Coastal vs Simba mechi ya kujuana

Dar es Salaam. Kocha wa Coastal Union, Yusuf Chipo amesema katika mchezo wao wa leo dhidi ya Simba anataka kufuta rekodi ya kufungwa na timu hiyo mara kwa mara na kurudisha ari ya ushindi kikosini.

Coastal Union na Simba zinashuka leo saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa CCM Mkwakwani, jijini Tanga, wakati wenyeji wakikosa rekodi nzuri mbele ya mabingwa mara 22 wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Huu unakuwa mchezo wa kwanza kwa kocha Juma Mgunda kurudi kwenye Uwanja wa Mkwakwani, tangu alipoondoka katika kikosi cha Coastal Union na kujiunga na Simba, Septemba 7, mwaka huu.

Hilo linaifanya mechi hiyo kuwa ya kipekee, kwani Mgunda anaijua vizuri Coastal Union kutokana na vijana wote aliowaacha kuwepo, wakati kocha msaidizi, Joseph Lazaro akizijua mbinu za bosi wake wa zamani.

Coastal haijawa na matokeo mazuri mbele ya Simba, kwani kwenye mechi zao nne zilizopita, imetoa suluhu moja na kufungwa mara nne.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu jana, Chipo alisema yeye si muumini wa kufuata historia, hivyo leo ni siku mpya kwao na wanataka kuhakikisha wanapata ushindi.

“Mimi si mtu wa historia, kwahiyo hayo yameshapita na sasa

tunaangalia ya leo, tunataka tupate matokeo mazuri ili turejee kwenye morali yetu, tumepoteza michezo mwili mfululizo (dhidi ya Azam FC na Dodoma Jiji),” alisema Chipo.

Akizungumzia mchezo wenyewe, kocha huyo raia wa Kenya alisema timu ambayo itafanya makosa lazima itaadhibiwa na kwa upande wake amezungumza na vijana wake kupunguza makosa ndani ya uwanja.

“Mechi ni ngumu sana na sisi hatuna matokeo mazuri, Simba ina matokeo mazuri, hivyo hapo ndiyo ugumu wa mchezo ulipo.

“Mechi zetu mbili zilizopita tulipoteza kwa sababu mwishoni tulikosa utulivu, lakini nilishazungumza na vijana wangu tutulie kwenye mchezo huuu,” alisema.

Kocha wa Simba, Juma Mgunda alisema anaiheshimu Coastal Union na amewataka wachezaji wake kuhakikisha wanazitumia vyema dakika 90 ambazo kila mmoja anahitaji matokeo ili kujiweka sehemu nzuri kwenye msimamo.

“Mimi kuwa kocha muda mrefu pale na kuwafahamu vizuri si sababu ya kwenda kuwadharau, cha msingi ni wachezaji wangu kuwaheshimu,” alisema Mgunda.

Katika mchezo mwingine wa leo, Dodoma Jiji itakuwa kwenye Uwanja wa Liti, Singida, kuikaribisha Ruvu Shooting.