Sh5.4 bilioni kuboresha barabara mlimani Ludewa

Meneja wa Tanroad Mkoa wa Njombe Ruth Shaloah wakwanza kushoto akisoma taarifa ya ujenzi wa barabara eneo la Mlima Kimelembe Wilayani Ludewa Mkoa wa Njombe.

Muktasari:

  • Zaidi ya Sh5.4 bilioni zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara eneo la Mlima Kimelembe wilayani Ludewa Mkoa wa Njombe.

Ludewa. Serikali yatenga 5.4 Bilioni kwa ajili ya ujenzi wa barabara eneo la mlima Kimelembe kufuatia mtelemko na kona kali zilizopo katika mlima huo.

Hayo yamesemwa leo Februari 3, 2023 na Meneja wa Wakala wa Taifa wa Barabara Tanzania (Tanroads) mkoani Njombe, Ruth Shaloah wakati akitoa taarifa ya ujenzi wa barabara eneo la mlima huo mbele ya Kamati ya Siasa mkoa huo.

Shaloah amesema fedha hizo zitakwenda kupunguza kona kali za mlima huo kwani usanifu wa ujenzi wa barabara kwa eneo hilo ushafanyika na sasa wapo hatua ya manunuzi.

Ameongeza kuwa ujenzi wa eneo hilo la barabara utafanywa na wakandarasi wawili ili kurahisisha kazi kutokana na umuhimu wa barabara hiyo.

“Ujenzi wa barabra eneo hili la mlima Kimelembe utafanywa na wakandarasi wawili ili kazi ikamilike mapema na kuwarahisishia wasafirishaji wa makaa ya mawe na wasafiri wengine,” amesema Shaloah.

Kwa upande wake Mbunge wa Ludewa, Joseph Kamonga amesema kukamilika kwa ujenzi wa barabara mlima Kimelembe ni neema kwa Wanaludewa.

“Huu mlima umekuwa chanzo cha ajali zinazosababisha magari kutumbikia bondeni kutokana na kona na mtelemko mkali na wananchi wamepoteza maisha kwenye huo mlima na wengine wamepata ulemavu, hivyo kuja kwa fedha hizi ni neema kwetu Wana-Ludewa,” amesema Kamonga.

Ameongeza kuwa kukamilika kwa ujenzi wa eneo hilo kutaongeza chachu ya uwekezaji kufuatia rasilimali ya makaa ya mawe na ziwa Nyasa kuwa upande wa Mlima.


“Uelekeo wa Mlima huu mbele yake kuna rasilimali ya makaa ya mawe na pia kuna bandari yenye meli pale Manda.

“Meli ile inatakiwa iwe inapata mizigo kutoka ukanda wa huku juu hivyo kukamilika kwa ujenzi wa mlima huu kutasaidia kusafirisha bidhaa mbalimbali kwenda Malawi na Tarafa ya Mwambao,” amesema Kamonga.

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Njombe, Deo Sanga (Jah People) amewataka wananchi wa Kata ya Nkomang’ombe kujiandaa na fursa za kibishara zinazo kuja na uwekezaji wa makaa ya mawe baada  ya kukamilika kwa ujenzi wa barabara hiyo.