Asam Oil inajivunia uongozi wa soko la mafuta nchini

Muktasari:

Ukitaka kutaja orodha ya makampuni ambayo yamekuwa mstari wa mbele katika kusimamia sera ya maudhui ya ndani, basi hakuna namna ambayo kampuni ya Asam Oil itakosekana.

Ukitaka kutaja orodha ya makampuni ambayo yamekuwa mstari wa mbele katika kusimamia sera ya maudhui ya ndani, basi hakuna namna ambayo kampuni ya Asam Oil itakosekana.

Asam Oil inayomilikiwa na mfanyabiashara mzawa, inawakilisha makampuni machache ya mafuta yanayokua kwa kasi ambayo yanachangia sana pato la taifa na ukuaji wa uchumi.

Kampuni hiyo ndiyo inayoongoza katika uuzaji wa mafuta yanayozingatia ubora, usalama, afya na muda moja kwa moja.

Kampuni hii huuza mafuta ya dizeli au petroli moja kwa moja kwenye magari ya marafiki zetu nyumbani, kazini na wanapokuwa safarini. Asam Oil imejidhatiti vyema kufanyia kazi maagizo ya wateja wake na kuwafikishia mafuta milangoni mwao.

Kampuni ilianzishwa mwaka 2014, ikijihusisha na usafirishaji wa mafuta kwa kutumia magari na vituo vidogo vya mafuta katika mikoa 8 ambayo ni pamoja na vituo vya mafuta vya Engine na uwekaji wa vifaa vya kuwekea mafuta.

Kituo cha kwanza cha cha mafuta cha kampuni kilikuwa Vikindu mkoani Pwani na kimeajiri wafanyakazi wa kutosha ambao wanaweza kufanikisha malengo ya kampuni pekee.

Kampuni hiyo ambayo imejipambanua vyema kwa uuzaji wa mafuta nchini imeendelea kujitofautisha na washindani wake katika soko. Na moja ya hatua hizo ni kuhakikisha vituo vyake vyote vya mafuta na malori ya kusafirisha mafuta yanafanya kazi kwa saa 24 tofauti na vingine ambavyo hufunga biashara saa 22:00 jioni au chini ya hapo.

Mkakati mwingine ni uboreshaji wa huduma za maduka makubwa yanayopatikana katika vituo vya mafuta vya kampuni hiyo, ambapo kuna mpango wa kuunganishwa na mfumo wa malipo ya kielektroniki ili kurahisisha malipo ya gharama za maji na umeme.

Kusimamia kanuni za usalama

Katika eneo la usalama, umewekwa katika makundi mawili; usalama katika usafirishaji wa mafuta na vituo vya mafuta.

Katika suala la usalama kwenye vituo vya mafuta, huanzia pale tu mteja anapofika kituoni. Sera yake inaelekeza kuwa waendesha bodaboda wanapaswa kwanza kushuka katika pikipiki zao kabla ya kuweka mafuta katika vyombo vyao kwa ajili ya usalama.

Upo mkakati mwingine wa kupanua vituo vya mafuta kwa kuanzisha maeneo salama ya kukusanyika wafanyakazi pale wanapohisi kuwapo kwa hatari.

Hata hivyo, kampuni inakusudia kuweka kifaa katika bomba maalumu chini ya ardhi kitakachokuwa kikifanya kazi ya kufuatilia kwa ukaribu shughuli za kituo cha mafuta ikiwamo utoaji wa mafuta.

Pia kampuni huzingatia kanuni za usalama wakati wa upakiaji wa mafuta kwenye vituo kwa muda wa si chini ya dakika 15. Hii inafanywa ili kuwaepusha wateja na wafanyakazi dhidi ya mlipuko na kuimarisha bidhaa ya mafuta sokoni.

Kwa kuonyesha jinsi wanavyojali usalama wa wafanyakazi wake, kampuni hairuhusu wafanyakazi wake kutoa huduma kwa wateja wakiwa wamevaa kandambili, viatu vyenye uwazi, au bila ya kuwa na viatu, kwani ni kinyume na sera. Ili wafanyakazi waweze kufanya kazi ni lazima wawe katika mavazi yanayowakinga dhidi ya majanga ya ajali.


Nafasi ya mwanamke

Asam Oil ni miongoni mwa kampuni chache za Kitanzania ambazo zinatambua na kuheshimu nafasi ya mwanamke katika shughuli za ukuzaji uchumi.

Na hili linathibitishwa na Scolastica ambaye ni moja ya madereva malori wa kampuni hiyo. Scolastica, binti aliyekulia katika familia ya wasomi, anasema kuwa udereva malori haikuwa kazi ambayo aliwahi kufikiria kuifanya katika maisha yake.

“Mimi baada ya kufeli mtihani wa kidato cha nne, nikajikuta nimeenda kusomea fani ya urembo katika Chuo cha VETA, kwa bahati nzuri nilimuona dada mmoja pale chuoni akichukua kozi ya kuendesha mashine za barabarani na alikuwa akishangiliwa na watu wengine alipokuwa akifanya mafunzo kwa vitendo, jambo ambalo lilinipa hamasa kubwa na baadaye kuomba kubadilishiwa kozi ili nisomee uendeshaji wa dumper.”

Anasema baada ya kozi kuisha alipata kazi mgodini na huko alizidi kuhamasika baada ya kuona baadhi ya wafanyakazi wenzake wa kiume wakiendesha tipa ndogo.

Alijufunza kuendesha tipa ndogo kupitia mmoja wa wafanyakazi wenzake ambaye naye alijifunza kuendesha dumper kutoka kwake.

Hakuchoka Scolastica, baada ya hapo alijiendeleza kimasomo VETA mkoani Morogoro na baada ya kuhitimu aliomba kazi katika kampuni mbalimbali.

Scolastica anakiri kuwa kazi ya udereva malori ina kadhia zake licha ya ukweli kwamba haimzuii kuendelea kujituma.

“Madereva malori wanawake ni wachache kwa sababu kampuni nyingi hazina mfumo mzuri wa kuwajengea uwezo wanawake, pia wanawake wenyewe hawajiamini,” anaeleza zaidi.

Kwa sasa, Scolastica ni dereva wa malori ya mafuta katika kampuni ya Asam Oil akijivunia miaka 6 ya uzoefu kazini. Anakiri kuwa hakuna kampuni aliyowahi kuona ikiwapa wanawake kipaumbele kama Asam Oil.

Kwa upande wake, Meneja wa Stesheni ya Asam Oil, Mwembeyanga, Temeke, Dar es Salaam, Bi Hellen katika mahojiano na Gazeti hili, anasema kuwa kwake haikuwa rahisi kuamini uwezo wake alipoteuliwa kuwa meneja wa stesheni hiyo.

“Sio rahisi kwa kuwa watu wengi katika akili zao tayari wanaona ni ngumu katika ngazi za uongozi wa juu wa kampuni mwanamke kupata nafasi, kwa kuwa imezoeleka ni za wanaume na wewe (mwanamke) kuonekana huwezi.”

Hellen ana miaka miwili na nusu katika majukumu yake na akidai kuwa moja ya changamoto kubwa ni kasumba iliyopo dhidi ya wanawake ambayo ni tatizo la dunia nzima.

Akijibu swali la kwanini, kampuni ya Asam Oil imekuwa na imani kubwa kwa wanawake kuliko wanaume, anasema kuwa yote ni kwa sababu wanawake ni wachapakazi, waadilifu na waaminifu zaidi.


Mafanikio

Kampuni inaona ongezeko la vituo vya mafuta kama mojawapo ya mafanikio yake makubwa. Hii imesaidia kuhudumia watu wa maeneo ya mbali hususan wale wasiofikiwa na huduma za vituo vya mafuta (dizeli au petroli) hapo awali. Kampuni ya Asam Oil kwa sasa inajivunia kuhudumia maghala yote ya mafuta nchini.

Changamoto

Miongoni mwa vikwazo vikubwa vinavyoikabili Asam Oil, ni vita dhidi ya udanganyifu. Baada ya kuweka jitihada za kuja na mifumo bunifu na ya kisasa ya kufuatilia na kusimamia usalama, imani ya kushinda vita dhidi ya udanganyifu wa madereva wa malori ya mafuta katika biashara ya mafuta imeanza kuonekana walau kwa kipindi hiki.

Kampuni inashauri kuwepo na kitengo kimoja cha serikali kitakachowezesha makampuni ya mafuta kutekeleza mahitaji hayo kwa urahisi zaidi kuliko ilivyo sasa ambapo utahitajika kutembelea kila ofisi kwa muda wake.

Mipango ya baadaye

Kwa kuangalia nyakati hizi zinazobadilika, kampuni inatazamia kuzindua kadi maalumu ambayo itawezesha mteja kupata punguzo la mauzo ya huduma mahususi zinazotolewa na kampuni. Ikiwa hiyo haitoshi, Asam Oil inatarajia kuanzisha mfumo utakaowawezesha wateja kujihudumia wenyewe kama vile wako nyumbani.

Mbali na shughuli za kampuni, utekelezaji wa miradi ya kijamii ni shukrani tosha kutoka kwa kampuni yoyote, kampuni inapanga kuanzisha kampeni yake ya ndoto ya kupanda miti ambapo, wanatamani kupanda miti Milioni 1 ifikapo 2050.