Paula kumbuka hata wahuni wanazeeka

Yes mtoto wa P Funk. Yes mtoto wa Kajala Masanja. Viumbe wawili wenye mizuka ya sanaa. Mmoja mchizi muziki mwingine mchizi filamu ingawa siyo kiviiile. Ni kama Kanumba aliamua tu. Kwa pamoja waliunganisha damu na kumpata Paula.

Achana na Kajala mwenye akili za Bongo movie huyu. Uliza watu Kajala wa Jiteute ya Phabian Masawe, Dada K wa ‘Obey Polisi’. Wakati huo rangi yake ni ile ile ya Bariadi, Maswa, Magu, Kwimba na Buzuruga. Yaani kabla haijaongezwa 'bando la wiki'.

Alikuwa mfano halisi wa mtoto wa kike wa Kiafrika. Mzuri mpaka anakera. Madogo kibao wamekula vitasa vya kutosha kwa P Funk pale. Hakutaka ulete mazoea na 'tunda lake la Kisukuma'. Ukienda kurekodi fuata kilichokupeleka.

Ukitaka kumzoea Kajala lazima utandikwe na nyimbo utarekodia kwa bibi yako. Wivu wa Majani hakuna aliyeshangaa. Hata wewe ungeleta wivu mtoto mteke kama maini. Kichwani nywele fupifupi zinavutia kuliko posho za bungeni.

Kajala yule ningeambiwa nichague ajira ya Unicef au nimmiliki, bila ajizi wala kusita siyo tu ningeikataa ajira hiyo, bali ningewashtaki kwa kumfananisha Kajala na vitu vya kijinga. Ningeikana mara tatu ajira yao.

Kama marehemu Ndikumana alivyochanganywa na 'mwili rojorojo' wa Irene uwoya. Ndivyo ambavyo Majani alikuwa 'Zuzu' mbele ya Kajala. Uzuri ulimfanya awe msichana maarufu mjini bila kazi yoyote.

Hakuwa msanii wakati huo. Wala hakushiriki Miss Bantu ingawa alistahili. Majani akasema “msinichezee’’. Akamficha jumla. Pale studio Bamaga. Ilikuwa rahisi kusikiliza 'biti' au kurekodi kuliko kumuona Kajala.

Alilindwa na kuhifadhiwa kama Malkia wa Sheba. Wasanii waliomfahamu kabla aliwavutia kuliko 'biti' za Majani. Yaani ilikuwa raha kumtazama Kajala kuliko kusikiliza makelele ya midundo studio pale. Nielewe… Kajala huyu na yule, yule alikuwa bora zaidi.

Maendeleo huja kama mafuriko. Yaani yanaleta vitu vingi hata visivyohitajika, huondoa vitu vingi hata vinavyohitajika kuwepo. Maendeleo yameondoka na rangi adimu ya Kajala. Rangi iliyofanana na mbao ya mninga imetoweshwa kikatili.

Alikuwa na rangi ya 'chocolate' haswa. Alikuwa zaidi ya utundu wa 'filta' za instagram wanazokoleza madem wa mjini. Unamjua Kajala? Achana na biashara ya muziki. Penzi la Kajala lilipoota mbawa kikawa chanzo cha Majani kulisusa 'gemu'.

Mimi siyo tu ningesusa 'gemu', pia ningeenda kuishi kwa 'Mshua' Uholanzi. Bora kuachwa na basi la mshahara kuliko kutengwa na mwili na sura ya Kajala yule. Dem mkali mpaka anapendwa na madem wenzake.

'Ene wei' siyo rangi ya Kajala tu. Maendeleo yameondoa vitu vingi. Kila shirika nchini au idara yoyote ilikuwa na bendi ya muziki. Uhamiaji, Bima, DDC, Tancut Almasi, JKT, Jeshi la Polisi na mashirika na taasisi nyingi zilimiliki bendi.

Hivi sasa siyo tu hakuna bendi, hata mashirika yenyewe mengi yametoweka kama kisonono. Dunia imebadilika sana. Wazee waliburudishwa na muziki mwishoni mwa juma. Waliajiriwa kama wafanyakazi wengine kwenye shirika au taasisi husika.

Bendi za mashirika zilikufa kama mashirika yenyewe. Zikabaki bendi za watu binafsi. Nazo hivi sasa zimekufa zinasubiri mazishi.

Hata muziki wa kizazi kipya makundi yametoweka jumlajumla.

Hakuna Wanaume Family/Halisi wala East Coast Team. Wamebaki wasanii binafsi ambao nao siyo wengi kwa kiwango kile. Mwaka unaenda wa 14 huu mastaa halisi wanabaki Diamond, Alikiba na Konde. Wengine wanaishia kuwa wasindikizaji mpaka kimafanikio. Nenda Nigeria hapo huoni tofauti kubwa ya Davido, WizKid, Tekno, Burna Boy, P Square na wengine kama kina Don Jazz.

Hawalingani ndiyo lakini hawatofautiani kama Bongo. Huwezi kuona staa wa kweli ndani ya Nigeria akiishi kwenye nyumba ya kupanga. Lakini Bongo mastaa waliopanga ni wengi kuliko wenye nyumba. Lakini wote wanaitwa mastaa Kibongobongo.

Hata wizara husika hapa kwetu. Sanaa wanafanya kama kitu cha ziada. Wanachofuatilia ni matusi na jumbe zinazokera utawala. Zaidi ya hapo hawafuatilii lolote. Ndio maana wasanii wa kuigiza hawaeleweki hii leo. Wanaonekana wana nafuu ya maisha hawana kazi mitaani wala tamthilia runingani. Wenye kazi huko mitaani na tamthilia runingani kila siku, hawaonyeshi nafuu ya mafanikio.

Basata nao wako 'bize' kusubiri Diamond aimbe matusi wamfungie. Ney wa Mitego na Nikki Mbishi watoe ngoma za kuongelea 'ishu' za watawala wawafungie. Lakini kukuza sanaa na soko hilo jukumu wamewaachia kina Said Fella.

Vijana wako 'bize' na instagram.

Chuo cha Sanaa Bagamoyo hakina ile harufu ya utamu kama wakati ule. Hakivutii vijana kwenda kujifunza sanaa. Ukiwakuta Bagamoyo ujue wanavizia wajane wa kizungu kwenye fukwe.

Paula kazaliwa kipindi ambacho utandawazi ni mkubwa kuliko imani ya dini zote. Mtoto anavutiwa zaidi na matumizi ya simu na mitandao kuliko madrasa na 'sande skuli'. Kipindi ambacho wanaijua sura ya Davido kuliko ya Kardinali Pengo.

Habari za Diamond madem zake wanazijua zaidi kuliko kuosha miili yao. Mama yake, Kajala ni staa. Amekuwa staa kabla ya usanii wa kuigiza. Baba yake ni staa wa muziki hata kabla ya kukutana na mama yake.

Toto la mastaa 'automatikale' litakuwa staa pia. Ndiyo Paula. Bahati mbaya sana tena sana. Mara nyingi Paula amekuwa akihusishwa na upuuzi mwingi mitandaoni. Kuliko mambo mema mengine. Kuna wakati alizushiwa kurekodi 'video fupi’ ya ngono. Habari zake zikasambaa sana akiongelewa kama mtu mzima. Kumbe ni mtoto mdogo bado anayehitaji kulindwa na jamii. Lakini jamii ikamgeuza kuwa kitu tofauti.

Kwa sababu mama yake alitaka Paula aishi kama yeye. Mtoto wa shule tayari alikuwa na kurasa zake mitandaoni. Anajibishana na mashabiki na mastaa kibao. Elimu na huo upumbavu ni maji na mafuta. Ilikuwa ngumu mno kufaulu. Walezi hizi lawama zinawavaa kama ngozi. Hazibanduki. Maendeleo yamefanya taarifa za Paula ziwe wazi kama vazi la kahaba.

Miaka mitano nyuma tungepeleka lawama kwa walezi. Leo tunamueleza yeye kuwa hata wahuni huzeeka.