Wafanyabiashara Kibaha walia wingi wa kodi

Mkuu  wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge akizungumza kwenye mkutano wa Baraza la Wafanyabiashara Mkoani humo leo. Picha na Sanjito Msafiri

Muktasari:

  • Baadhi ya wafanyabiashara mkoani Pwani wamelalamikia mrundikano wa kodi wakitaka Serikali izipunguze ili kuboresha biashara zao.


Kibaha. Wafanyabiashara mkoani Pwani wameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kupunguza mrundikano wa tozo na kodi mbalimbali zinazotozwa kwa sasa hali itakayowawezesha kufanya shughuli zao kwa tija.

Wametoa ombi hilo leo Ijumaa Februari 3, 2023 wakati wa baraza la biashara la Mkoa huo lililofanyika Mjini Kibaha.

"Kodi ni nyingi sana kuna TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania), Halmashauri watu wa Zimamoto, Osha (Mamlaka ya Afya na Usalama Kazini) watakuja.

“Bado utadaiwa umeme, ankara za maji na kodi ya fremu hivyo unajikuta huna kitu," amesema Abdallah Ndauka.


Ndauka ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabishara Mkoani Pwani, amesema kuwa changamoto iliyopo ni mamlaka za Serikali kutoangalia chanzo cha kufa mitaji kwa wajasirimali na badala yake wanajikita kwa wanao anzisha biashara.

Kwa upande wake Rwehumbiza Peter amesema kuwa asilimia 10 ya tozo wanayotozwa na Halmashauri kwenye nyumba za kulala wageni limekuwa likiwaumiza lakini anaona faraja inanukia baada ya kusikia liko mbioni kuondolewa.

"Tumekuwa tukikatwa asilimia 10 kwa sisi wamiliki wa nyumba za kulala wageni, hilo limekuwa likituumiza sana lakini leo nimesikia kuwa Serikali iko mbioni kulifanyia kazi nashukuru," amesema.

Naye Charles Zakaria ameiomba Serikali kuweka mpango utaokawezeha mifuko ya pesa inafanya kazi kwa vitendo hasa kusaidia wafanyabiashara mitaji tofauti na ilivyo sasa kwani imekuwa vigumu kuwanufaisha jambo ambalo limekuwa likiwasukuma kukimbilia kwenye mabenki ambako wanaumizwa na riba kisha kukata mitaji.

Mwenyekiti wa Mkutano huo ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge amewataka watumishi waliopewa dhamana ya kuwasaidia wafanyabiashara hao kutosubiri waletewe vilio hivyo ofisini na badala yake wawatembelee wajasiliamali hao ili kujua vikwazo vinavyowakabili na kuvifanyia kazi.

Kunenge amesema kuwa Serikali ya sasa imejikita kutatua changamoto za wananchi katika nyanja mbalibali na ili kutimiza hilo ni vema watendaji wa ngazi zote wakawa wepesi wa kufanya kazi.