Upinzani hustawi baada ya minyukano CCM

Wafuasi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wakifurahia jambo kwenye moja ya mikutano ya kampeni za uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020. Picha na mkataba

Naikumbuka Julai 13, 2011. Mfanyabiashara na kada wa CCM, Rostam Aziz alitokeza kwenye uso wa vyombo vya habari, akitangaza uamuzi uliogubikwa na hasira. Alijiuzulu ubunge na vyeo vyote ndani ya chama, ikiwemo ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec).

Hasira za Rostam hazikuwa mafichoni. Lugha ya mwili jumlisha maneno kichwani ni jawabu la kuchushwa na kilichokuwa kikiendelea ndani ya CCM. Hususan kumhusu yeye. Alihusishwa na vitendo vya ufisadi. Alituhumiwa kwa anguko la CCM hasa majimboni.

Ilikuwa haijafika hata miezi tisa tangu Uchaguzi Mkuu 2010. Matokeo ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 30, 2010, yalionesha kuwa urais CCM walipata asilimia 63.8 ya kura zilizopigwa, kutoka asilimia 80.2 mwaka 2005. Wabunge CCM walishinda majimbo 186 (2010) kutoka 206 (2005).

Kupungua kwa kura za CCM 2010, kuna athari za kabla na baada. Matokeo ya kuvunjika Baraza la Mawaziri Februari 2008 na falsafa ya “Kujivua Gamba”, iliyoibuliwa na Kamati Kuu CCM. Rostam alikuwa mwathirika wa siasa za 2008, vilevile lawama za baada ya Uchaguzi Mkuu 2010.

Kujivua gamba

Kujivua gamba ni nini? Kwamba kuna wana CCM waliokuwa wakishutumiwa kwa vitendo vya ufisadi. CCM walitaka wajisafishe mithili ya nyoka anavyovua gamba na kurudi ujana. CCM kupitia falsafa ya Kujivua Gamba, walilenga kuwa wapya. Wajitenge na makada wao wenye makandokando.

Rostam alizungumzwa, Waziri Mkuu wa nane, Edward Lowassa, alisemwa. Tena Rostam na Lowassa walikuwa mithili ya mapacha wawili, jinsi walivyozungumzwa. Rostam alipokuwa anatangaza kujiuzulu, alisema alichoshwa na siasa za majitaka. Akajitoa.

Muhtasari kuhusu Rostam na matokeo ya Uchaguzi Mkuu 2010, unatuleta kwenye mjadala kuwa CCM hawajawahi kubomolewa na upinzani, isipokuwa visa vya wao wenyewe ndani kwa ndani. Kasi ya kuwania madaraka huchukua sehemu kubwa.

Mwaka 2005, CCM waliingia kwenye uchaguzi imara kwa sababu hakukuwa na makundi. Kundi lililokuwepo ni moja, likiitwa “Mtandao”. Naam, ndio mtandao uliomuingiza madarakani Rais wa Nne, Jakaya Kikwete.

Wapo wanasiasa walioumizwa na kujeruhiwa kisiasa kutokana na rafu za Mtandao. Waziri Mkuu wa Nne na Katibu Mkuu wa uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), Salim Ahmed Salim, alidhalilishwa na kupoteza kabisa hamu ya kufanya siasa.

Salim aliwahi kusema kuwa aligundua kwamba kugombea urais Tanzania ni njia mojawapo ya kujivunjia heshima. Kwa majina aliyopewa, nafasi aliyowekwa, Salim alijiona kupoteza heshima yake aliyoijenga ndani ya taifa na jumuiya za kimataifa.

Siasa za kuchafuana

Siasa za CCM ni za kuchafuana kuliko kuibuka na hoja au kujenga haiba yenye kuvutia wananchi. Bahati mbaya zaidi, imegeuka kuwa mwendo rasmi wa siasa za nchi. Ukitaka kukubalika CCM, unatafuta washindani wako. Unatengeneza kashfa za kuwachafua.

Waziri Mkuu wa Sita, John Malecela na wa Saba, Fredrick Sumaye, kwa pamoja walikuwa na simulizi yenye kuumiza kuelekea Uchaguzi Mkuu 2005. Hata hivyo, bahati kwa CCM ni kuwa Salim, Sumaye na Malecela hawakuwa na makundi imara yenye nongwa.

Laiti Salim angekuwa na kundi, hali isingekuwa salama mwaka 2005. Vivyo hivyo kwa Sumaye na Malecela. Kutoka mwaka 2005 hadi sasa, uanzishaji makundi imekuwa hulka sugu ndani ya CCM. Athari kubwa ilionekana mwaka 2010 na 2015.

Kundi la Mtandao lilianza mwaka 1995. Lilimsumbua aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM, Rais wa Pili, Ali Hassan Mwinyi. Likamtikisa mwana CCM aliyekuwa na kadi namba moja, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Kwa Mwalimu aliweza kuwadhibiti.

Mwanzilishi wa Mtandao alikuwa Lowassa. Aliposhirikiana na Spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta, kumshawishi Rais wa Nne, Jakaya Kikwete, kuwa timu moja kuelekea Uchaguzi Mkuu 1995. Upacha wa Kikwete na Lowassa ukaundwa.

Hata baada ya Lowassa kukatwa jina kwenye Kamati Kuu CCM mwaka 1995, hali haikuwa rahisi kutokana na uwekezaji wa Lowassa. Mwalimu Nyerere alilazimika kutoka mbele ya vyombo vya habari na kutetea uamuzi wa Kamati Kuu.

Kikwete aliposhindwa na Rais wa Tatu, Benjamin Mkapa, kulikuwa na sauti za vijana, walewale waliofanya fujo Lowassa alipokatwa, safari hiyo walimtaka Kikwete asikubali matokeo na atangaze kuhamia upinzani.

Ndio sababu, Kikwete alipokuwa anataka kuongea ndani ya Mkutano Mkuu CCM, aliyekuwa Katibu Mkuu, Lawrence Gama, alikataa kumpa ‘maikrofoni’. Mwalimu Nyerere alipoona hitaji la Kikwete kuongea, akaagiza apewe nafasi.

Kisha, Kikwete akawashangaza wengi alipotangaza kumuunga mkono Mkapa na kuagiza timu yake ijielekeze kwa mgombea aliyeshinda. Ikawa furaha kwa Mwalimu Nyerere, Mwinyi mpaka mgombea mwenyewe, Mkapa.

Kumbe sasa, kama si uimara wa Mwalimu Nyerere na busara za Kikwete kukubali kushindwa, pengine mgawanyiko CCM ungekuwa mkubwa. Vivyo hivyo, endapo Salim, Malecela na Sumaye wangeunda makundi kuelekea Uchaguzi Mkuu 2005, chama kingeenda kwenye uchaguzi kikiwa vipande.

CCM na kikulacho

Historia inaonyesha kuwa methali ya “kikulacho kinguoni mwako”, ndio mtihani mkubwa CCM. Sasa hivi tayari majina yanapenya hadi mitandaoni. Mara Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa hatakiwi, anayetakiwa ni January Makamba.

Mbunge wa zamani wa Arusha Mjini, Godbless Lema, aliandika hivi karibuni kwenye akaunti yake ya Twitter kuwa anazo taarifa za ndani kwamba George Simbachawene ndiye Waziri Mkuu anayefuata baada ya Majaliwa.

Kwa akili ya kawaida unajiuliza, nani anaweza kuvujisha hizi taarifa? Ukimfikiria Rais Samia Suluhu Hassan, utapindisha shingo kukataa. Majaliwa hawezi kujitengenezea nuksi. January na Simbachawene, wanawezaje kuvujisha habari zao kabla ya wakati?

Ukifika hapo, utagundua kwamba haihitaji elimu kubwa ya intelijensia kubaini uwepo wa watu wenye lengo la kumchonganisha Majaliwa na bosi wake, Rais Samia. Majaliwa amtazame Rais Samia kwa jicho la chuki, kuwa hamwamini.

Historia ni mwalimu. Kikwete akiwa Rais na Lowassa Waziri Mkuu, mgogoro wao ulitengenezwa kwa namna iliyowaacha wao wenyewe wakiwa hawaaminiani. Kikwete hakumwamini Lowassa, vivyo hivyo kwa mwenzake. Mwisho, ukaibuka uadui mkubwa wa kisiasa.

Uchonganishi kuhusu Majaliwa na nafasi ya Uwaziri Mkuu, bila shaka, unakusudia kumfanya apoteze imani na wasaidizi wake ambao ni January na Simbachawene. Ajione yupo katikati ya uadui, kwa bosi wake mpaka wasaidizi chini yake.

Lowassa alipokuwa anajiuzulu uwaziri mkuu, alisema kulikuwa na matamanio ambayo yeye aliamua kwenda kuyatimiza. Akasema ni “uwaziri mkuu”. Ilikuwa wakati wa kashfa ya Richmond.

Lowassa alitaka Watanzania wajue kwamba mengi yaliyotendeka ni matamanio ya watu kuona anaachia kiti cha Waziri Mkuu.

Hata sasa, Majaliwa anaweza kuona nafasi yake inatolewa macho sana na kuna watu matamanio yao ni kuona anang’oka. Atamtazama vibaya Rais Samia, hatawaangalia kwa macho ya wema, January na Simbachawene.

Endapo Majaliwa atapata wakati mzuri wa kutafakari, anayetengeneza maneno ndiye mwenye masilahi na cheo chake. Si Samia wala January na Simbachawene. Daima, mchonganishi hujenga fitina akiwa analenga matokeo yenye sura ya mgogoro.

Mnyukano ndani ya CCM

Swali, nani anaweza kuwa na masilahi na uwaziri mkuu wa Majaliwa kwa sasa? Jibu ni moja tu, ni wao wenyewe CCM ndani kwa ndani.

Yupi anakusudia kuona mgawangiko kwenye Serikali ya Samia? Jawabu ni lilelile, CCM wao kwa wao.

Majaliwa aking’oka, atakayepata ni mbunge wa kuchaguliwa kutoka CCM. Hakuna mpinzani mwenye masilahi binafsi na Majaliwa kutenguliwa uwaziri mkuu.

Ukitokea mvurugano wa ndani kwa ndani kwenye Serikali ya Samia, watanufaika wabunge CCM, ikiwa kuna mawaziri wataondolewa, nafasi zitajazwa miongoni mwa wabunge. Na karibu wote ni CCM.

Hivi sasa unaweza kustaajabu January anashambuliwa kuwa ni Waziri wa hovyo. Kisa umeme unakatika. Unajiuliza swali, tangu lini Tanzania ilijihakikishia umeme wa uhakika usiokatika?

Mbona kelele za sasa ni nyingi kuwahi kutokea? Kumbe ni mwangwi ndani ya CCM.

January alisemwa kuwa anahujumu kukamilika kwa mradi wa Bwawa la Kuzalisha Umeme la Julius Nyerere (JNHPP). Kisha tukashuhudia tukio la kuruhusu maji kuingia ndani ili kuanza rasmi kazi ya kufua umeme.

Februari 2022, January alielezea kuwa tatizo la umeme ni miundombinu, hivyo inahitaji muda kuirekebisha. Alieleza changamoto ya nyaya zenye uwezo wa msongo mdogo wa umeme kubeba msongo mkubwa mpaka transfoma yenye uwezo wa kuhudumia nyumba 50 kubebeshwa nyumba zaidi ya 100.

Ukifuatilia jinsi January anavyoshughulikiwa, unapata jibu la mapambano ya wao kwa wao. Atoke January aingie mwingine. Na mara nyingi mapambano ndani ya CCM huwa hayabebi masuala kuhusu wananchi. Ni migogoro ya vyeo.

Mikutano ya hadhara

Kipindi hiki imetolewa ruhusa ya mikutano ya kisiasa. Endapo CCM watapitia kipindi kigumu, yupo mtu anaweza kusingizia ruhusa ya mikutano. Ukweli haupo hivyo.

Vyama na nguvu ya upinzani hutumika kama maficho ya ukweli, maana upinzani haujawahi kuibomoa CCM, bali vita ya ndani.

CCM wangekomesha kwanza makundi na michuano ya urais isiyo na tija. Wamwache Rais, Waziri Mkuu na timu ya mawaziri ifanye kazi. Bunge lifanye kazi ya usimamizi. Vyama vya upinzani vifanye ukosoaji.

Miaka nenda rudi, migogoro ya CCM ndio huwapa agenda wapinzani. Ufisadi lilitoka CCM na kubebwa na wapinzani.

Kama tamaa za urais ndani ya CCM na makundi ya vyeo, vitazidi nguvu za chama na Serikali, upinzani utastawi. CCM itafika 2025 ikiwa vipande.