Mzamiru kwa Sawadogo? Bado

Muktasari:

  • Ujio wa Sawadogo ni kama unataka kumtoa kwenye reli Mzamiru ambaye amekuwa na uwezo mkubwa kwenye eneo la ukabaji na hata uchezeshaji katika kiungo cha Simba.

KIUNGO wa Simba, Mzamiru Yassin amepigiwa chapuo na mastaa wa zamani wa timu hiyo na kuweka wazi uwezo wake hauwezi kulinganishwa na kiungo wao mpya Hamed Sawadogo.

Ujio wa Sawadogo ni kama unataka kumtoa kwenye reli Mzamiru ambaye amekuwa na uwezo mkubwa kwenye eneo la ukabaji na hata uchezeshaji katika kiungo cha Simba.

Sawadogo amesaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia Simba katika dirisha dogo la msimu huu.

Kiungo huyo akiwa kwenye kikosi cha Simba ameshacheza mechi mbili na zote alianza huku moja ikiwa ya Ligi (Dodoma Jiji) na kombe la Azam  (Coastal Union) wakati upande wa Mzamiru yeye kwenye mechi hizo alikuwa benchi kwenye mchezo dhidi ya Coastal huku wa Dodoma hakuwepo kabisa.

Kitendo cha kocha  Roberto Oliviera 'Robertinho' kumtoa mdogo mdogo Mzamiru kwenye mipango yake ni kama vile wadau wa soka wameshangazwa kwani wana amini mchezaji huyo bado ana mchango mkubwa tofauti na Sawadogo.

Akizungumza na Mwanaspoti, mshambuliaji wa zamani wa Simba, Bakari Kigodeko alisema uwezo wa Mzamiru upo juu na anajituma zaidi lakini upande wa Sawadogo kwa sasa ni mapema sana.

"Sawadogo bado sana kwa Mzamiru, inabidi ajitume sana na inawezekana huko mbele akamzidi lakini ukweli kwa sasa bado kiwango chake hakijawa kikubwa sana,"alisema Kigodeko.
Upande wa beki wa zamani Simba, Fikiri Magoso alisema hakuna ubishi kwamba Mzamiru amekuwa kwenye kiwango kikubwa tofauti na Sawadogo na kulinganishwa na mchezaji huyo ni kama kutopewa thamani kubwa.

Magoso alisema Mzamiru amekuwa na mchango mkubwa ndani ya Simba na timu ya Taifa na hilo linatokana na kujituma kwake anapokuwa yupo ndani ya uwanja.

"Mzamiru kwa maoni yangu mimi naona kabisa ni mchezaji mzuri na anayeipambania timu muda wote, huyo Sawadogo bado anahitaji muda zaidi.,"alisema Magoso.