Mwanamuziki Lokassa ya Mbongo afariki dunia

Mwanamuziki, Denis Lokassa maarufu Lokassa ya Mbongo enzi za uhai wake.

Muktasari:

  • Mwanamuziki mkongwe kutoka nchini Congo, Denis Lokassa maarufu Lokassa ya Mbongo amefariki dunia jana Jumanne usiku Machi 14, 2023 nchini Marekani baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Dar es Salaam. Mwanamuziki mkongwe kutoka nchini Congo, Denis Lokassa maarufu Lokassa ya Mbongo amefariki dunia jana Jumanne usiku Machi 14, 2023 nchini Marekani baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Lokassa ambaye alikuwa ametimiza miaka 80, alikuwa ni kiongozi wa bendi maarufu ya Soukous Stars ambapo ilikuwa ikifanya shughuli zake Paris, Ufaransa.

Miongoni mwa bendi ambazo amefanya nao kazi ni pamoja Tabu Ley Rochereau’s Afrisa International na baadaye akajiunga na African Stand Bendi.

Mwanamuziki huyo amekuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari pia alikuwa akusumbuliwa na kupooza miaka michache iliyopita.

Mwanamuziki mwenzake Mekanisi Modero amesema amepokea taarifa za msiba wa Lokassa kutoka kwa mhudumu wa afya ambaye alikuwa akimuuguza.

“Alikuwa akipumua kwa shida kabla ya mauti kumfika katika mji wa Nashua New Hamshire nchini Marekani,” amesema.

Lakassa atakumbukwa kwa vibao ambavyo vilitamba kama vile Bonne Annee, Monica, Marie- Josse na Assitou.

Mwanamuziki huyo atakumbukwa kwa kulikung’uta gitaa wakati akiwa na Tabu Ley Rochereau’s Afrisa International kuanzia mwaka 1970 hadi 1978.

Wakati akiwa na Afrisa alifanya kazi na waimbaji maarufu Pepe Ndombe, Sam Mangwana na Michelino Mavatiku Visi.

Mwanamuziki huyo licha ya kuwa raia wa Congo, alifanya kazi yake ya muziki akiwa nje ya nchi hiyo kwa muda mrefu.