Benki ya CRDB na miaka 2 ya kuliwezesha Taifa

Rais Samia Suluhu Hassan na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela wakisogeza vitambaa pembeni kuashiria uzinduzi wa jengo jipya la Benki hiyo ililopo katika barabara ya Ali Hassan Mwinyi, jijini Dar es Salaam. Wengine ni viongozi waandamizi wa Serikali.

Miaka miwili ya Rais Samia imebeba matumaini makubwa kwa Watanzania kwa namna amepambana kuhakikisha maisha ya Watanzania yanaimarika katika nyanja zote.

Benki ya CRDB, ambayo ni taasisi kubwa ya fedha na kinara kwa huduma za fedha nchini imekuwa ikifanya kazi bega kwa bega na Serikali ya Rais Samia tangu alipochukua ofisi Machi 19, 2021.

Chini ya uongozi wa Abdulmajid Nsekela, Benki ya CRDB imekuwa ikiunga mkono jitihada za maendeleo ya Tanzania kwa mkazo mkubwa huku uwezeshaji wanawake na vijana wajasiriamali kwa hivi karibuni ikiwa ni ajenda yake ya msingi. 

Wanawake na vijana ni makundi ambayo yamekuwa yakiachwa nyuma kwa muda mrefu katika shughuli za kiuchumi na hivyo kuchelewesha maendeleo yao na jamii nzima.

Rais Samia Suluhu Hassan (watatu kushoto) kwa pamoja na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Lela Mohammed Mussa (wapili kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela wakikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa maabara ya sayansi katika Skuli ya Sekondari ya Kizimkazi yenye thamani ya Sh50 Milioni iliyojengwa kwa msaada wa Benki ya CRDB Agosti 02, 2022. Wengine pichani ni viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Katika azma ya kujenga Taifa lenye kizazi cha vijana na wanawake wabunifu wanaoenda na kasi na mabadiliko ya sayansi na teknolojia, Benki hiyo chini ya mwamvuli wa kampuni yake tanzu ya CRDB Bank Foundation imekuja na programu yake ya iMBEJU ambayo ni programu endelevu ya uwezeshaji inayolenga kukuza uwezo kwa wajasiriamali wachanga vijana wenye bunifu mbalimbali na wanawake wenye biashara bunifu kupitia ushauri, mafunzo, na ufadhili wa mitaji wezeshi.

Programu ya iMBEJU inaendeshwa kwa miundo miwili; Muundo shindani wa uwezeshaji wa biashara changa za vijana, na muundo wa uwezeshaji wanawake wajasiriamali, anaeleza TullyEsther Mwambapa, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation.

Pia anafafanua kuwa kwa upande wa muundo shindani wa uwezeshaji wa biashara changa unafanywa kwa ushirika na taasisi za Serikali ambazo ni Tume ya TEHAMA (ICTC) na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ambapo maombi yote yanawasilishwa kwa njia ya mtandao kupitia washirika hao wa programu ya iMBEJU.

Kwa upande wa muundo wa pili ambao unahusu wanawake wajasiriamali, maombi yake yanawasilishwa katika matawi ya Benki ya CRDB yanayopatikana nchi nzima. Muombaji lazima awe mwanachama kutoka katika kikundi chenye makubaliano ya iMBEJU na Benki ya CRDB na viongozi wa kikundi lazima waidhinishe fomu za maombi. Fomu za maombi zinapatikana katika matawi ya Benki ya CRDB pamoja na kwa viongozi wa kikundi husika.

Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa akiwasilisha mada ya program ya imbeju inayolenga kuwezesha vijana wenye biashara bunifu pamoja na wanawake wajasiriamali.

Programu hii ya Imbeju itawezesha vijana na wanawake kuboresha biashara zao kupitia mafunzo, ushauri na mitaji wezeshi mambo yanayotarajiwa kukuza vipato vya makundi haya muhimu katika jamii ambapo takwimu za sensa za mwaka 2022 zinaonyesha vijana ni takribani 75% za wanawake wakiwa 51% ya jamii ya Tanzania.

Uanzishwaji wa programu hii umekuja wakati muafaka ambapo Rais Samia anatimiza miaka yake miwili ya uongozi ni jambo la kujivunia kwa Benki ya CRDB. Wakati Serikali kupitia halmashauri ikitenga asilimia 10 kwa ajili ya vijana na wanawake, Benki yenyewe inakuja na programu mahsusi ya uwezeshaji wanawake na vijana kuiuchumi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela akishika tuzo ya Euromoney iliyo-wasilishwa katika ofisi za benki hiyo jijini Dar es Salaam.

Mbali na uanzishwaji wa bidhaa na huduma mahsusi kwa ajili ya makundi mbalimbali, Benki ya CRDB hutenga asilimia 1 katika faida yake kutekeleza miradi ya kijamii yenye lengo la kusaidia Serikali kuboresha na kuweka mazingira wezeshi kwa Watanzania.

Mkakati wa benki katika kusaidia jamii umejikita katika maeneo manne; elimu, afya, mazingira na uwezeshaji wa vijana na wanawake, na kwa miaka miwili iliyopita peke yake benki imetumia kiasi cha Sh3.6 bilioni.

Katika upande wa afya, benki imetumia kiasi cha Sh1.13 Milioni, elimu (Sh889 Milioni), mazingira (Sh222 Milioni) wanawake, vijana na michezo (Sh998 Milioni) na miradi mingine (Sh1.17 bilioni) kwa mwaka 2021 na 2022.

Baadhi ya miradi iliyofanyika katika eneo la elimu ni pamoja na ujenzi wa madara mapya ya shule, ununuzi wa madawati zaidi ya 1000 kwa wilaya zilizopo Tanzania bara na visiwani, na ukarabati wa madarasa 31 katika shule 22 nchini.

Katika eneo la afya, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita pamoja na mambo mengine, benki imesaidia fedha za matibabu kwa watoto zaidi ya 200 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Ujenzi wa Kituo cha Mawasiliano cha Taasisi ya Saratani ya Ocean Road na pia imesaidia kutoa Sh220 Milioni kusaidia matibabu ya akina mama wenye ujauzito hatarishi katika Hospitali ya CCBRT.

Benki imechangia kuendesha kampeni ya ‘Pendezesha Tanzania’ kwa kuhamasisha upandaji wa miti nchi nzima kupitia matawi yake zaidi ya 263 yaliyosambaa nchi nzima.

Katika michezo, benki imeanzisha mbio za hisani za CRDB Bank Marathon, mashindano ya Ngalawa ya CRDB Bank Ngalawa Race yanayofanyika Kizimkazi Zanzibar, mashindano ya mpira wa kikapu ya CRDB Bank Taifa Cup pamoja na kudhamini Klabu ya Soka ya Namungo.


Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa akipokea moja ya kazi bunifu kutoka kwa kijana mbunifu alipotembelea eneo lao wakati wa uzinduzi wa programu ya iMBEJU inayoratibiwa na Taasisi ya CRDB Bank Foundation uliofanyika katika ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Mafanikio ya miaka 2 ndani ya Benki

Moja ya mafanikio makubwa kwa taasisi yoyote ni faida baada ya kodi, na Benki ya CRDB imefanya vizuri kwa mwaka 2022 kupata faida ya Sh353 bilioni ambayo ni rekodi mpya kuwahi kuwekwa na benki hiyo.

Mbali na faida hiyo, hivi karibuni Benki ya CRDB imesaini mkataba wa Euro Milioni 150 na Benki ya Uwekezaji ya Jumuiya ya Ulaya (European Investment Bank) kwa ajili ya kuongeza huduma za uwezeshaji fedha biashara ndogo na kati pamoja na uwezeshaji kwa wafanyabiashara wanawake na uwezeshaji katika uchumi wa Bluu.

Pamoja na mafanikio mengi yaliyopatikana na Benki hiyo ndani na nje ya nchi, Benki hiyo imefanikiwa kupata tuzo mbalimbali ikiwemo tuzo ya Benki Bora Tanzania inayotoa huduma kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati (SME) inayotolewa na Jarida maarufu la Global Finance kwa mwaka 2023 na ile ya Benki Bora nchini inayotolewa na Jarida la Euromoney kwa mageuzi makubwa iliyoyafanya katika sekta ya fedha mwaka 2022.