NDANI YA BOKSI: Namuwaza Zuchu katika mikono ya Ruge

Zuchu

Muktasari:

Mwanamuziki ili utoboe lazima uwe na vitu vinne sahihi. Ambavyo havina ‘eksichuzi’ kwenye sanaa yako kwa dunia ya sasa. Dunia hii ya intaneti siyo ile ya Issa Matona wala Hemed Maneti. Ipo kasi kuliko kimondo.

Mwanamuziki ili utoboe lazima uwe na vitu vinne sahihi. Ambavyo havina ‘eksichuzi’ kwenye sanaa yako kwa dunia ya sasa. Dunia hii ya intaneti siyo ile ya Issa Matona wala Hemed Maneti. Ipo kasi kuliko kimondo.

Kuwa na kipaji ndio jambo la msingi kabisa kwenye sanaa. Kukiendeleza ni suala mtambuka. Na usimamizi wa watu sahihi zaidi ni jambo la bahati nasibu. Kwa maana ya usimamizi wa kuona fursa ndani ya kipaji chako. Na nyota. Yes!

Kuna watu wapo kwa ajili ya kukupa moyo kwenye maisha ya kipaji. Wao watakusifia kuwa unaweza. Wewe ni mkali sana na kwenye ‘gemu’ lazima utoboe. Alikiba kitu gani, hakuwezi hata kidogo. Kila aina ya maneno ya faraja watakupa na wewe kama boya utavimba bichwa.

Hao huishia kukusifia kwenye vikao vya baa au popote. Watakutupia bia mbili tatu ili uwaburudishe kidogo na ‘akapela’ kadhaa. Nao kama majuha watajisifu kufahamiana na kila mdau wa sanaa. Kama msanii mwenyewe ni pisi kali wataenda ‘fronti’ zaidi.

Tantalila nyingi na mwisho wa siku hata kama hana mvuto au ni mdogo kwa umri. Akili yake ya pombe itafanya amuone ni Beyonce flani hivi amazing. Amuone mtu mzima mwenzake na kushea shuka za ‘gesti’.

Hawana mwendelezo wa kumsaidia zaidi baada ya hapo. Msanii ataishia kuwa kicheche chake na kuongeza ‘data bezi’ ya mademu waliomegwa na huyo bwege. Wanaokutana na haya maswahibu ni wengi. Usione tu mtu kawa staa. Mapito ni magumu sana.

Tena haohao ndio huwatia ndimu kina Anjela, Ibrah na wenzao, kuwa wanatumiwa kijanja huku wao wakifa maskini na vipaji vyao. Kwa mpuuzi atawasikiliza na kuachana na watu sahihi. Kisha anaenda kujifia na kipaji chake.

Kama hukumjua kabla Jay Melody. Hukumuona kabla Mbosso na wale wenzake. Unasemaje anatumika na wajanja leo hii? Baada ya kumuona runingani na jukwaani? Kafikaje alipo mpaka ukamuona na kuleta ngonjera zako za anatumiwa?

Msanii inakuwaje ukubali maneno ya shabiki kuwa unatumiwa. Ambaye kakuona baada ya uwekezaji wa akili za watu wengine katika kipaji chako? Na wewe unaamini maneno yake na kuona mtu sahihi kwako? Kikwete alisema akili za kuambiwa?

Sasa kuna wanaomsikiliza msanii. Wanagundua ana kipaji na namna gani watamtumia ili kipaji chake kigeuke kuwa mfereji wa pesa. Msanii apate na muwezeshaji afaidike. Hao watu wana vitanda vyao tayari kule peponi.

Huwakuti baa wakisifia msanii na kumnunulia bia. Wakijinadi kujuana na wadau wa sanaa wala viongozi. Majina yao utayasikia kwa wasanii husika huko baa. Wakiwaongelea kwa mema sawa na mabaya yao. Hawa ndio watu sahihi.

Kina Lady Jaydee walikuwa na vipaji kabla. Lakini pesa zilijenga urafiki na akaunti zao baada ya kuonyeshwa njia na watu wa aina hii. Ndivyo ilivyo kwa Ray C, Q Chilla, Nature, Linnah, Mwasiti, Marlaw. Baadaye kina Ruby, Nandy, Maua Sama na wengineo.

Mwana FA hakukaa na kujisifu kabla ya kumuonyesha njia Maua Sama. P Funk hakutaka sifa ili kumtoa Juma Nature. Ndivyo kwa G Lover (Guru), alikiona kitu ndani ya Mr Blue kisha akamuonyesha njia sahihi na kutoka.

Jide na Ray C, walikuwa watangazaji kabla ya kujikita jumla kimuziki. Kuna wanamuziki wa kike hawakupitia njia hiyo ambao ndiyo wengi kwa sasa.

Lakini nao pia walishikwa mkono na watu waliona kitu ndani yao. Na sasa wanakula matunda ya vipaji vyao. Yes!

Wengi hawajui kama Afande Sele ni Sugu ndiye aliyeona kitu ndani yake na kumshika mkono. Dunia ya muziki wetu haikumjua Afande Sele kabla ya Sugu kumleta kwetu. Kama ambavyo na Sele alikiona kitu kwa Dogo Ditto na kumshika mkono.

Kuna wanamuziki wengi sana ambao wameshiriki kuinua wanamuziki, akiwamo Dully Sykes, ambaye kwa kiasi kikubwa alikuwa taa kwa vijana wa Kariakoo na Ilala. Hakuna staa wa Ilala asiyetambua nguvu ya Dully. Waulize wote.

Kuna Juma Nature, mpaka kesho anaendelea kuwa daraja la masela kibao. Na siyo kwa masela wa Temeke tu, hata Chegge kutoka Kigoma huko alishikwa mkono na Nature. Ndivyo ilivyo kwa Domokaya na Mandojo kuna mkono wa Kibra.

Na katika watu ambao siyo wasanii lakini wameibua na kuwajenga sana wanamuziki. Ni Kim Magomelo (marehemu) na ‘Yo Rap Bonanza’, Dj G Lover, Said Fella, Abdul Bonge (marehemu), Dj Bon Lov na Ruge Mutahaba (marehemu). Wapo kibao tu.

Msisitizo. Kuwa na kipaji ndio jambo la msingi kisanaa. Kukiendeleza ni suala mtambuka. Usimamizi na watu sahihi ni bahati nasibu sana. Kwa maana ya usimamizi wa kuona fursa ndani ya kipaji chako. Usisahau kuna nyota kali kwa msanii husika. Mtazame Zuchu, mwanamuziki wa kike mwenye vitu vyote vinne. Kipaji, kukiendeleza, usimamizi na nyota. Wapo wenye vipaji sana lakini nyota inakosekana. Tunaishia kuwasifia tu kuwa huyu ana kipaji lakini hatanuki kisanii. Salamu kwa Grace Matata. Zuchu ni msanii asiye na miaka hata mitano toka aanze kutamba. Lakini leo hii akitoa ngoma hata baba yake wa muziki Mondi anakaa. Kalamba sana mchanga hapa kati. EP yake ni ngoma aliyofanya na Zuchu pekee ndio ilikimbiza zaidi.

Baada ya WCB kutamba sana na dude la Harmonize ‘Kwangwaru’. Hapo kati hakuna ngoma iliyovuka mstari wa lile ting’a mpaka alipokuja Mtoto wa Bububu kutoka kwa Bibi Paje na bomu la ‘Sukari’. Dai na machalii wake wote waliloa.

Nje ya ‘Kwangwaru’ na ‘Sukari’, hakuna pini lingine lililoshika akili za Taifa hili. Zuchu ‘kosistensi’ yake ni safi kama theluji ya Mlima Kilimanjaro. Hata ile ‘Mwambieni’ pia ni ngoma iliyozima data za watu mjini. Binti ana vitu vile vinne kamili vya mwanamuziki wa sasa. Ingawa nakiri wazi kwamba Zuchu, ana kipaji kikubwa na kukiendeleza vyema.

Ana wasimamizi wazuri sana na zaidi ana nyota yake kali. Lakini nimekuwa nikiwaza mara kwa mara kwamba hiki kipaji cha binti huyu wa Kizenji, kingekutana na akili za Ruge. Aiseeee!!!

Alamsik bin Noor....