Filamu 189 zapenya tuzo za filamu, Joti atajwa mara nyingi

What you need to know:

Jumla ya filamu 189 zimetajwa kupenya mchujo wa awali kuwania tuzo za filamu bora mwaka huu, huku mchekeshaji Joti akitajwa mara nyingi.

Dar es Salaam. Jumla ya filamu 189 zimetajwa kupenya mchujo wa awali kuwania tuzo za filamu mwaka huu, huku mchekeshaji Lucas Mhuvile maarufu kwa jina la Joti akiongoza kujitokeza mara tano katika tuzo hizo.

Orodha hiyo imetolewa leo Jumanne Novemba 29, 2022 na kamati inayosimamia tuzo hizo katika mkutano na waandishi wa habari.

Akitaja orodha hiyo, Willium Mtitu mbaye ni mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo, amesema Joti ameingiza filamu tano ambayo ni Mvuvi, Msomi Tunakwenda Kuoa, Usipite Eneo la Jeshi, Sitaki ugali na Kikao na kumfanya kuwa msanii aliyeingiza kazi nyingi katika tuzo hizo.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa bodi ya filamu, Kiagho Kilonzo amesema idadi ya filamu zilizopenya katika hatua hiyo ya awali kwa mwaka huu imeongezela kwa asilimia nne  ukilingnisha na mwaka jana wakati tuzo hizo zinaanza kutolewa ambapo zilikuwa 120.

Pia amesema katika uwasiliashaji wa kazi hizo mara baada ya kufungua dirisha ya kuzipokea Oktoba mwaka huu, filamu 840 ziliweza kuwasilishwa ikiwa ni ongezeko la asilimia 23 ya filamu zilizowasilishwa mwaka jana ambazo zilikuwa 630.

"Ukiacha wingi wa filamu lakini pia kumekuwepo na ubora mkubwa katika fani na maudhui hadi kuipa kamati wakati mgumu kuzichuja hadi kuzipata zilizo bota," amesema Katibu hiyo.

Kwa upande wake Joti amesema siri ya kuwasilisha kazi hizo tano ni katika kujaribu bahati yake kwa kuwa mwaka jana aliwasilisha mbili na akashinda moja.

"Kila kitu unajifunza kutokana yaliyopita, hivyo niliona kama mwaka jana niliwasilisha kazi mbili nikashinda moja, basi mwaka huu ngoja niingize nyingi ambazo nashukuru katika mchujo wa awali zote zimepita na nina matumaini hata katika fainali za utaji tuzo nitashinda pia," amesema Joti.

Akieleza faida ya kushiriki tuzo hizo, Joti ambaye mwaka jana aliibuka mchekeshaji bora, amesema inamuongezea uwanda mkubwa wa kufanya kazi na watu mbalimbali, inamuheshimisha na kuona kile wanachofanya wasanii kinathaminiwa na serikali na jamii kwa ujumla.

Mastaa wengine walioingia katika kinyng'anyiro hicho ni Chuchu Hans kupitia filamu zake mbili ya Cheupe na Laura.

Pia yupo Blandina Chagula (Johari) na filamu yake ya 'Maji ya Shingo', Leah Mwendamseke (Lamata) na tamthiliya ya Jua Kali na Neema Ndempaya na filamu yake ya Malkia na ile ya Karma, mchekeshaji Tabu Mtingita na filamu yake ya Mama mkwe.

Tuzo hizo zinatarajiwa kutolewa Desemba mwaka huu jijini Arusha.