Zitto: Hizi ni sababu za kung’oka mwakani

Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe (kushoto) akizungumza katika mahojiano na Mhariri wa siasa wa gazeti la Mwananchi, Salehe Mohamed, katika ofisi za chama hicho jijini Dar es Salaam. Picha na Sunday George

Muktasari:

  • Hali ni tofauti kwa Zitto Kabwe, kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo ambaye kikatiba anamaliza muda wake Machi 2024, baada ya kukiongoza chama hicho kwa miaka 10 kama katiba ya chama hicho inavyomtaka.

Ni jambo la nadra kuona kiongozi mwasisi wa chama cha upinzani Tanzania aking’atuka katika uongozi baada ya kukitumikia chama kwa muda fulani, wengi huendelea kukaa madarakani na vyama vinakuwa kama mali yao.

Hali ni tofauti kwa Zitto Kabwe, kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo ambaye kikatiba anamaliza muda wake Machi 2024, baada ya kukiongoza chama hicho kwa miaka 10 kama katiba ya chama hicho inavyomtaka.

Zitto alijiunga na chama hicho mwaka 2014 akitokea Chadema, ambako alikuwa na mgogoro na viongozi na kusababisha kuvuliwa uanachama wa chama hicho. Aliingia ACT Tanzania kabla ya kubadilisha jina na kuwa ACT Wazalendo.

Kama mwanasiasa kijana, Zitto analeta somo jipya la demokrasia ndani ya vyama vya siasa ambavyo kwa kipindi kirefu vimekuwa havina demokrasia, viongozi wake wamekuwa wakijimilikisha vyama hivyo na wakati mwingine ukiangalia huoni mrithi aliyeandaliwa.

Jambo hilo limekuwa likitoa taswira hasi kwa baadhi ya vyama vya upinzani ambavyo vinalilia demokrasia ya nje, lakini ndani yao hakuna nafasi hiyo na vingine hukiuka kabisa katiba zake.

Katika mahojiano maalumu na Zitto aliyofanya na Mwananchi wiki hii, anaeleza namna chama chake kinavyowaletea Watanzania siasa mpya, ikiwemo kuibua sura mpya za wanasiasa ambazo zitaendeleza gurudumu baada yake.

Anasema kupitia baraza kivuli aliloliunda, wameibua vijana mahiri katika uongozi ambao walikuwa hawafahamiki, jambo ambalo anajivunia kuandaa kizazi ambacho kitaendeleza siasa baada ya kumaliza muda wake.

Zitto anasema kiongozi yeyote ambaye hatengenezi mrithi wake, basi huyo ni kiongozi ambaye amefeli. Anasema tayari chama chake kimetengeneza vijana wengi wenye uwezo wa kuongozi hata yeye asipokuwepo.

“Muda wangu wa uongozi unakwisha Machi 30, 2024. Kama hatujengi watu wa kutosha, nani atakuja kuwa kiongozi? Lakini kwa sababu Watanzania wamezoea ukiwa kiongozi wa chama cha upinzani, wewe ni wa kudumu, hilo ni jambo la ajabu sana.

“Mimi kama kiongozi ninasema hapana, nimetumia muda wangu kwa mujibu wa katiba yetu, wa miaka 10 na actually (hakika) nimerudisha nyuma kwa sababu ilikuwa nimalize mwaka 2025, nimesema hapana, hatuwezi kubadilisha uongozi mwaka wa uchaguzi, turudi nyuma tufanye mwaka 2024,” anasema.

Alisema Machi 2024, watakuwa na kiongozi mwingine wa ACT Wazalendo na kwamba jopo la viongozi kivuli linawapa machaguo ya kwenda kusema fulani anafaa, na hilo analiona kuwa la muhimu zaidi kwenye siasa.

Zitto anabainisha kwamba amekuwa akijizuia kusema ili kuwapa nafasi viongozi wengine kusema kupitia wizara wanazozisimamia katika baraza kivuli la chama hicho. Anasema kupitia hilo, viongozi wengine wanajulikana na kupata ujasiri wa kufanya siasa.

“Tuna watu ambao wana uwezo mkubwa. Ukiangalia reaction ya wanasiasa kwenye suala la Loliondo, ukilinganisha na wanasiasa wa vyama vingine na siasa ambayo Bonifasia Mapunda aliifanya kwenye suala la Loliondo, unaona tofauti kwa sababu sisi kuna vijana wanafanya utafiti na kulifahamu jambo,” anasema kiongozi huyo.

Mwanasiasa huyo ambaye alikuwa mbunge wa Kigoma Mjini, anawataka wanahabari kuwapa nafasi viongozi wao ili waweze kutetea masilahi ya Taifa kupitia baraza kivuli ambalo limeundwa na ACT kuziba pengo la kukosekana kwa baraza kivuli bungeni.

Likiwepo la kusema nitasema
Zitto alikuwa mkosoaji mkubwa wa Rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli na kila lilipotokea jambo hakusita kujitokeza na kukemea vikali jambo hilo hadharani na kuitaka Serikali kuchukua hatua.

Baada ya Rais Samia kuingia madarakani, Zitto amepunguza ukosoaji kama alivyokuwa huko nyuma, jambo ambalo limekuwa likiibua mjadala kwenye mitandao ya kijamii ambapo watu wamekuwa na mapokeo tofauti.

Hata hivyo, yeye anaeleza kwamba kama kuna jambo lolote lenye masilahi mapana kwa umma, lazima aingie. Anasema pale panapohitajika kusema atasema kama kiongozi wa ACT Wazalendo.

“Moja ya mambo ambayo nilikuwa kinara wakati wa utawala wa Magufuli ilikuwa ni kutetea watu, watu wanaotekwa. Ndiyo maana mlisikia namzungumzia Ben Saanane, Simon Kanguye, Erick Kabendera nje na ndani ya Bunge.

“Sasa, mnataka niseme vile, nionyeshe nani katekwa, sema fulani ametekwa hukusema, biashara fulani imevunjwa hukusema, mwandishi wa habari fulani amekamatwa hukusema. Kila msimu una shughuli zake.

“Msimu wa kushangilia, wewe ukizomea, watu watakuona juha. Msimu wa kushangilia, wewe ukizomea watu watakuona zwazwa. Msimu wa Rais Magufuli ulikuwa ni msimu wa kuhami demokrasia, angalau zibakie sauti chache za kupigania demokrasia,” anasema Zitto.

Anaongeza kwamba msimu wa Rais Samia ni msimu wa kusimamia mageuzi yanayotakiwa katika nchi ili angalau nchi irudi katika mazingira yaliyokuwepo kabla ya mwaka 2015. Alisisitiza kwamba misimu hiyo miwili ni tofauti.


Bima ya afya
Akizungumzia mapendekezo ya chama chake kuhusu suala la bima ya afya kwa wote, Zitto alishauri kufungamanishwa mifuko ya hifadhi ya jamii na bima ya afya ili iwe kama mafao ndani ya mifuko hiyo.

Zitto alitoa kauli hiyo ikiwa ni siku moja kabla ya kuanza kwa vikao vya Bunge vilivyoanza jana jijini Dodoma, ambapo miongoni mwa miswada itakayowasilishwa ni pamoja na ule wa bima ya afya kwa wote.

Serikali itaurejesha bungeni muswada huo na kusomwa mara ya pili, baada ya kuwa imeuondoa mwaka 2022 uliposomwa kwa mara ya kwanza, kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni kukosekana kwa chanzo halisi cha mapato ya kuwezesha kutoa huduma hizo kwa wote.

Akizungumza katika mahojiano hayo ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Zitto anatoa mapendekezo ambayo yatasaidia kukuza mfuko wa bima ya afya ili usaidie Watanzania wote.

Anasema katika Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kuna fao la matibabu ambalo halitumiki tangu mwaka 2019 kutokana na Serikali kuliondoa, huku wanufaika wake wakibaki waliojiunga na mfuko huo kuanzia mwaka 2018 kurudi nyuma.

Zitto anasema fao la matibabu lipo kisheria na bodi ya NSSF haina mamlaka ya kulizuia, hivyo haina budi kuliachia litumike.

“Watu wanaochangia fao la matibabu na NSSF wako milioni moja na nusu, sawa asilimia 20 ya makusanyo yote ambayo mfuko huo unakusanya, hivyo yachukue na kuyapeleka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

“Kwa hatua hiyo peke yake, ndani ya mwaka mmoja kiwango cha fedha ambacho NHIF itakipata kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na NSSF kwa idadi ya walioko sasa ni zaidi ya Sh530 milioni ambayo ni asilimia 20 ya michango yote na hili ni jambo ambalo limefanyiwa mahesabu na watu wa bima,” alieleza Zitto.

Katika hatua nyingine, mwanasiasa huyo amesema kwa watu ambao wamejiajiri kwa shughuli mbalimbali, wakiwamo wamachinga na wakulima wanaweza kuingiza kipato cha juu kuzidi hata walioajiriwa, lakini hakuna kivutio chochote cha kuwafanya wajiunge na mifuko ya hifadhi ya jamii.

Hivyo, ameshauri Serikali ione namna ya kuwashawishi watu wa aina hiyo kujiunga katika mifuko hiyo.

Vilevile, Zitto amegusia suala la Watanzania wa kipato cha chini ambao wengine wapo chini ya Mpango wa Kusaidia Kaya Maskini (Tasaf), akishauri walipiwe mafao katika mifuko ya hifadhi ya jamii.

“Badala ya kuendelea kuwapa tokeni kwa mwezi ni bora walipiwe