Kifo cha Mussa Babaz chamuibua Profesa Jay, familia yake yazungumza

Muktasari:

  • Mashabiki wa Profesa Jay wameshindwa kuzuia furaha zao mara baada ya msanii huyo kuibuka katika mtandao wa Instagram na kuandika ujumbe wa kutoa pole kufuatia kifo cha meneja wa wasanii Mussa Babaz kutoka nchini Kenya.

Dar es Salaam. ‘Kifo cha Mussa Babaz chamuibua Profesa Jay’. Hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya msanii huyo ambaye jina lake halisi ni Joseph Haule na Mbunge wa zamani wa Mikumi, kuibuka kwenye mtandao wa Instagram na kuachia ujumbe wa kuomboleza kifo cha Mussa Babaz.

Profesa Jay hajawahi kuonekana hadharani wala kupakia chochote kwenye mitandao ya kijamii tangu alipolazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa siku 127 akipatiwa matibabu baada ya kuwa na changamoto ya kiafya.

Hata hivyo jana Jumatatu Machi 13 mwaka huu msanii huyo aliibukia kwenye ukurasa wa kijamii wa Instagram na kuandika ujumbe uliosomeka “Poleni sana wanangu, Tumuombee BABAZ apumzike Salama, Amina.” ni baada ya msanii Roma Mkatoliki kupakia video akiomboleza kifo cha Babaz ambaye alikuwa ni meneja na mwanzilishi wa kundi la Rostam linaloundwa na Roma na Stamina.

Katika andiko hilo Roma aliandika “Lakini Hakuweza Kufanikiwa, Tumempoteza Mungu wetu Baba, Mwanzilishi wa Rostam, Roho yake ipumzike kwa Amani. Rambirambi zangu kwa Familia na Watu wa Mombasa,”aliandika Roma na baadaye Profesa Jay akasindikiza na ujumbe huo.

Baadhi ya watu walishidwa kuzui furaha zao baada ya kuona ujumbe wa Profesa Jay ammbaye hajawahi kupakia chochote kwenye mitandao yake ya kijamii tangu Januari 23, 2022 akiwemo mtu aliyejitambulisha kwa jina la Funditechnician, aliandika “Nimefurahi kuona coment ya Professor Jay Mungu yu mwema”, razkenya aliandika, kaka am happy to see your comment, hali yako vipi? Unaendeleaje? Tunakujali siku zote. #wamitulinga.

Mussa Babaz ni promota na meneja wa wasanii kutoka nchini Kenya, alifariki jana Machi 13, 2023 na katika enzi za uhai wake aliwahi kufanya kazi na wasanii wa Tanzania kama Roma na Stamina (ROSTAM), Young Killer, Jay Melody, Aslay chini ya kampuni yake Babaz Entertainment.

Mwananchi Digital ilimtafuta mdogo wa Profesa Jay, Nicholous Haule ‘Black Rhino’ ambaye amekuwa ndio amekuwa msemaji wa familia katika kipindi chote ambacho msanii huyo anaumwa ili kujua kama kweli ni yeye ameandika ujumbe huo na kutaka kujua kiujumla maendeleo yake kiafya.

Katika majibu yake, Black Rhino amesema “Yaah itakuwa ni ujumbe wake, kwa sababu sasa hivi anatumia simu zake, anachati kama kawaida, ukweli sasa hivi ameimarika zaidi na zaidi ukilinganisha na alivyokuwa awali.

“Kwa hiyo sasa hivi anaweza kuandika meseji, kujibu meseji, uwezo wa kumpigia simu mkaongea, anaendelea vizuri,”amesema Rhino.

Kuhusu Babaz alisema ni mtu ambaye walikuwa wanafahamiana kwani alishawasaidia wasanii mbalimbali, hivyo Profesa Jay kama wasanii wengine ameguswa na msiba huo.

Akizungumzia kuhusu hali yake kwa sasa, amesema msanii huyo bado anaendelea na mazoezi ya viungo kwa sababu yupo katika hatua za kupambania kurudisha afya yake lakini sio mtu aliyepona kabisa na kuweza kurudi katika shughuli zake za kila siku.

“Kumbuka huyu mtu aliumwa takribani mwaka mzima, kibinadamu kurudi haraka katika hali ya kawaida na kuanza kufanya shughuli ulizokuwa unazifanya awali ni ngumu,”alifafanua Rhino.

Hata hivyo amewaomba mashabiki zake waendelee kuvuta subira kwani atakapokuwa sawa atazungumza mbele ya umma rudi yake.