Baleke amtisha Mayele

Muktasari:

  • Baleke aliyejiunga na Simba dirisha dogo na kufunga bao pekee la mchezo wa ligi dhidi ya Dodoma Jiji kabla ya kuwasha moto kwenye ASFC walipovaana na Coastal Union na kushinda bao 1-0 lililodungwa na Sadio Kanoute, alisema kupitia mechi hizo mbili amejifunza mengi.

MSHAMBULIAJI mpya wa Simba, Jean Baleke ni kama amemtisha kinara wa mabao wa Ligi Kuu, Fiston Mayele wa Yanga baada ya kusema amejipanga kufanya mambo makubwa baada ya kuanza kwa kasi akiwa na uzi wa kikosi hicho cha Msimbazi.

Baleke aliyejiunga na Simba dirisha dogo na kufunga bao pekee la mchezo wa ligi dhidi ya Dodoma Jiji kabla ya kuwasha moto kwenye ASFC walipovaana na Coastal Union na kushinda bao 1-0 lililodungwa na Sadio Kanoute, alisema kupitia mechi hizo mbili amejifunza mengi.

"Naamini katika kufanya kazi kwa bidii na nidhamu ndani na nje ya uwanja, sio tu kwa sababu nipo Simba nafanya hivyo tangu nimeanza kucheza soka, nisingependa basi ningechagua kazi nyingine ya kufanya," alisema Baleke aliyewahi kucheza TP Mazembe na kuongeza;

"Kwa sehemu nimeiona ligi ina ushindani mkali, kwangu nafurahia kwani muda mwingi  nitautumia kuhakikisha nafanya kazi kwa umakini na kuthamini nafasi nitakayopewa na kocha."

Wakati anajiunga na Simba alitokea klabu ya Nejmeh ya Lebanon pia aliichezea TP Mazembe na JS Kinshasa hizo mbili za DR Congo, jambo ambalo alisema amepata uzoefu wa namna ya kazi zake kuzifanya kwa ubora.

"Katika timu hizo zilikuwa na wachezaji wenye ushindani wa juu ambao utanisaidia kuuendeleza ndani ya timu yangu mpya, ambayo ina mastaa wenye uwezo mkubwa uwanjani na wapambanaji kwenye majukumu yao naamini nitamaliza msimu kwa kishindo," alisema.