Wanachotaka waajiri kutoka vyuoni, wahitimu

Muktasari:

  • Katika kukabiliana na ukosefu wa ujuzi unaotakiwa kwa wahitimu , wadau katika soko la ajira wamevitaka vyuo vikuu, kuandaa watalaam katika mtindo utakaowawezesha kuonyesha thamani yao kwenye soko.

Katika kukabiliana na ukosefu wa ujuzi unaotakiwa kwa wahitimu , wadau katika soko la ajira wamevitaka vyuo vikuu, kuandaa watalaam katika mtindo utakaowawezesha kuonyesha thamani yao kwenye soko.

Wadau wengi wamekuwa wakipendekeza ushirikiano wa karibu kati ya taasisi za elimu ya juu na viwanda au waajiri, ili kukabiliana na tatizo la uwezo na kushirikiana kuwatengenezea wahitimu ujuzi, ambao unahitajika katika soko la ajira.

Katika kuhitimisha maadhimisho ya miaka 60 tangu kuanzishwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), chuo hicho kilikutanisha wadau mbalimbali kujadili taasisi hiyo katika maendeleo ya Taifa na mwelekeo wa siku zijazo na suala zima la ajira.

Kongamano hili la wadau ni la mwisho tangu kuanza kwa maadhimisho hayo ya miaka 60, yaliyoanza kuadhimishwa Oktoba mwaka jana.

Hatua hiyo imekuja kipindi ambacho kumekuwa na malalamiko kutoka kwa waajiri kuhusu wahitimu kushindwa kufanya kazi kwa vitendo, jambo ambalo limekuwa likiziweka taasisi hizo kwenye darubini.

Walichosema waajiri

Ili kukabiliana na changamoto hiyo, wadau hao wanavishauri vyuo vikuu vyote kujenga utamaduni wa kuwatembelea waajiri na kuweka mikakati ya kubadilishana uzoefu wa namna bora ya kukabiliana na hali hiyo.

“Tungependa vyuo vikuu vije kuona kazi tunazofanya na aina ya wafanyakazi tunaowahitaji, pia tutaweza kupokea wahadhiri kwa muda kabla hawajaenda kufundisha wanafunzi ambao tutahitaji kuwaajiri baadaye,” anasema Simon Shayo ambaye ni Makamu Rais wa mgodi wa dhahabu wa Geita (GGML).

Hilo lilielezwa pia na Mkurugenzi wa sera, utetezi na utawala wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF)Zaky Mbena, akitaka chuo hicho kije na mkakati wa kuwapa wanafunzi maarifa ya kimsingi ya Tehama, ambayo ni ya lazima kwa wahitimu wa sasa katika dunia inayobadilika.

“Kinachowapunguzia wahitimu wetu wengi na kinachokwamisha nafasi zao za kuajiriwa ni kushindwa kuonesha ‘mtazamo sahihi’ na ‘stadi laini’ ambao ndio tunaangalia sana kabla ya kuajiri.Tatizo kubwa ni wahitimu wengi kukosa mtazamo sahihi, tunatakiwa kuangalia namna silabasi na programu zetu zinavyoweza kuangalia eneo hili ambalo kwa sasa ni kikwazo kwa waajiri.

‘’Tunatakiwa kuanzisha ushirikiano wa kimkakati kati ya sekta binafsi (viwanda) na wasomi. TPSF na UDSM waungane na kujenga jukwaa la kuimarisha ushirikiano wa kudumu ili kwa pamoja tusaidie kizazi hiki na kijacho,” anasema Mbena.

Anasema kuwa vijana wengi wamekuwa wakikosa ujuzi wa kuingiliana katika mazingira na mfumo rasmi wa ushirika, jambo ambalo linawafanya waonekane hawafai licha ya kuwa na sifa stahiki.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Hifadhi ya Jamii Afrika Mashariki na Kati (ECASSA) Dk Irine Isaka, anasema tatizo la mitazamo sio tu ni mzigo wa vyuo vikuu, bali ni mlolongo unaoanzia nyumbani katika malezi ya kila siku ya watoto.

“Wazazi wengi wamewaacha watoto wao kwa wahudumu wa nyumbani. Hivyo walikaa na kusubiri kila kitu waletewe, hivyo kuwadhoofisha katika suala la motisha katika kazi na ushirikiano.Ili kukabiliana na changamoto hizo za kimaadili na kutoa fursa kwa vyuo vikuu kujenga uwezo mwingine wa kitaaluma, jamii nzima inapaswa kuwaandaa vijana katika masuala yanayohusu kazi,’’ anaeleza.

Anaaongeza: “Lazima tuwaambie wasitegemee kuajiriwa na baada ya miezi mitatu wanataka kuwa mameneja, baada ya miezi sita wanakuwa wakurugenzi. Hii ndiyo changamoto kubwa, pamoja na uvivu pamoja na visingizio vingi.’’ Mkurugenzi Mtendaji wa Superdoll Tanzania, Seif Ali Seif anasema wahitimu wa Tanzania wanakidhi umahiri unaohitajika katika soko la ajira, ila wanakosa sifa muhimu inayochangia sehemu kubwa ya mahitaji ya waajiri.

Hali hiyo anasema imeilazimu kampuni yake kutengeneza programu maalum kwa wahitimu, inayolenga kuwabadilisha kutoka kuwa wahitimu wa kawaida hadi kuwa wataalamu.

“Kuna pengo kubwa la ujuzi miongoni mwa wahitimu wengi. Ni changamoto kubwa inayotulazimisha kuwapa mafunzo upya kabla ya kufanya kazi. Hii ni changamoto ambayo kwa pamoja tunaweza kuondokana nayo.

“Tumetengeza programu maalum za kuwanoa waajiriwa wanaotoka vyuoni kuwa watalaamu. Huu ni mwanzo tu na tuko tayari kutoa ushirikiano, huku tukilenga katika kujenga uchumi wa nchi yetu na kusaidia ajenda ya Serikali ya kutengeneza nafasi za ajira milioni nane ifikapo mwaka 2025,” anasema Seif.

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa William Anangisye anasema hiyo ni moja ya ajenda za chuo hicho kwenda nayo katika miaka 60 ijayo ya kutoa elimu bora na utafiti ili kuongoza vyuo vingine kimfano, na kuhakikisha kuwa wanafunzi wanakuwa na sifa zote muhimu za kuajiriwa kabla ya kuhitimu.

“Tungependa sasa taasisi yetu iwe sehemu ya utatuzi wa matatizo yanayowakabili Watanzania. Hili ndilo linalotutia wasiwasi na kutufanya tusogee haraka kutafuta ushirikiano huu wa karibu.

“Naamini tutakapofanya nao kazi (viwanda), yatatokea makubwa ambayo yangekuwa na manufaa kwa Watanzania wote, kwa sababu lengo letu ni kuona tunachofundisha kinakuwa muhimu kwa wanafunzi wetu,” anaeleza Profesa Anangisye.