Ken Gold yatimua benchi la ufundi

Muktasari:

  • Mnyali alijiunga na timu hiyo tangu msimu uliopita akitokea Mbeya Kwanza, ambapo kwa sasa alikuwa ameiongoza mechi 12, akishinda tano, sare mbili na kupoteza tano wakiwa nafasi ya nane kwa pointi 17.

Mbeya. PAMOJA na ushindi mnono wa walioupa Ken Gold, lakini benchi la ufundi chini ya kocha mkuu, Michael Mnyali wamefikia makubaliano ya pande zote na timu hiyo kuachana.

Ken Gold jana ilicheza uwanja wake wa nyumbani Sokoine jijini hapa, ikiibuka na ushindi wa mabao 5-2 dhidi Pan African huku nyota wake, Mishamo Michael akiondoka na mpira kufuatia kufunga mabao matatu ‘hat-trick’.

Mnyali amethibitisha kuachana na timu hiyo sambamba na msaidizi wake, Latifu Masesa akieleza kuwa mabosi wake hawajaridhishwa na matokeo ya timu hiyo.

“Ni kweli leo ndio mechi yangu ya mwisho kuiongoza Ken Gold, nimeondoka na msaidizi wangu, Masesa, sababu kubwa ni kwamba hawajaridhishwa na matokeo kwa ujumla,” amesema Mnyali.

Katibu wa timu hiyo, Benson Mkocha amesema wameamua kuachana na makocha hao kutokana kutoridhishwa na matokeo huku wakianza hesabu za kusaka kocha mpya.

“Tumeachana nao kuanzia leo baada ya kuangalia mwenendo wa timu na matokeo yake kutoturidhisha, muda wowote tutamtangaza kocha mpya,” amesema Mkocha.