaji, tija na upanuzi wa biashara.