Amapiano isivyowatambua wasanii bongo

Licha ya wasanii wengi na wakubwa wa Bongofleva kutoa nyimbo nyingi za miondoko ya amapiano, hakuna hata mmoja aliyepata nafasi katika tuzo za muziki huo nchini Afrika Kusini, huku wenzao wa Nigeria wakipeta.

Msimu wa pili wa Amapiano Awards utafanyika Aprili 2, 2023 katika ukumbi wa Sun Arena, Pretoria ambapo vipengele zaidi ya 25 vitawaniwa na wasanii wa Afrika Kusini na kwingineko Afrika.

Mkongwe wa miondoko hiyo nchini humo, Kabza De Small ndiye anaongoza kuwania vipengele vingi, ambapo anawania tisa, kikiwemo cha Msanii Bora wa Mwaka, huku nyimbo zake nne zikiwania kipengele cha Wimbo Bora wa Mwaka.

Wengine ni Young Stunner na Toss wanaowania vipengele vinane, Waffles vipengele saba, huku Kelvin Momo, Daliwonga na Focalistic wakiwania vipengele sita kila mmoja.

Miondoko ya amapiano ilianza mwaka 2012 huko Gauteng, Afrika Kusini, ingawa kuna utata ni wapi hasa asili ya muziki huo nchini humo, wapo wanaodai ulianzia katika vitongoji vya Johannesburg - Soweto.

Kwa miaka mitatu iliyopita, wasanii wa Bongofleva kama Diamond Platnumz, Marioo, Harmonize, Rayvanny, Zuchu, Nandy, Whozu, Mbosso, Damian Soul na wengineo walitoa nyimbo za amapiano ambazo zilifanya vizuri sana, lakini wamekosekana kwenye tuzo hizo, jambo linaloacha maswali kwa wengi.

Kipengele ambacho wasanii Bongo walitazamiwa kuwepo (Friends of amapiano), ni wasanii wa Nigeria tu ndio waliopenya ambao ni Asake, Davido na Wizkid.

Akizungumza na gazeti hili, Damian Soul, aliyefanya vizuri na wimbo wake wa amapiano ‘Mapopo’, alisema tuzo sio kitu cha msingi sana, ila kinahamasisha, ila kukosekana kusiwakatishe tamaa wanaofanya amapiano

Alisema tuzo zinaweza kuwa na siasa au mchezo wa watu fulani, unaweza kushangaa mwasisi wa miondoko ya reggae, Bob Maley hakuwahi kushinda tuzo ya Grammy, lakini leo hii Beyonce ndio ana Grammy nyingi kuliko msanii yeyote duniani.

“Kuna wasanii wamefanya vizuri kwenye miondoko hiyo Afrika Mashariki, wasipotuweka kwenye tuzo zao haimaanishi amapiano zilizofanyika nchini sio kali.

“Wamewaweka Wanigeria kwa sababu wamewazidi kwenye soko lao, wapo mbali, hao kina Asake, Davido, kwa hiyo kwa tasnia yetu bado kuna vitu hatujawashinda, hivyo tunatakiwa kupambana kuhakikisha tunaenda katika levo kubwa ya kidunia ambayo watakuwa hawana budi kutukubali,” alisema Damian Soul.

Kwa upande wake G Nako kutoka kundi la Weusi, alisema kila tuzo zinakuwa na malengo yake, hivyo haya ni matokeo ya waandaaji kwa kuzingatia walikuwa wanaangalia maeneo gani hasa.

“Tuzo sio kipimo cha kufanya vizuri, nyingine zinaweza kuwa za kimkakati, huwezi kujua kwa sababu hizo tuzo hazifanyiki hapa kwetu, lakini sisi tunachojua kuna kazi ambazo zimefanya vizuri hapa, Kenya, Uganda na maeneo mengine,” alisema G Nako.

Mdau wa Bongofleva na Promota, DMK Global ambaye amekuwa akiwaandalia wasanii Bongo shoo nchini Marekani alisema:

“Tunahitaji kuwekeza sana katika kuutangaza muziki wetu nje ya jumuiya ya Afrika Mashariki.

Naye msanii wa kundi la Navy Kenzo na Prodyuza, Nahreel alisema muziki wa Bongofleva unahitaji maboresho ya kiukuaji ili kushika wasikilizaji wengi wa nchi nyingine, kitu ambacho Afrika Kusini na Nigeria wamefanikiwa baada ya kuuamini muziki wao.

“Hizi zote unazosikia kama amapiano zimeboreshwa kidogo, utakuta kuna Jazz, Soul, House, vivyo hivyo Afro Beats, kuna RnB, Hip Hop, kwa hiyo watu wanachanganya na kuboresha wanakuja na kitu ambacho kinaweza kusikilizwa na wengi, tuboreshe muziki wetu,” alisema Nahreel.