Chadema yatoa msimamo chaguzi zijazo


Wawakilishi wa Baraza la Wazee wa Chadema (Bazecha) Mkoa wa Mara wakimkabidhi zawadi ya mbuzi Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika leo Jumapili Januari 22, 2023 katika Viwanja vya shule ya Msingi Mukendo mjini Musoma.

Picha na Peter Saramba

Muktasari:

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesisitiza bila katiba mpya na tume huru ya uchaguzi basi hakutakuwepo na uchaguzi mkuu nchini.


Musoma. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesisitiza bila katiba mpya na tume huru ya uchaguzi basi hakutakuwepo na uchaguzi mkuu nchini.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara mjini Musoma leo Jumapili, Januari 22, 2023, Naibu katibu mkuu wa Chadema bara, Benson Kigaila amesema msimamo huo tayari ulishatolewa na chama chake pamoja na magumu waliyopitia katika kipindi cha miaka saba iliyopita msimamo huo haujabadilika.

"Serikali ya CCM inapoendelea kuvuta miguu juu ya suala la katiba mpya sisi tunaendelea kupiga mstari pale pale tulipokwisha uchora ni kwamba bila katiba mpya na tume huru ya uchaguzi, uchaguzi hautafanyika huo ndio msimamo wetu," amesema

Amesema katiba mpya ni hataji la Watanzania hivyo hakuna sababu ya Serikali kupuuzia hitaji hilo badala yake inatakiwa kutekelezwa kwa maslahi ya Watanzania na nchi kwa ujumla.

"Moto haufichwi kwenye shuka pamoja na kifungo cha miaka saba lakini leo mmekuja hapa mkidai na kuitaka katiba mpya hivyo ni lazima ipatikane kwani bado hamjachoka na hamtochoka kuidai," amesema

Naye katibu mkuu wa chama hicho, John Mnyika amesema endapo kungekuwa na katiba mpya inayodaiwa na wananchi basi leo wananchi wangekuwa na uwezo wa kuwawajibisha wabunge wengi ambao amedai wameingia bungeni kwa njia zisizokuwa halali.

"Katiba ya Jaji Warioba imetamka wazi wananchi wanataka wawe na uwezo wa kuwawajibisha wabunge wasiowajibika na kama hiyo katiba ingekuwa inatumika basi hadi sasa tungekuwa tumewawajibisha wale wabunge walioingia bungeni kimagumashi," amesema.