Mayele: Nataka kuweka rekodi

BAADA ya kuanza msimu kwa kasi akifunga mabao 11 katika mechi saba za mwanzo za mashindano, straika wa Yanga, Fiston Mayele amesema kazi bado haijaisha kwani anataka rekodi zaidi msimu huu.
Mayele alianza kwa kuifunga Simba mabao mawili katika mechi ya Ngao ya Jamii ambayo Yanga ilishinda 2-1, kisha akafunga bao moja moja kwenye mechi za Ligi Kuu Bara dhidi ya Polisi Tanzania, Coastal Union na Mtibwa Sugar kabla ya kucheza michezo miwili ya raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zalan ya Sudan Kusini na kufunga hat-trick mbili kwa kila mechi.
Nyota huyo kutoka DR Congo aliyemaliza msimu uliopita na mabao 16, moja pungufu na aliyokuwa nayo kinara, George Mpole wa Geita Gold, aliliambia Mwanaspoti kuwa, ameshajua ni wapi alikosea msimu huo na sasa amejipanga kupiga kazi kwelikweli na kuweka heshima ndani na nje ya nchi.
“Msimu uliopita haukuwa mbaya kwangu na kwa Yanga kiujumla, ila kuna baadhi ya sehemu tuliteleza na kushindwa kufikia baadhi ya malengo binafsi na ya klabu kwa ujumla licha ya tulitimiza asilimia kubwa sana ya kile tulichokipanga,” alisema Mayele na kuongeza;
“Kama klabu tumejipanga kuendelea tulipoishia, ila binafsi natamani kufanya vizuri zaidi. Naamini Yanga ya msimu huu ni bora sana, kuna kila aina ya mchezaji anayeweza kuibeba timu hivyo naamini kwa mchango mkubwa wa wenzangu nitafanya makubwa zaidi."
Mayele alifafanua; "Kila mchezaji anatamani kuwa bora na kuchangia mafanikio ya timu kutokana na eneo lake analocheza. Kipa hataki kufungwa wala beki hataki kupitwa hivyo na mimi kama mshambuliaji natamani kufunga zaidi na ikiwezekana kuvunja na kuweka rekodi zilizopo kwenye ligi ya ndani na Kimataifa hivyo nipo tayari kuipambania Yanga.”
Yanga inatarajiwa kushuka uwanjani Jumatatu kucheza na Ruvu Shooting katika mechi ya Ligi Kuu Bara kisha kuisubiri Al Hilal ya Sudan kwa mchezo wa awali wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika utakaochezwa wikiendi ijayo kabla ya wiki ijayo kurudiana ugenini nchini Sudan.