Zitto: Tunakuja na siasa mpya

Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe (kushoto) akizungumza katika mahojiano na Mhariri wa siasa wa gazeti la Mwananchi, Salehe Mohamed, katika ofisi za chama hicho jijini Dar es Salaam. Picha na Sunday George

Muktasari:

  • Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema chama hicho kinawaletea Watanzania siasa mpya zitakazotoa majawabu kwa changamoto zinazowakabili katika maisha yao ya kila siku.

Dar es Salaam. Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema chama hicho kinawaletea Watanzania siasa mpya zitakazotoa majawabu kwa changamoto zinazowakabili katika maisha yao ya kila siku.

Zitto alibainisha hayo jana jijini Dar es Salaam katika mahojiano maalumu na Mwananchi kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo maandalizi ya ufunguzi wa mikutano ya hadhara ya chama hicho utakaofanyika Februari 19.

Alisema kupitia mikutano ya hadhara, chama hicho kinakwenda kuikosoa Serikali na kuja na majawabu katika masuala ambalo yanawasibu wananchi kama vile kupanda kwa gharama za maisha kulikosababishwa na kupaa kwa bei za bidhaa.

Kiongozi huyo wa chama alisema wana kawaida ya kufanya tafiti kuhusu hali ya maisha ya Watanzania na walibaini mambo matatu yanayowakabili kuwa ni kupanda kwa gharama za maisha, ukosefu wa ajira na umasikini.

“Tunawaletea Watanzania siasa mpya za kutoa majawabu ya changamoto zinazowakabili. Majawabu hayo tunayaita ‘ahadi zetu kwa Watanzania’, kwa hiyo tuna majawabu ya kupanda kwa gharama za maisha na kukosekana kwa ajira,” alisema Zitto.

Mwanasiasa huyo mashuhuri alisema baada ya kuzindua mikutano ya hadhara Februari 19 mkoani Dar es Salaam, wataendelea na mikutano hadi Machi 18 katika mikoa mingine ya Tanga, Unguja na Pemba huko Zanzibar, baadaye watapumzika kwa ajili ya mfungo wa Ramadhan kabla ya kuanza awamu ya pili.

Alisema wamejipanga kufanya mikutano ya hadhara na sababu ya kuanzia Dar es Salaam ni kwa kuwa ndiyo kitovu cha nchi hii na ndiyo chachu ya mageuzi hapa Tanzania. Alisisitiza kwamba wanataka mageuzi ambayo ni endelevu.

“Mabadiliko ya kisiasa yanaanzia eneo ambalo ni kubwa katika nchi, tunaanzia Dar es Salaam, hatuwezi kuikimbia Dar es Salaam. Tunataka mageuzi ambayo ni endelevu, ndiyo maana tunaanzia hapa,” alisema mwanasiasa huyo.

Zitto ambaye alikuwa mbunge wa Kigoma Mjini katika Bunge lililopita, alisema Watanzania waliikosa mikutano ya hadhara kwa miaka saba, hawawezi kuwaletea mambo yaleyale waliyokuwa wakiyasikia huko nyuma.

Aliongeza kwamba ACT Wazalendo ndiyo kilikuwa chama cha mwisho kufanya mkutano wa hadhara, Juni 5, 2016 katika Uwanja wa Zakhiem, Mbagala kabla Rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli hajatangaza marufuku ya mikutano hiyo.

“Tangu ACT Wazalendo imeanzishwa, chama hakikupata fursa ya kuwaonyesha wananchi siasa mpya, sasa fursa hiyo imepatikana. Tunakwenda kuwaonyesha siasa mpya za kuleta majawabu,” alisema.


SUK Zanzibar

Kiongozi huyo wa ACT Wazalendo alisema mawaziri wawili wanaotokana na chama hicho wanafanya vizuri kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) huko Zanzibar kwa sababu wamekuwa wabunifu katika wizara zao.

Alisema chama chake ndicho kilichopoteza watu wengi zaidi kuliko chama kingine chochote kwa sababu mashirika ya haki za binadamu yanabainisha kwamba kilipoteza takribani watu 19 katika uchaguzi wa mwaka 2020, hata hivyo hakikususa.

“Tunashirikiana na Serikali kuhakikisha kwamba tunapata fedha za kuendesha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,” alisema Zitto na kueleza kwamba changamoto zipo lakini wanakaa chini na kuzungumza. Alisisitiza kwamba kumekuwa na changamoto zinazojitokeza lakini wamekuwa wakizitatua kwa njia inayotakiwa kwa kuzungumza na viongozi wa Serikali wakiwaeleza kwamba hawawezi kuendelea kama walioumiza watu wakati wa uchaguzi hawatachukuliwa hatua.


Baraza Kivuli la Mawaziri

Katika mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwa Baraza la mawaziri kivuli wa ACT Wazalendo, Zitto alisema wamepata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kuanzisha utaratibu huo ambao ulizoeleka bungeni.

Pia, alisema chama hicho kimeibua wanasiasa wapya ambao wanakiendeleza chama hicho kutokana na vipaji vyao vya uongozi. Aliwataja baadhi yao kuwa ni pamoja na Emmanuel Mvula, Abdul Nondo, Elizabeth Sanga na Riziki Mngwali.

“Kwa ujumla tumefanikiwa kuibua masuala, mawaziri wetu vivuli wamekuwa wakizungumzia masuala mbalimbali yanayojitokeza na kutoa njia mbadala ili kutatua changamoto zinazojitokeza, hizo ndiyo siasa mpya ambazo tunazileta,” alisema mwanasiasa huyo.

Aliongeza kwamba wamefanikiwa kuwa na ofisi za Baraza la Mawaziri Kivuli pamoja na kuwapatia maofisa wa kuwasaidia kufanya tafiti juu ya masuala mbalimbali kabla ya kutoa taarifa kwa umma.