Chongolo awashukia viongozi migogoro ya ardhi vijijini

Muktasari:

  • Chongolo  amesema hayo leo Jumapili Januari 29, 2023 wakati akizungumza na wananchi na wanachama wa CCM wa kata ya Dakawa wilayani Mvomero katika siku ya pili ya ziara yake ya siku tisa mkoani Morogoro alioianza jana Januari 28, 2023.

Dar es Salaam. Katibu mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo amesema baadhi ya viongozi nchini ni chanzo cha migogoro ya ardhi kwenye vijiji na kata mbalimbali.
Amesema kati ya migogoro hiyo ni kipindi cha kuelekea chaguzi, baadhi ya viongozi kuongeza eneo la kitongoji kingine katika eneo lake  kwa maslahi yake binafsi jambo linalosababisha kero kwa wananchi.
Chongolo  amesema hayo leo Jumapili Januari 29, 2023 wakati akizungumza na wananchi na wanachama wa CCM wa kata ya Dakawa wilayani Mvomero katika siku ya pili ya ziara yake ya siku tisa mkoani Morogoro alioianza jana Januari 28, 2023.
" Mara nyingine inakuwa maslahi ya maeneo, unakuta eneo fulani limejaa basi wanakata maeneo ya wengine ili kuhamia huko. Sababu nyingine ni tamaa ya mashamba au kuuza maeneo, malisho na kulima," amesema Chongolo.
Ziara hiyo inalenga kuimarisha na kukagua uhai wa chama hicho pamoja  na kusikiliza kero za wananchi wa wilaya mbalimbali za mkoa wa Morogoro
Akiwa ameambatana na katibu wa itikadi na uenezi, Sophia Mjema na katibu wa oganaizesheni, Issa Haji Ussi ' Gavu' Chongolo amesema, ‘’sisi viongozi ndio tuna jukumu la kutatua changamoto, tukinyooka na kusimamia sheria za nchi ambazo zipo wazi  hakuna kijiji kisicho na mpaka ambacho  kimeanishwa. Ukiona kuna ugomvi kati ya kijiji na kijiji basi viongozi wa eneo hilo hawajanyooka.’’
" Nimeona nianze na hili kwa sababu Mvomero ni maarufu kwa migogoro ya ardhi, lazima tuamue kwa dhati ya mioyo yetu kwamba tunakwenda kutatua changamoto  za mipaka kati ya maeneo na maeneo ambazo hazina haja ya kulelewa kwa muda mrefu."

Chongolo alieleza hayo baada ya mbunge wa Mvomero, Jonas Van Zeeland  kumweleza katibu mkuu huyo changamoto mbalimbali zinazolikabili jimbo hilo zikiwemo za migogoro ya mipaka ya wakulima na wafugaji.