Wazazi watakiwa kuwakagua watoto kubaini ukatili

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Moshi Mjini,Faraji Swai akizungumza na wananchi katika viwanja vya Njoro.Picha na Florah Temba

Muktasari:

  • Ili kukabiliana na vitendo vya kikatili kwa watoto vilivyokithiri katika jamii, wazazi wametakiwa kuwa karibu na watoto wao na kuwakagua, kwa kuwa wengi wamekuwa waoga kueleza vitendo vya kikatili wanavyofanyiwa.

Moshi. Jamii imetakiwa kurejea kwenye utamaduni wa zamani wa wazazi kukaa karibu na watoto wao, ili kukabiliana na changamoto ya vitendo vya kikatili ikiwemo ubakaji na ulawiti kwa watoto.

Rai hiyo imetolewa leo Ijumaa Februari 3, 2023 na Mwenyekiti wa CCM, Wilaya ya Moshi Mjini mkoani Kilimanjaro, Faraji Swai wakati akizungumza na wananchi kwenye maadhimisho ya miaka 46 tangu kuzaliwa kwa chama hicho yaliyofanyika katika viwanja vya Njoro.

Swai amesema vitendo vya kikatili vimekithiri katika jamii na ili kukabiliana na tatizo hilo, wazazi wanapaswa kuwa karibu na watoto wao na kujenga utamaduni wa kuwakagua na kuwachunguza.

"Wazazi kuweni karibu na watoto wenu, kwani vitendo vya ukatili kwa sasa vimekithiri katika jamii.

“Tengenezeni utaratibu wa kuwakagua na kuwachunguza mara kwa mara, kwani wengi wao wanafanyiwa vitendo vya ukatili na kutokana na uoga hawawezi kusema kwa kuhofia vitisho wanavyopewa na wahusika," amesema.

Aidha kiongozi huyo amewaonya wanachama wanaoeneza majungu, uzushi na uongo juu ya mtu au watu kwa maslahi yao binafsi na kueleza kuwa watakaobainika watachukuliwa hatua kali.

"Hatutakubali kuona mtu au watu wakikirudisha nyuma chama kwa kutengeneza majungu na kusambaza uzushi na uongo dhidi ya mtu au watu kwa maslahi yake binafsi, hatutasita kuwachukulia hatua kali kwa mujibu wa miongozo na kanuni za chama,” amesema.

Kwa upande wake Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi Mjini, Ibrahimu Mjanakheri amesema katika kipindi cha miaka miwili, Serikali imetoa zaidi ya Sh5.8 bilioni kwa Manispaa ya Moshi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Ametumia pia nafasi hiyo kuishauri serikali kuona umuhimu wa kutoa mikopo ya vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, inayotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri kwa mtu mmoja mmoja badala ya vikundi.

"Tunaishauri Serikali, mikopo hii ya asilimia 10 kwa vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, itolewe kwa mtu mmoja mmoja na si vikundi, kwani ipo tija ya kumsaidia mtu mmoja, mmoja kwa kuwa kila mtu ana jambo lake," amesema.

Awali mkutano huo ulitanguliwa na ukaguzi wa miradi ya maendeleo, upandaji wa miti, kufanya usafi pamoja na kutembelea wazee.