Simba yapanda kileleni...Phiri amkamata Mayele

Muktasari:

  • TIMU ya Simba imemaliza kibabe mzunguko wa kwanza Ligi Kuu baada ya kuichapa Coastal Union mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Mkwakwani ikifikisha pointi 34.

TIMU ya Simba imemaliza kibabe mzunguko wa kwanza Ligi Kuu baada ya kuichapa Coastal Union mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Mkwakwani ikifikisha pointi 34.

Mabao mawili ya Moses Phiri dakika ya 53, 61 na moja la Clatous Chama dakika ya 89 yametosha kuihakikishia Simba ushindi huo mbele ya Wagosi Wakaya.

Simba imependa kileleni mwa msimamo wa ligi ikifikisha pointi 34 baada ya michezo 15, miwili zaidi ya Yanga yenye 32.

Wagosi wa Kaya wameendelea kusalia nafasi ya 13 kwenye msimamo ikiwa na pointi 12 baada ya mechi 14.

Phiri amefikisha mabao 10 kwenye ligi, idadi sawa na Fiston Mayele wa Yanga.

Clatous Chama amefikisha asisti saba kwenye ligi akiwa ndio kinara baada ya kutoa pasi ya bao la kwanza katika mchezo huo likifungwa na Phiri dakika ya 53 kipindi cha pili.

Katika mechi 15 Simba imeshinda 10, sare nne, kufungwa mmoja, pointi 34, mabao ya kufunga 31, imetikiswa mara saba.
Kwa upande wa Coastal Union katika mechi 14, imeshinda tatu, sare tatu, imefungwa minane, pointi 12, mabao ya kufunga  12 ya kufungwa 18.

Katika michezo nane ya mwisho Coastal Union kucheza na Simba kwenye Ligi Kuu haijaweza kupata ushindi zaidi ya suluhu mbili huku ikiwa na kumbukumbu ya vichapo vikali vya mabao 8-1 cha Mei 8, 2019 na 7-0 Novemba 21, 2021.

Kikosi cha Simba kilichoanza ni; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Joashi Onyango, Henock Inonga, Mohamed Huseen, Sadio Kanoute, Pape Sakho, Mzamiru Yasin, John Bocco, Mosses Phiri na Clatous Chama.

Upande wa Coastal Union kikosi ni; Mahamoud Mroivili, Cosmas Andrew, Omar Mbaruku, Lameck Lawi, Khatibu Kombo, Mtenje Albano, Moubarack Amza, Betrand Ngafei, Vincent Abubakar, Greyson Gwalala na Hamad Majimengi.